Akili Platform Tanzania wafikisha elimu kuhusu afya ya akili Kagera

NA DIRAMAKINI

UONGOZI wa Shirika la Akili Platform Tanzania umeendelea kufikisha elimu juu ya dhana ya Afya ya Akili kwa makundi mbalimbali nchini ambapo awamu hii ilikuwa ni zamu ya Mkoa wa Kagera.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi wa shirika hilo, Roghat Robert wakati akitoa mrejesho kuhusiana na safari yao Wilaya ya Muleba mkoani Kagera kwenye tukio adhimu la Kagera Woman Galla 2023.

Shughuli kuu ilikuwa ni Kagera Woman Galla 2023 ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mheshimwa Fatuma Mwasa ambaye ni mwanamke wa kwanza kuwa mkuu wa mkoa huu akiwa amejiimarisha katika misingi ya uongozi wenye ushirikiano na ushirikishwaji wa jamii.

Robert amesema, shughuli hiyo adhimu ilifanyika Desemba 2, 2023 katika eneo la Nalphine Hotel huku ikiwakutanisha washiriki zaidi ya 150 ambapo wote walipata elimu kuhusu afya ya akili.

"Pia, tumefanikiwa kutambulisha shirika kwa Wanakagera na kupitia hapo familia 20 zenye watoto wenye ulemavu wa akili ziliweza kutambulika ambapo katika hili tumeacha mabalozi tutakaofanya nao kazi katika eneo hili la Afya ya Akili.

Aidha, katika shughuli hii adhimu Shirika la Akili Platform Tanzania lilifanikiwa kupata mwaliko kutoka kwa Mwenyekiti wa Kagera Woman Galla, B.Gissela Tibaijuka ambaye ni mama mwenye kupenda akina mama wapate kujikomboa katika nyanja mbalimbali akiwa na timu yake nzima.

"Katika Wilaya ya Muleba, Balozi wa Akili Platform Tanzania aliyekabidhiwa mwongozo na kitabu cha rejea ni Bi Gissela Tibaijuka ambapo atasimamia Wilaya ya Muleba akiwa na jukumu la kufikia kata 49,"amesema.

Vile vile, kwa upande wa Wilaya ya Bukoba, Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema aliyepewa jukumu la uwakilishi ni Bi.Eliana Eliasi na wengine kama watakavyotangazwa kwenye taarifa kuu.

"Tulifanikiwa kuuza vitabu vya Dhana ya Afya ya Akili ambavyo viko kwenye lugha ya Kiswahili kabisa kwa toleo la kwanza na tulifanikiwa kukutana na wafanyakazi wa Serikali na wafanya biashara na kupata mazungumzo kazi.

"Yote kwa yote tulifanikiwa kupata watu wapya ambao ni daraja la kufikia mafanikio ya ukombozi wa fikra katika familia na mtu mmoja,"amebainisha Robert.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mtendaji huyo amesema,changamoto kuu ni ukosefu wa elimu ya afya ya akili kwani watu bado wanajua afya ya akili ni ugonjwa.

"Hii ilitupa fursa ya kutambua kuwa bado kama shirika tuna jukumu la kutumia njia mbalimbali kutoa elimu ya dhana ya afya ya akili ndani ya Mkoa wa Kagera.

"Changamoto ya pili ni muda kutokana na ratiba somo likiwa limeanza kukolea muda haukuwa rafiki. Kwa ufupi waandaaji walifanya kazi kubwa sana, kwani wameonesha thamani ya undungu kwa kuwakutanisha pamoja akina mama kupata elimu, chakula na michezo ni dhahiri kuwa hii ni tunu ya upendo, amani na mshikamano katika kufikia maendeleo endelevu ya familia zetu.

"Katika hili kama Akili Platform Tanzania tunaendelea kushirikiana katika kuandaa makongamano zaidi ili kufungua uelewa zaidi."

Pia.Uongozi wa Shirika la Akili Platform Tanzania umeipongeza na kutambua mchango wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupita kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera.

Sambamba na safu yake nzima kwa kuridhia kuwa sehemu ya kusanyiko la Kagera Woman Galla 2023. "Ni wazi alikuwa na shughuli nyingi ila aliziacha na kujumuika, ni ishara ya ustahimilivu na upendo wa dhati."

Mada zilizokuwepo zote zilikuwa muhimu sana na adhimu kwa kila Mtanzania.

01. Dhana ya Afya ya Akili katika jamii

02. Dhana ya ulaji bora na lishe katika familia

03. Dhana ya ukatili katika jamii

04. Dhana ya uchumi katika jamii

05. Dhana ya mahusiano ya kimapenzi na ndoa

Kila mada ilipigwa ipasavyo na wafundishaji.

Mkurugenzi Mtendaji wa Akili Platform Tanzania, Roghat Robert aliwaomba akina mama kuendeleza jukumu ya kutumia familia kuwa kiungo cha maendeleo kwa kuzingatia wajibu wao katika familia ambao ni kuratibu shughuli zote za familia kwa kushirikiana na wenza wao

Robert pia aliwaomba watambue kuwa katika maisha kuna wakati unapata furaha, kuna wakati unapata huzuni na kuna wakati unapata hofu, wasiwasi na majuto hivyo ni muhimu sana kujua.

Aidha,amesema ofisi kuu ya Akili Platform Tanzania ndani ya Mkoa wa Tabora ipo Wilaya Tabora Mjini katika Kata ya Cheyo ndani ya Mtaa wa Ikulu nyumba Na.28.

"Jambo dogo kwako, kwa mweza wako ni kubwa na jambo kubwa kwako kwa mwenza wako ni dogo. Hivyo, kutumia tiba ya saikolojia ni muhimu sana nyakati ngumu.

"Niseme wazi kuwa, utafutaji usifanye uvunje ndoa yako, uteseke na msongo wa mawazo, kiwewe na upweke pamoja na unyong'ofu, mwisho ukavunja ndoa yako pambana ila kumbuka bado wewe ni mwanamke tu,"amefafanua Robert.

Alihitimisha kwa kuwakumbusha kuwa, ni muhimu sasa watoto kufundishwa kazi za mikono katika familia na watoto wasifanywe kama mayai kiasi kwamba hata kujitunza wao na kujitegemea wakati wa ujana wao ikawa mzigo.

"Niseme tu, mabalozi wetu hasa wewe wa Muleba na Bukoba kila kata tafuta akina mama watano na akina baba watano wakipatika na vijana watano kila kata hawa wakishaelewa nini tunafanya watakuwa msaada mkubwa katika mkoa wetu wa Kagera,"amefafanua Mkurugenzi Mtendaji huyo wa Akili Platform Tanzania.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news