Ujumbe wa Mwinjilisti Temba wagusa watumishi wengi wa Mungu

NA DIRAMAKINI

WATUMISHI mbalimbali wa Mungu wamempongeza Muhubiri na Mwinjilisti wa Kimataifa wa Kanisa la Penuel Healing Ministry la Ubungo Kibangu jijini Dar es Salaam,Alphonse Temba kwa ushauri alioutoa kuwa,watumishi wa Mungu waache kuwaelemea washirika badala yake wachangamkie fursa za uwekezaji ikiwemo kununua ardhi kwa mipango ya sasa na baadae.

Temba ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Redio Penuel iliyopo mkoani Kilimanjaro amesema,mtumishi yeyote wa Mungu ambaye anaifikiria kesho njema kwa ajili ya kulihubiri neno la Mungu, hawezi kubweteka kwa kusubiria sadaka na mafungu ya 10.

"Nataka nizungumze sauti hii leo kwa watumishi wa Mungu, maandiko tangu mwanzo wa uumbaji mpaka mwisho yamenena mambo mengi, na yamejirudia kwa kila kiwango cha ufahamu wa ki-Mungu kwa uelewa wa mwandamu.

"Katika kila kizazi, tunamuona Mungu kwa kiwango kikubwa, kwa kifupi sana ninataka nitoe taarifa fupi ikusaidie, tunamuona Mungu baada ya uumbaji katika Mwanzo 1, tunamuona Mungu hatimaye anamkabidhi Adamu na Hawa, mwanzo kabisa Adamu anakabidhiwa ardhi ya bustani huku akimpa masharti aitunze na kuilima.

"Point yangu ni watumishi wengi wa Mungu wanaamini Mungu atatumia watu kuwabariki, ndiyo maana tunapokea sadaka, mafungu ya kumi na sadaka nyingine mbalimbali.

"Kadri watumishi wanavyofunguliwa na wanavyoamini neno la Mungu kwa mfano malimbuko wengi wanaita mbegu, wengine sadaka za hiari, sadaka za ujenzi, sadaka za uijilisti na nyinginezo.

"Watumishi wa Mungu hizo dhana zimebadilika, wakati wazee wetu baada ya uhuru, Lazaro na Mzee Kulola na wengine wengi waliokuwa wakihubiri miaka ile na ukarimu na kadhalika kwa wananchi na kumtafuta na kumtumikia Mungu kwa wakati ule kumekuwa tofauti na hii karne ya 21.

"Ambayo pamoja na kwamba neno halibadiliki, maisha ya watu, ufahamu wa watu unabadilika ndiyo maana leo hii unaweza kuona kabisa watu wana changamoto kubwa sana za kiuchumi katika maisha yao na unajikuta kwamba wachache sana wana ule ufahamu.

"Wa kupambana pamoja na mambo ambayo wanayapitia wamkumbuke Bwana, hivyo basi ni wakati wa kuishi kama Paulo alipofika mahali sasa akaamua kufanya kazi ya mahema ili injili isitukanwe, ili injili isiwaelemee watu.

"Watumishi wa Mungu tusiwaelemee washirikka kwa kusema yatakuja mafungu ya kumi na sadaka na malimbuko, matokeo yake tunatabiri uongo au kutia moyo za uongo, au kuhamasisha watu kwa kuwapenda kwa sababu tu ya kupata kipato.

"Tusifike huko na kila mtu ana neema yake, lakini iko neema moja tunayo sote ya kuwekeza hata sisi binafsi kwa sababu maandiko yanasema kwamba, mzazi mzuri ni yule anayempa mwanaye, mjukuu anayemrithisha mjukuu.

"Anayemrithisha mjukuu urithi, mtoto na kadhalika, watu wa Mungu Kwala Dry Port (Bandari Kavu ya Kwala) itakwenda kuwa eneo si la kawaida, Kwala Dry Port linaenda kuwa eneo si la kawaida, linaenda kuwa eneo la viwanda zaidi ya 200, Wachina wameshafika zaidi ya asilimia 50 ya ujenzi.

"Kutakuwa na watu zaidi ya milioni 1 watakaofaidika direct na indirect kwa hizo kazi, lakini kule maeneo bado ni bei chini sana, heka ni bei chini sana,"alifafanua Mwinjilisti Temba.


