KIGOMA-Watu nane wamefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa vibaya kufuatia ajali ya gari ndogo aina ya Toyota Succeed yenye namba za usajili T890 DYZ iliyokuwa ikisafirisha abiria katika wilaya za Kibondo na Kakonko mkoani Kigoma.
Ni baada ya kugongana na gari nyingine aina ya Faw yenye namba T833 DUA mali ya Kampuni ya CHICO katika Kijiji cha Kamkugwa wilayani Kibondo mkoani humo.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma,Kamishna Jenerali mstaafu wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Thobias Andengenye amewataja waliofariki katika ajali hiyo iliyotokea Desemba 23, 2023 kuwa ni dereva na mmiliki wa gari ndogo Hamis Chaurembo (27).
Wengine ni waliokuwa abiria Bernadina Reuben (22), Maduha Asukile Ntinganiza Bihezako (67) Vedastus Paul (28), Vladmir Vedastus (1) na marehemu wengine wawili majina yao bado hayajatambuliwa.
Mheshimiwa Andengenye amewataja majeruhi katika ajali hiyo kuwa ni Flavianus Felician(28), Juma Said (27), Daniel Samwel (33), Silvanus Muhingwa (43), Sara Bundala (20) na Doris Mafumbo (22).
Aidha, watatu kati yao wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa Bugando jijini Mwanza huku wengine watatu wakiendelea na matibabu katika Hospitali ya Wilaya Kibondo.
RC ametoa rai kwa kwa watumiaji wa vyombo vya usafiri mkoani Kigoma kuendelea kuchukua tahadhari ikiwemo kuzingatia alama za usalama barabarani pamoja na kuepuka mwendo kasi.
Vile vile ametumia fursa hiyo kuikumbusha jamii mkoani humo kuchukua tahadhari mbalimbali za kiusalama hususani katika kipindi hiki cha msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.