Wanahabari tuzitumie kalamu zetu kusaidia mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia-Kenneth Simbaya

NA FRESHA KINASA

MKURUGENZI wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari nchini (UTPC), Kenneth Simbaya amewahimiza Waandishi wa Habari nchini kutumia taaluma yao kusaidia mapambano ya vitendo vya ukatili wa Kijinsia ambavyo vipo katika jamii.

Amesma kuwa, ushiriki wao ni muhimu sana na itasaidia kuvitokomeza vitendo hivyo na kuimarisha Usawa wa Kijinsia kwa ustawi bora wa Jamii na taifa kwa ujumla.

Kenneth ameyasema hayo wakati wa Uzinduzi wa kampeni maalumu ya siku 16 za kupinga Ukatili wa Kijinsia kupitia vyombo vya habari vya mitandao ya Jamii uliofanyika katika Ukumbi wa Flomi Hotel Mjini Morogoro.
Aidha, uzinduzi huo ulitanguliwa na mafunzo ya semina ya 'Usawa wa Kijinsia' yaliyoanza kuanzia Novemba 23, 2023, hadi Novemba 28, 2023, yaliyohusisha Waandishi 28 kutoka Klabu za Waandishi wa Habari hapa nchini.

Amesema kuwa, vitendo vya ukatili wa Kijinsia vipo kuanzia ngazi za familia hasa wamekuwa wakifanyiwa wanawake na watoto kwa kiasi kikubwa. Hivyo jukumu la wanahabari ni kuhakikisha wanaandika habari zinazotoa elimu ya madhara ya vitendo hivyo, ushiriki wa Jamii kupambana navyo na jinsi vinavyorudisha nyuma juhudi za maendeleo kuanzia katika ngazi ya familia Jamii hadi Taifa.
Amebainisha kuwa, nguvu na mchango wa vyombo vya habari ni mkubwa sana katika kuhakikisha vitendo vya ukatili wa Kijinsia vinaisha ikiwemo kuelimisha madhara ya mila na desturi kandamizi, madhara ya vitendo vya ukeketaji, mimba za utotoni, ukatili wa kisaikolojia, kingono, ulawiti na vipigo kwa wanawake na watoto ambao hasa wamekuwa waathirika wakubwa wa matukio hayo na baadhi yao kuwapa ulemavu.

"Ukatili unarudisha nyuma maendeleo, sisi Waandishi wa Habari tunapoona mambo yasiyofaa tunaowaji wa kukekea, kutoa elimu, kuibua mada na kueleza kwa Mamlaka na watunga sera hatua za kuchukua katika kuleta muunganiko chanya wa kuhakikisha kila mmoja anatekeleza kwa ufanisi mapambano hayo.
"Kampeni hii tumeizindua leo Novemba 25, 2023, mpaka kampeni hii mwisho decemba 10, 2023, tutakuwa tumepata zaidi ya watu 1000 ambao tutawafikia na kushirikiana nao kupinga ukatili. Waandishi tutumie taaluma yetu kuwapa Wananchi mambo ya kuzungumza juu ya kumaliza ukatili nini kifanyike na pia wanaofanya ukatili waibuliwe mbele ya vyombo vya sheria."amesema Simbaya.

Aidha ameahauri kwamba, kama taifa tunataka kuondokana na umaskini ni lazima kuwekeze kwa Watoto wa kike ikiwemo kuwasomesha ambapo wakisoma taifa na jamii imeshinda katika nyanja mbalimbali hivyo wawezeshwe na kuwekewa mazingira wezeshi kufikia ndoto zao .

Kwa upande wake Lilian Lucas Katibu wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Morogoro akizungumza katika uzinduzi huo kwa niaba ya Rais wa UTPC Deogratias Nsokolo amewataka wanahabari kutokata tamaa kuwasemea wanawake na watoto dhidi ya vitendo vya ukatili kwani wakinyamaza kimya matukio hayo yataendelea kuwepo.
Hilda Kileo Ofisa Programu wa UTPC amesema kuwa katika kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia kila siku litawekwa swali moja katika kurasa za mitandao ya Jamii za 'UTPC' na kundi la (Whatsapp) ambalo limeundwa kuwapa nafasi Wanahabari maeneo mbalimbali nchini kuunganisha nguvu zao za kutoa maoni kwa njia ya mjadala na kuchangia mada ili kuwezesha kupata suluhisho la kutokomeza vitendo vya ukatili wa Kijinsia.

"Nitumie fursa hii kuwaalika Wanahabari, Wadau na watunga sera kujadiliana masuala haya muhimu ndani ya siku hizi 16 kuwa na sauti moja itakayowezesha ushiriki wetu katika kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto,"amesema Hilda.
Siku 16 za kupinga ukatili wa Kijinsia huadhimishwa kila mwaka duniani kote ifikapo Novemba 25 hadi Desemba 10. Ambapo mashirika mbalimbali ya kiraia. Wanaharakati wa haki za binadamu, Wanahabari, watunga sera na Wananchi huwaleta pamoja kwa lengo la kupinga ukatili na kutetea haki za wanawake na watoto. Matukio mbalimbali ya utoaji elimu na mijadala ya Wazi na makongamano hufanyika.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news