Vyombo vya habari tusiwaache DCEA wenyewe mapambano dhidi ya dawa za kulevya-Dkt.Rioba

NA GODFREY NNKO

MKURUGENZI Mkuu wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC), Dkt.Ayub Rioba Chacha amevitaka vyombo vya habari nchini kushirikiana bega kwa bega na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ili kuweza kutokomeza dawa hizo ambazo zina madhara makubwa katika jamii na uchumi.

“Media ina sehemu yake kubwa katika jamii, tusiwaache (DCEA) wenyewe maana si kazi rahisi;
Ameyasema hayo leo Novemba 14, 2023 jijini Dar es Salaam katika siku ya pili ya semina kwa wahariri wa vyombo vya habari iliyoratibiwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA).

Dkt. Rioba katika semina hiyo alikuwa akiwasilisha mada ambayo iliangazia juu ya nafasi ya vyombo vya habari katika kupambana na dawa za kulevya.

“Hii kazi siyo rahisi, na tumeona ikifanyika ni juzi tu tumeona (DCEA) ikikamata watu fulani wakitengeneza biskuti za bangi.”

Amesema, licha ya dawa za kulevya kuwa ni tatizo la kihistoria,lakini jitihada za pamoja zinahitajika kuhakikisha watumiaji na wauzaji hawapati nafasi popote katika jamii.

“Hazikuanza leo huko Amerika ya Kusini dawa za kulevya limegeuka kuwa janga la kisiasa. Hivyo, si tatizo dogo linahitaji nguvu ya pamoja kudhibiti katika jamii.”
Amesema, lengo ni kujenga jamii imara na uchumi imara.mDkt.Rioba ametolea mfano huko Marekani ndani ya miaka 10 imetumia zaidi ya dola 1.6 biloni kwa ajili ya kupambana na dawa za kulevya, fedha ambazo zingeweza kuelekezwa katika miradi ya maendeleo kwa ustawi bora wa jamii.

“Utaweza kuona ni kiasi gani cha fedha kinatumika katika kudhibiti dawa hizo na ukubwa wa tatizo.”

Amesema, sababu za kutumia dawa za kulevya ni kuiga mambo kwa kuhisi ni ukisasa, kuiga watu mashuhuri, kushawishiwa na marafiki rika kijiweni.

“Ukiwa kijiweni ni rahisi sana kushawishika, na kushindwa kuhimili changamoto za maisha huku wengine wakifanya hivyo kwa ajili ya kutaka kujifurahisha kumbe wanapotea.”

Dkt.Rioba amesema, athari za dawa hizo ni Taifa kupoteza nguvu kazi, kuporomoka kwa maadili, kuongezeka kwa vitendo vya uhalifu na mengineyo.

“Fedha nyingi hutumika kupambana na kuzuia. Kwa sababu unapambana na watu wenye nguvu kweli kweli ya kifedha.”

Amesema, vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kuendelea kuandaa vipindi ambavyo vitatoa elimu kwa umma kuhusu dawa za kulevya.
“Kwa hiyo tushirikiane na vyombo kama DCEA ili kuhakikisha siku za mbeleni tunakuwa na Taifa la watu ambao si mazezeta.

“Media ikidhamiria inaweza, lakini changamoto iliyopo ni kuwa na uelewa na ujuzi mdogo wa kufuatilia habari za kiuchunguzi.”

“Tunahitaji sana ujuzi wa kufuatilia habari za kiuchunguzi, gharama za kufuatilia.Kwa sababu, mbinu za kibiashara huwa zinabadilika kila wakati.

“Wanahabari wapewe elimu kuhusu dawa za kulevya na habari za kiuchunguzi.Pia, vyombo vya habari vifanye uchunguzi kuweza kuwatambua wazungu wa unga, huwa wanakaa wapi.

“Tuwe na vipindi ambavyo vinatoa shuhuda za watu ambao walikuwa watumiaji wa dawa za kulevya, lakini wakaacha na sasa wanajishughulisha na mambo mengine, hiyo itakuwa elimu kubwa sana,”amefafanua Dkt.Rioba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news