DODOMA-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wathamini wote wawe waadilifu, wenye weledi na wazingatie miiko ya taaluma katika kazi zao za kila siku.
Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa wathamini ni watu muhimu katika kufanikisha mipango ya maendeleo ya Taifa. “Mnapaswa kuwa waadilifu na kuzingatia thamani halisi ya ardhi, jengo au chochote kinachofanyiwa uthamini,” amesema.
Amesema hayo leo Novemba 9, 2023 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Nne wa Mwaka wa Wathamini unaofanyika kwa siku mbili katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma.
“Kazi ya uthamini si ya wababaishaji au vishoka, hivyo basi kila mthamini hana budi kuthamini na kuheshimu taaluma yake.”
Mheshimiwa Majaliwa amesisitiza kuwa: “Wapo baadhi ya wathamini ambao si waadilifu kwa kushirikiana na watendaji wengine hutoa makadirio ambayo hayawiani na thamani halisi. Vitendo hivyo husababisha kupoteza mapato ya Serikali lakini pia kuwanyima haki wale wanaostahili kupata haki.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa amewataka watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hususani wathamini washirikiane na sekta binafsi kufanya kazi za uthamini. “Tumieni fursa ya uwepo wa wathamini binafsi ili kutoa huduma bora na ya haraka hapa nchini, kufanya hivyo mtakuwa mnatekeleza maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya ushirikishaji wa sekta binafsi kwa maendeleo ya Taifa.”
Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wathamini hao watumie mkutano huo kufanya majadiliano ya kina kuhusu masuala ya taratibu za utwaaji ardhi na sheria zake, ukokotozi wa fidia katika maeneo ya madini, viwango vya thamani ya ardhi na mazao, changamoto za kisera za utwaaji ardhi pamoja na kupata suluhu ya malalamiko ya wananchi.
Naye, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geoffrey Pinda amesema kuwa uthamini wa fidia ni ufunguo wa maendeleo na mabadiliko chanya ya kiuchumi kwa kuwa unawezesha wawekezaji kupata ardhi na kuwekeza mitaji yao.
Amesema kuwa Wizara kwa kushirikiana na Bodi ya Usajili wa Wathamini nchini imejipanga kuhakikisha shughuli zote za uthamini zinaboreshwa. “Wizara itasimamia upatikanaji wa huduma hii kwa wananchi kwa wakati, kutatua kero mbalimbali za wananchi katika eneo hili la fidia na kuwezesha Bodi kuwachukulia hatua kali wale wote wanaohujumu shughuli za uthamini nchini.”
Amesema kuwa uthamini hufanyika na kuwezesha upatikanaji wa ardhi itakayotumika kwa ajili ya matumizi ya umma, kuweka miundombinu ya msingi, huduma za jamii, viwanda na kupanga makazi.