SONGWE-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Songwe ambayo baadhi ya majengo yamekamilika na kuanza kutoa huduma.
"Nimekuja kuwahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuwahudumia katika sekta mbalimbali kama vile maji, elimu na afya;
Akizungumza na wananchi na viongozi walioshiriki uwekaji jiwe la msingi leo
Novemba 23, 2023, Waziri Mkuu amesema hospitali hiyo ni ya kimkakati kwani
inahudumia wagonjwa kutoka Malawi na Zambia.
Akitoa maelezo ya mradi huo, Mkandarasi Elekezi,Mhandisi Vedasto alimweleza Waziri
Mkuu kwamba baadhi ya majengo kama maabara na OPD yamekamilika na yameanza
kutumika.
"Jengo la Mama na Mtoto limefikia asilimia 54 ya utekelezaji, la EMD na ICU limefikia asilimia 80,nyumba ya mtumishi imekamilika na inatumika."
Alisema ili hospitali hiyo iwe imekamilika kwa mujibu wa taratibu za Wizara ya Afya,
inapaswa iwe na majengo zaidi ya 17 lakini hadi sasa majengo matano ndiyo yamejengwa na baadhi yanatumika.
Naye, Mganga Mfawidhi wa hospitali hiyo, Dkt. Juma Ramadhani Juma alisema hospitali
hiyo ina uwezo wa kulaza wagonjwa 60kwa wakati mmoja na ina uwezo wa kuhudumia
wagonjwa 80 kwa siku.
"Tumeshatoa huduma kwa wananchi milioni 1.3, tuna huduma za kibingwa za watoto,
macho, afya ya mama na uzazi na huduma za dharura. Ujenzi ulikamilika utawasaidia
wananchi ambao sasa hivi wanaenda umbali wa KM. 100 kupata huduma ambazo
hazipatikani hapa kwetu," alisema.
Hospitali hiyo ambayo ilianza kujengwa mwaka 2019, hadi sasa imeshatumia sh. bilioni
16.3 ambazo kati yake sh. bilioni 13.1 zimetumika kwa ujenzi na sh. bilioni 3.2 zimetumika kununulia vifaa tiba.