WATUMISHI

Kwa nyakati tofauti watumishi wa Mungu wamesema, Mwinjilisti Temba amekuwa mshauri mwema si tu kwa huduma za kiroho bali hata kijamii, kisiasa na kiuchumi.

"Ndugu Temba ni miongoni mwa watumishi wachache sana wa Mungu ambao wana shauku ya kutaka kuona kila mmoja anafanikiwa au anapiga hatua kupitia huduma anayoisimamia, si hivyo tu hata katika kijamii tunaona namna ambavyo anasaidia wengi tena kimya kimya.

"Kwa hiyo, ushauri huu wa Mwinjilisti Temba kwangu kwanza nimeufurahi, pili mimi mwenyewe ninakwenda kuufanyia kazi maana nimekuwa na huduma hii ya kanisa kwa miaka 17 sasa, sijapata mafanikio yoyote.

"Waumini ambao ninawategemea hawawezi kunifanya nizifikie ndoto zangu kiuchumi na kuifanya huduma hii kupanuka zaidi, hivyo ninaangalia namna ya kwenda kuwekeza katika ardhi hata nisipojenga kwa sasa basi ninaweza kujiingiza katika kilimo,"amesema mmoja wa Manabii kutoka Chanika katika Halmashauri ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam.

Mtumishi mwingine amesema, "....pia nimejifunza kuwa Mungu anaweza kutumia njia ambayo hujaitarajia kuweza kukubariki nje na madhabahuni.Kwa sababu, nina muda mrefu natumika, lakini kiuchumi sioni matokeo makubwa.

"Japo sijawahi kuwaza kufanya uhuni wa ku-manipulate watu ili nipate pesa, So nimeendelea kujengeka kiimani,kuwa ni vyema kuendelea kusimama na ukweli ,ipo siku Mungu atafunguwa njia,"amefafanua Mtumishi mwingine.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kitaifa ya Maaskofu na Mashekhe ya Maadili,Amani na Haki za Binadamu kwa Jamii ya Madhehebu ya Dini nchini, Askofu William Mwamalanga amesema,Mwinjilisti Temba amezungumza mambo muhimu kwa lugha laini ya ualimu ambayo kila mtu akijifunza atasonga mbele.

"Temba ametumia lugha iliyojaa mafundisho laini, lakini mafundisho ya kweli kabisa, hebu niseme kuwa ametolea mfano wa Dar es Salaam, ukitoa mfano wa Dar es Salaam ukitembea miji mingi Tanzania watumishi wa Mungu wenye mfano wasiolemea watu wengine unawakuta vijijini ambako wanalima wao, wanafanya kazi ya kilimo na kufuga na wengine kwenye madini.

"Na kazi yao ya huduma ambayo Mungu amewaita unaona inakuwa njema hilo nimethibitisha na kuona watu wengi, kama anavyosema mtu wa Mungu Temba hapo, shetani anachokifanya anatumia sifa za uongo, watu wa Mungu wengi wanatumia uongo utaona wamejibamba majina mengi wanajiita Senior Bishop, Senior Pastor. Manabii na siku hizi kuna muungano wa manabii wanakutana.

"Lakini kwenye mji kama Dar es Salaam utaona manabii wengi wa leo ni wale wanaojipendekeza kwenye Serikali, kwa viongozi wanaojipendekeza pendekeza wanaitwa itwa, wananunuliwa gari na washirika, angalia watu wanaowanunulia gari unaweza kuona wengine hata kwa wanasiasa wanaingia huko wanahimiza mafundisho yao ya ajabu ajabu kabisa.

"Wana mafundisho ya ajabu kabisa ya kuwaloga watu, watu kwa sababu ya shida unataona wanamiminika leo ni siku ya kupewa hela wanakimbilia huko. Hata mafundisho ya msingi ya kumfundisha neno mtu la utakatifu hawajui, kwa hiyo huyo mtu anakwenda hivyo.

"Anatafuta hela kwa maji hayo, chumvi hizo wengi wanakaa hapo kama wameshakuwa watumwa wamelogeka, lakini cha pili uvivu wa watu wa Mungu umepelekea wabakie hivyo na kuhimiza tu sadaka.

"Migogoro mingi ipo huko wanafikiri ndio maisha ya Mungu. Pia wanahimiza tu sadaka, Uongo mwingi wa shetani unatekelezwa na watu wa Mungu kuliko upagani.

