WAZIRI MKUU AZINDUA MRADI WA UMEME VIJIJINI SONGWE

SONGWE-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amezindua mradi wa usambazaji umeme vijijini na vitongojini utakaogharimu sh. bilioni 5.2 na dola za Marekani milioni 10 ambao unatarajiwa kusambaza umeme katika vitongoji 171 vya wilaya za Mbozi, Ileje, Momba na Songwe.

Uzinduzi wa mradi huo unaotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umefanyika leo Ijumaa, Novemba 24, 2023 katika kijiji cha Ivugula, kata ya Mahenje, wilaya ya Mbozi, mkoani Songwe.
Akizungumza na wakazi wa kijiji hicho, Waziri Mkuu amesema uzunduzi huo ni kiashiria kuwa kazi ya kupeleka umeme vijijini inaendelea. “Hatua hii ni kutekeleza dhamira ya Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kutaka kila nyumba ya Mtanzania iwake umeme,” alisema.

Akitoa taarifa ya Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili Mzunguko B (REDPIIB), Mkurugenzi wa Mipango na Utafiti wa REA, Mhandisi Godfrey Chibulunje alisema mradi huo unalenga kupeleka umeme katika vitongoji ambavyo havina umeme ila vimepitiwa na miundombinu ya msongo wa kati wa umeme.

Alisema Wakala wa Nishati Vijijini unatekeleza miradi mitano katika maeneo tofauti ya mkoa huo ambayo ni REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili (REA III Round II); na Mradi wa Ujazilizi Fungu la Pili B (REDPIIB). Mingine ni Mradi wa Kupeleka Umeme katika Vitongoji (HEP); Mradi wa Kupeleka umeme kwenye migodi midogo na maeneo ya kilimo na Mradi wa Kupeleka umeme kwenye Vituo vya Afya na Pampu za Maji.

Alisema mkoa wa Songwe una vijiji 307 ambapo hadi sasa, vijiji 281 sawa na asilimia 91.5 vimepatiwa huduma ya umeme kupitia miradi mbalimbali ya umeme vijijini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news