Waziri Mkuu:Elimu ya lazima itakuwa miaka 10 badala ya saba kama ilivyo sasa

DODOMA-Serikali imefanya maboresho kwenye baadhi ya maeneo katika Sera ya Elimu na Mafunzo ili kutoa elimu ya ujuzi badala ya elimu ya taaluma pekee ambapo elimu ya lazima itakuwa ya miaka 10 badala ya saba kama ilivyo sasa.

Akitoa taarifa kuhusu maboresho hayo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema utekelezaji wa maboresho hayo utaanza mwaka 2027 sambamba na kufuta mtihani wa darasa la saba na badala yake kuanza kufanyika kwa tathmini darasa la sita kwa ajili ya kujiunga na elimu ya lazima ya sekondari.

Waziri Mkuu ameyasema hayo Novemba 2, 2023 wakati akitoa taarifa kuhusu kuidhinishwa kwa Sera ya Elimu na Mafunzo 2014, Toleo la 2023 na Mitaala ya Elimu Ngazi ya Elimu ya Awali, Msingi, Sekondari na Elimu ya Ualimu kwenye kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu bungeni jijini Dodoma.

Amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kubainika kwa changamoto mbalimbali zikiwemo, mfumo wa elimu kujikita zaidi kwenye elimu ya jumla na kukosa fursa za elimu na mafunzo kwa kuzingatia mahitaji na njia mbalimbali za ujifunzaji kutokidhi kulingana na mazingira.

Ametaja changamoto nyingine kuwa ni: “Mitaala kutokidhi mahitaji ya mabadiliko ya kiuchumi, kijamii, kisayansi na kiteknolojia, mfumo usio fanisi wa udhibiti na ithibati ya elimu na upungufu wa nguvu kazi. Changamoto hizo zilizaa hitaji la kuboresha sera yetu ya elimu ili kukidhi mahitaji ya sasa na wakati ujao.”

Akifafanua kuhusu maeneo yaliyoboreshwa kwenye sera hiyo ambayo tarehe ya uzinduzi wake itatangazwa baadaye, Mheshimiwa Majaliwa amesema: “Sera ya Elimu na Mafunzo imefanyiwa mabadiliko kwenye maeneo kadhaa ikilinganishwa na sera iliyopita kwa kuongeza fursa za elimu ya amali (elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi) ambayo itaanza kutolewa kuanzia kidato cha kwanza.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema elimu ya ualimu nayo itaanza kuanza kutolewa kwa wahitimu waliomaliza kidato cha sita na kuendelea. “Mafunzo ya ualimu yatajumuisha mwaka mmoja wa mafunzo chini ya uangalizi (internship) baada ya kuhitimu mafunzo tarajali (Pre-service training).”

Amesema maeneo yaliyoboreshwa ni katika mfumo wa upimaji na tathmini ambao utazingatia mahiri zinazohitajika kwa kila ngazi kwa lengo la kuwa na upimaji endelevu na matumizi ya mbinu mbalimbali za upimaji na tathmini ya maendeleo ya wanafunzi katika kujifunza.

“Serikali itatoa na kusimamia matumizi ya kitabu kimoja cha kiada kwa kila somo katika elimu ya msingi na Sekondari ili kufanikisha upimaji wa matokeo ya ufundishaji na ujifunzaji unaofanana pia Serikali itaweka utaratibu wa kubaini na kuendeleza wanafunzi wenye vipaji na vipawa mbalimbali.”

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Wizara yenye dhamana na elimu ina wajibu wa kuandaa mikakati na mipango ya sekta ikiwa ni pamoja na kutafuta rasilimali mbalimbali kwa ajili ya utekelezaji na kufanya ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa sera hiyo.

Aidha, Waziri Mkuu amesema Wizara yenye dhamana na TAMISEMI itakuwa na wajibu wa kuratibu na kusimamia Tawala za Mikoa zenye jukumu la kutekeleza sera kwa kutoa elimu na mafunzo katika ngazi ya awali, msingi na sekondari na Wizara yenye dhamana na Utumishi itahusika na upatikanaji wa rasilimali watu.

Waziri Mkuu ameongeza kuwa Wizara yenye dhamana na fedha itahusika na utafutaji na upatikanaji wa rasilimali fedha, Tawala za Mikoa zitasimamia utekelezaji wa sera na miongozo ya utoaji elimu na mafunzo kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa.

“Mamlaka za Serikali za Mitaa zitaendelea na utekelezaji wa sera na hivyo kutoa huduma za elimu ili kuwafikia walengwa wote. Katika kutimiza azma hiyo, Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi ikiwemo mashirika ya kidini, mashirika yasiyo ya Serikali na wadau wengine katika kuboresha upatikanaji na utoaji wa elimu na mafunzo.”

Amesema mgawanyo wa majukumu utafuata mifumo ya kitaasisi iliyojengwa kisheria na kwa kadri ya utaratibu wa Serikali. “Wizara yenye dhamana ya elimu pamoja na taasisi zake itaendelea kuwa na wajibu wa kusimamia, kuratibu na kuimarisha upatikanaji na utoaji wa elimu na mafunzo nchini.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news