MWANZA-Mfanyabiashara wa Kata ya Ilangala katika Kisiwa cha Gana kilichopo Wilaya ya Ukerewe Mkoa wa Mwanza, Nyamitere Ugunya, amejitolea nyumba yake aliyokuwa anaitumia na kuikabidhi kwa Jeshi la Polisi ili iwe Kituo cha Polisi kwa ajili ya kutoa huduma za usalama kwa wakazi zaidi ya 6,000 wa kisiwa hicho.
Nyumba hiyo yenye vyumba zaidi ya 15 ambayo inatakiwa kufanyiwa ukarabati mdogo wa kuwekewa miundombinu na mifumo ya majitaka inatajwa itakidhi hadhi ya Kituo cha Polisi.
Akizungumza na wananchi wa kisiwa hicho kwa niaba ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, SACP Wilbrod Mutafungwa amempongeza mfanyabiashara huyo kwa moyo wake wa kizalendo.
Kamanda huyo amesema, baada ya kukamilika kwa ukarabati wa nyumba hiyo ili kukidhi vigezo na viwango vya kuwa Kituo cha Polisi katika eneo hilo kutarahisisha kutatua changamoto za kiusalama ambazo zimekuwa zikiwakabili wananchi na wakazi wa kisiwa hicho.
Aidha, wananchi waishio kisiwani hapo waliliomba Jeshi la Polisi kusaidia kukamilisha mapema ukarabati wa jengo hilo ili changamoto hizo za kiuhalifu zitatuliwe huku wakiomba mipaka inayotenganisha Tanzania na Uganda iwekwe ziwani ili kupunguza matukio ya wavuvi wa pande hizo mbili kuingiliana.
Hata hivyo, Kamanda Mutafungwa alitangaza kuanza kufanya operesheni kabambe na endelevu ndani ya Ziwa Victoria na maeneo mengine ili kutokomeza uhalifu na kuimarisha usalama zaidi katika maeneo yote.