NA GODFREY NNKO
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imekamata zaidi ya kilo 3,182 za dawa za kulevya aina ya Heroin na Metamphetamine.
Hayo yamesemwa leo Desemba 27,2023 na Kamishna Jenerali wa Mamlaka hiyo,Aretas Lyimo wakati akizungumza na Wanahabari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.
Amesema, ukatamataji huo mkubwa wa dawa ambazo hazijawahi kukamatwa hapa nchini umetokana na operesheni kubwa iliyofanyika jijini Dar es Salaam na mkoani Iringa.
Operesheni hiyo imefanyika Desemba 5 hadi 23,2023 huku watu saba wakikamatwa ambapo kati yao wawili ni raia kutoka Asia.
Kamishna Jenerali amesema kuwa, dawa hizo zingefanikiwa kuingia mitaani zingeleta madhara kwa watu zaidi ya milioni 70 kutoka ndani na nje ya nchi.
“Ukamataji huu umehusisha kiasi kikubwa cha dawa za kulevya ambacho hakijawahi kukamatwa katika historia ya Tanzania tangu kuanza kwa shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya.
"Hivyo, watuhumiwa waliokamatwa ni miongoni mwa mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya inayofuatiliwa nchini na duniani.
"Kiasi cha dawa zilizokamatwa, endapo zingefanikiwa kuingia mtaani zingewza kuathiri zaidi ya watu 76,368,000 kwa siku.
“Ukamataji huu umeokoa nguvu kazi ambayo ingeangamia kutokana na madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi,"amefafanua Kamishna Jenerali Lyimo.
Vile vile amesema, kiasi hicho cha dawa za kulevya kinajumuisha kilogramu 2,180.29 za dawa aina ya methamphetamine na kilogramu 1001.71 aina ya heroin zilizokamatwa katika Wilaya ya Kigamboni, Ubungo na Kinondoni jijini Dar es Salaam pamoja na Wilaya ya Iringa mkoani Iringa.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema kuwa, aina ya dawa ambazo wamezikamata zilikuwa zimefungashwa kwenye vifungashio vya bidhaa zenye chapa mbalimbali za majani ya chai na kahawa.
Tags
Breaking News
DCEA
DCEA Tanzania
Habari
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA)