DCEA yamshukuru Rais Dkt.Samia kwa kuwapa nguvu ya kung'ata 'mapapa wa unga'

NA GODFREY NNKO

KAMISHNA Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuifanya mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Shukurani hizo amezitoa Desemba 27,2023 katika ofisi ya mamlaka hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanahabari kuelezea kuhusu kukamatwa kwa shehena kubwa ya dawa za kulevya aina ya Heroin na Methamphemine .

“Kipekee ninaishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wetu mpendwa, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha mamlaka katika kuendelea kutekeleza kazi zake kwa ufanisi mkubwa sana,”amefafanua Kamishna Jenerali Lyimo.

Amesema, kupitia operesheni walizozifanya kati ya Desemba 5 hadi 23, 2023 jumla ya kilo 3,182 za dawa hizo zikiwa kwenye vifungashio vya kahawa na majani ya chai zilikamatwa katika Jiji la Dar es Salaam na Mkoa wa Iringa.

“Ukamataji huu umeokoa nguvu kazi yaani Tanzania tupo idadi ya watu milioni 60 hizi dawa zingefanikiwa kuingia sokoni basi zingeathiri si tu wanzania bali hata mataifa mengine maana nyingine zilikuwa zikisafirishwa nchi nyingine,”amesema Lyimo.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema, kiasi hicho cha dawa kinajumuisha kilo 2, 180.29 za dawa aina ya Methamphemine na kilo 1001.71 aina ya Heroin zilizokamatwa katika wilaya za Kigamboni, Ubungo na Kinondoni jijini Dar es Salaam na mkoani Iringa.
Pia, amebainisha kuwa, katika operesheni hiyo watu saba wamekamatwa kati yao wawili ni raia kutoka barani Asia.

Vile vile amefafanua kuwa,mbinu ambayo imekuwa ikitumika kufunga dawa hizo kwenye vifungashio vya bidhaa zenye chapa mbali mbali ikiwemo kahawa na majani ya chai inatumika kwa lengo la kurahisha usafirishaji wake na kukwepa kubainika.

Amesema, dawa ya Methamphemine ni dawa mpya ya kulevya iliyopo katika kundi la vichangamshi sawa na cocaine. “ Ukiacha dawa za Heroin, inayotengenezwa kwa mchanganyiko wa kemikali kutoka kwenye mmea wa afium taani opium popi inayolimwa inayolimwa katika nchi za Asia na baadhi kutoka Amerika, dawa aina ya Methamphemine ni dawa mpya ya kulevya iliyopo katika kundi la vichangamshi sawa na Cocaine.

“Dawa hii huwa kwenye mfumo wa vidonge, unga au chembechembe mithili ya chumvi ang’avu yenye rangi mbalimbali ambayo huzalishwa kwenye maabara bubu kwa kuchanganya aina mbalimbali za kemikali bashirifu.

“Dawa hii ni hatari sana,kwa afya ya mtumiaji, madhara yake ni makubwa na hayatibiki kirahisi kwani mtumiaji hupata madhara ya kudumu kwenye ubongo na hivyo kupunguza uwezo wa kutunza kumbukumbu, kusababisha urahibu na kuathiri mfumo mzima wa fahamu.

“Hii dawa aina ya Metamphetamine inachanganywa kwa kemikali mbalimbali, kemikali hizi bashirifu wanachanganya na inapatikana hii dawa aina ya Metamphetamine na hii dawa ni kali sana.

"Inaathiri moja kwa moja ubongo wa mtumiaji, inaathiri uwezo wake wa kutunza kumbukumbu, lakini pia matibabu yake ni magumu na mpaka sasa hivi hakuna dawa ya kuweza kutibu.

"Tofauti na ilivyo heroin kuna dawa ambayo unaweza ukaitibu na mtu akarudi katika hali yake ya kawaida, lakini hii Metamphetamine, dawa mpya ambayo athari yake ni kubwa sana kwa mtumiaji wa hiyo aina ya dawa ya kulevya."

Kamishna Jenerali Lyimo amesema, mamlaka inatoa onyo kwa wote wanaoendelea kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya hapa nchini kuacha badala yake wajikite kwenye biashara nyingine halali kwani DCEA imejidhatiti kukomesha biashara ya dawa ya kulevya nchini.

Kamishna Jenerali amesema kuwa, dawa hizo zingefanikiwa kuingia mitaani zingeleta madhara kwa watu zaidi ya milioni 70 kutoka ndani na nje ya nchi.

“Ukamataji huu umehusisha kiasi kikubwa cha dawa za kulevya ambacho hakijawahi kukamatwa katika historia ya Tanzania tangu kuanza kwa shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya.

"Hivyo, watuhumiwa waliokamatwa ni miongoni mwa mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya inayofuatiliwa nchini na duniani.

"Kiasi cha dawa zilizokamatwa, endapo zingefanikiwa kuingia mtaani zingewza kuathiri zaidi ya watu 76,368,000 kwa siku.

“Ukamataji huu umeokoa nguvu kazi ambayo ingeangamia kutokana na madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi,"amefafanua Kamishna Jenerali Lyimo.

Kamisha Jenerali huyo amesema, watuhumiwa hao waliokamatwa ni miongoni mwa mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya inayofuatiliwa nchini na duniani kote.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news