VITA GAZA:Mtanzania Clemence Felix Mtenga afariki nchini Israel, wizara yatoa pole

DODOMA-Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imeeleza kupokea kwa masikitiko na huzuni taarifa inayothibitisha kifo cha Bw. Clemence Felix Mtenga.

Kijana huyo wa Kitanzania ni miongoni mwa Watanzania wawili ambao pamoja na raia wa mataifa mengine walikuwa hawajulikani walipo tangu yaliyopotokea mapigano Oktoba 7, 2023 nchini Israel na katika maeneo ya Wapalestina hususani Gaza.

Hayo ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Novemba 17, 2023 na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia wizara hiyo ambayo imefafanua kuwa, marehemu Clemence alikuwa ni miongoni mwa vijana wa Kitanzania wapatao 260 waliokwenda nchini Israel kushiriki mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vitendo chini ya Mpango wa Ushirikiano kati ya Serikali ya Tanzania na Israel.

"Tayari wizara imechukua hatua stahiki ikiwemo kuijulisha familia na inaendelea kuwasiliana na Serikali ya Israel kuhakikisha kwamba taratibu za kuurejesha mwili wa marehemu nchini kwa ajili ya mazishi zinakamilika kwa wakati.

"Aidha,wizara inaendelea kufuatilia taarifa za Mtanzania mwingine ndugu Joshua Mollel ambaye bado hajulikani alipo tangu yalipotokea mashambulizi hayo.

"Wizara inatoa pole kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki pamoja na Watanzania kwa ujumla kwa msiba huu. Vilevile, Wizara inapenda kuuhakikishia umma pamoja na Diaspora wa Kitanzania ikiwemo wanafunzi waliopo masomoni nchini Israel kuwa, Serikali kupitia Ubalozi wake uliopo Tel Aviv, Israel, itaendelea kuwasiliana na mamlaka za Israel ili kuhakikisha Watanzania wote waliopo nchini humo wanakuwa salama wakati wote,"imefafanua sehemu ya taarifa hiyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news