Waziri Makamba awasili Uholanzi kwa ziara ya kikazi

THE HAGUE-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. January Yusuf Makamba (Mb.) amewasili Jijini The Hague, Uholanzi kwa ziara ya kikazi ya siku tatu kuanzia tarehe 13 hadi 15 Novemba 2023.
Pamoja na mambo mengine, Mhe. Makamba ataongoza ujumbe wa Tanzania katika Kongamano la Biashara na Uwekezaji Kati ya Tanzania na Uholanzi litakalofanyika tarehe 14 na 15 Jijini The Hague.

Aidha, pembezoni mwa kongamano hilo, Mhe. Waziri Makamba atapata nafasi ya kukutana na Waziri mwenzake wa Mambo ya Nje wa Uholanzi, Mhe. Kanke Bruins Slot. Kadhalika, Mhe. Makamba anatarajiwa pia kukutana na kufanya mazungumzo na Jumuiya ya Watanzania wanaoishi nchini Uholanzi (Tanzania Diaspora).
Waziri Makamba ameambatana na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Tausi Kida na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dkt. Daniel Mushi. Wengine wanaoshiriki kwenye ujumbe wa Mhe. Waziri ni Mabalozi na Maafisa Waandamizi kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki. Pamoja na Wakuu wa Mashirika mbalimbali Serikalini yanayotafuta ubia na mashirika ya Uholanzi.



Aidha ujumbe wa Waziri Makamba umehusisha wafanyabiashara 16 kutoka sekta binafsi za Tanzania ambao watashiriki kwenye kongamano hilo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news