"Na hata maombi hawana na hata kuomba hawajui namna gani ameomba kimekuwa hiki anafikiri nimeomba na hata maombi yenyewe mtu anasema nimefunga ni wiki mbili sasa, lakini hakuna kitu.

"Temba umesema mambo muhimu sana sijapata kuona, na kama mafundisho hayo ndiyo yangekuwa tunafundishana ingekuwa rahisi sana, juzi tu nilikuwa nawaambia watu Dodoma kuna miradi ya Serikali ya BBT, nikawaambia kanisa lazima wote miradi ya wakopeshane hizo fomu.

"Kuna mtu amekuja amesema Askofu kuna fomu hizi, siri kwa siri wanapelekana kwenda kuchukua hela tena hizo milioni 5 hazina riba nikawatoa vijana wote nikawaambia nendeni na ndugu zenu waleteni kina mama na vijana kwa siku mbili vijana 2,800 na 3,002 hivi tayari wamechukua fedha hizo milioni tano tano wako na biashara zao kwa sasa.

"Watanzania hawa wote sasa yaani ukiwa CCM unachukua nimewaambia kwa nini vijana msiwe na ajira, mimi nawafundisha vijana namna ya kupigana vita bila jasho au silaha yoyote leo wako wamejaa."

"Eti vijana wanasema wa CCM wanachukua na mimi nikawaambia nendeni mkachukue mbona wanafanikiwa yaani watu wanafundishwa hata maarifa hamna umefikaje Dar es Salaam, wakati mmoja tuliwaza tuanzishe radio na gazeti Dar es Salaam ilifikia wapi? Iliishia kudhulumiwa tu basi hakuna watu wanaofundisha Mungu ni roho, lakini mwili ni mwili unahitaji mwili kupata kwa ajili ya roho nzuri.

"Na ndio maana sasa unaona watu hawawezi kuwa watu wazuri, nimesikitika Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam nimemsikia akisema huko Dar es Salaam watu waliokutwa wanaimba kwenye kwaya, lakini anawakuta kwenye madanguro wanajiuza ni Wakristo lakini wamekwenda huko.

"Unakuta anaomba msamaha anatoa hadi hela anajitetea utashangaa ni Wakristo, kwa hiyo kuna kitu ambacho kanisa lilishwa likifikiri hasa ndio imani ya mbinguni kumbe ni imani ya kishetani.

"Mtume Paul anasema mkiona mtakapoanza kuitwa mimi wa Temba, Petro mjue ya kwamba mmeingiliwa.

"Kanisa la kwanza halikuwa hivyo, Kanisa la agano jipya sio hili sijui ni takataka gani hata mimi huwa nashangaa watu hawana upendo, watu hawapendani yaani mtu anasema mimi ndio Nabii Mkuu, mbingu ya Nabii Mkuu wapi na wapi?.

"Mimi Nabii wa mkoa mimi nabii wa kule, ni aibu aibu tu angalau mngefundisha watu wawahudumie watu, nimeona mkoa mmoja mtu anakwenda anawapa watu mitaji basi kama ndio hivyo jina la Bwana libarikiwe, ndio maana tunaona vyeo vya kiaskofu vinavyogombaniwa.

"Vimerudi kwenye dini zile zile maaskofu wenzetu wa dini zile hawalimi wala hawapandi kazi yao usulatani yeye ni kwenda huko huko, lakini wana mtaji na wanashika maeneo makubwa wana miradi mikubwa ni dini kubwa ile ile.

"Sembuse mimi na wewe umepata tu muujiza yaani mgonjwa kupona unafikiri hiyo ni ibada, kilema kutembea unafikiri hiyo ni ibada. Kazi ya Yesu sio toka pepo kila siku.

"Mwaka mmoja Kikwete akiwa Rais alikwenda Mbeya TAG kwenye kutimiza miaka 75 wakamwanbia azindue kitabu, Kikwete akashangaa miaka 75 mnazindua kitabu kimoja tu cha kanisa, nilimsifu sana Kikwete akasema basi nendeni Dodoma mkatoe yale mapepo bungeni yanatusumbua sana kwa dharau kubwa kabisa,sasa nini maana yake kama una akili za mbinguni unaona kichefu chefu...

