ZANZIBAR-Mkurugenzi Mwandamizi wa Benki ya Dunia,Axel Van Tvotsenburg amesema,benki hiyo itaendelea kushirikiana na Tanzania katika uendelezaji wa miradi mbalimbali kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu nchini.
Akizungumza na wananchi wa Mafufuni Wilaya ya Kaskazini "B" Unguja alipotembelea miradi ya kimaendeleo katika Shehia hiyo amesema, ameridhishwa na maendeleo ya miradi hiyo,hivyo Benki ya Dunia itaendelea kusaidia miradi ya kimaendeleo ili kuwasaidia wananchi.
Naye Waziri wa Ofisi ya Rais, Fedha na Mipango,Dkt. Saada Mkuya Salum amesema, matunda yaliyopatikana katika utekelezaji Miradi ya Benki ya Dunia nchini yameijengea uaminifu Tanzania jambo ambalo litahamasisha upatikanaji wa fedha zaidi kutoka benki hiyo.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini,Shadrack Nzirai amesema, taasisi yake inaendelea kuwawezesha wananchi kupitia miradi mbalimbali ya uimarishaji wa uchumi wao ili kuondokana na umaskini.
Nao wananchi wa Mafufuni wameishukuru Benki ya Dunia kwa kuwasaidia katika miradi ya kuwainua kiuchumi na kuahidi kuendeleza kuitunza miradi hiyo.