"Neno la Mungu linafungua mambo mengi, Mungu amesema kwa nini Yesu akasema tafuteni kwanza ufalme wa Mungu na ahadi yake, hiyo ni kanuni muhimu sana, Yoshua 24 ukisoma utaona, Mungu anawaambia nini wana wa Israeli,hawa Israeli wametoka kwenye mpango wa Mungu ambao ulikuwa kuwalea tu ukigusa kidogo vitu vipo.

"Wakati mwingine watu walikuwa na mpango kuninunulia gari nikasema msingi wangu sio ninyi mninunulie gari, Mungu ataninunulia gari.

"Mimi nitawanunulia ninyi, nawaambia watu gari sio kitu cha kukipenda ukiwa na ardhi mtu wa Mungu mtu yeyote ujue kabisa wewe ni trilionea, usikimbilie vijana kwenda mjini.

"Nawaambia kabisa Mungu anawaandalia watu watatu au wawili, kanisa la Mungu halianzi na maelfu ya watu kanisa la Mungu linaanza na mtu mmoja ukidumu na watu hata watatu au wanane usidhani kuwa wewe sio mtu wa Mungu hubiri na hao watu na watoto wao, wake zao ndio maana anasema anatafuta watu wawili mtu yule yukoje huyo Mtu?.

"Ukija kwa manabii wa uongo mitandaoni wamejazana, wanatabiri tabiri, shetani anawaendesha kweli kweli huwezi kusema nataka Rais afe Waziri Mkuu afe, wakifa utapata nini wewe? watu wa Mungu ukiwarejesha kwenda kwenye mateso ya kanisa wakati wa Herodia kwenye Matendo ya Mitume 12 watu hawajui silaha za kupigana vita hawazijui kabisa utasikia maneno yao ya kiburi tu.

"Sio waombaji, lakini ashukuriwe Mungu wapo waombaji Tanzania hapa wanajua kusimama na Mungu sio wababaishaji, sio waongo waongo wanafiki, au wajuaji juaji wametulia wana biashara, wanamashamba na wanamwangalia Mungu.

"Upendo unaousema sio lazima wote tuwe na pesa nyingi, lakini tungeshikamana kwa pamoja tukaacha ubinafsi, hakuna aliyesema wakati ule kitu hiki ni chake pekee wote walifanikiwa wakawa pamoja. Kanisa la kwanza walikuwa na upendo baada ya ushindi ule wa Herodia utaona kanisa lilivyofurahi.

"Kwa hiyo kama kanisa hatuna upendo, Temba umejaliwa sana kuwa na upendo, kuwaambia watu wa Mjini nimekuona sana ukifundisha injili Mkoa wa Pwani na Mungu amekupa neema hiyo kuhubiri watu injili tena wanakupa hadi na ardhi wanakulimia mpunga wenyewe.

"Huwezi kuacha kuwa tajiri, kwa mtaji wako umewapa kina mama wale wanafurahi sana, wanasema huyu mtu tunampa gunia 10, hawa watu lazima watafika mbali.

"Injili za uongo Mjini zimewadanganya watu hasa kina mama, wanaume wao wamekuwa wepesi kugundua, kwa hiyo tuendelee kufundisha upendo na injili ya kweli, injili za uongo Mjini watu wameathirika sana, umesema sana neno.

"Leo ndio maana watu wanadumbukia kwenye injili hizo. Tupendane kama Yesu anavyosema akaulizwa torati ni nini? Mpende Bwana Mungu wako kwa Moyo wako wote na kwa akili zako zote na ya pili yafanana na hii Mpende jirani yako Kama unavyojipenda Mwenyewe huwezi kuona jirani yako hana hata nguo ukaacha kumsaidia.

"Utakuwa Mchungaji gani unatembelea Prado la milioni 200 wengine wana mahama halafu sadaka zile wanachanga watu ndio za kuwekea mafuta jamani tumwogopeni Mungu.

"Wana pesa nyingi, na kiburi hapo hapo utafikiri lakini huskii wamezalisha popote, kwa ajili ya watu wasio na uwezo na wengi wamechangiwa pesa wamejenga mahoteli makubwa.

"Lakini watu wanaotoa hizo pesa wanapanga Manzese biashara kwenye magunia ambapo tulitakiwa tusikie mimi ningechukua ghorofa kwa ajili ya kina mama. Tuombe Mungu alete uamsho mwingine kabisa kwenye Taifa hili,"amefafanua kwa kina Askofu William Mwamalanga.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news