Dkt.Biteko apongeza utoaji huduma bora Hospitali ya Charles Kulwa

GEITA-Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dkt. Doto Biteko amepongeza Uongozi wa Hospitali ya kumbukumbu ya Charles Kulwa iliyoko Wilayani Bukombe mkoani Geita kwa kuendelea kutoa huduma bora kwa kufuata maadili ya taaluma bila kuibua malalamiko kutoka kwa wananchi wanaotibiwa katika hospitali hiyo.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (kulia),Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella (kushoto) mwenye suti nyeusi na Mkurugenzi wa Hospitali ya Charles Kulwa, Dkt.Baraka Charles katika uzinduzi wa wodi za wagonjwa katika hospitali hiyo.

Biteko amesema hayo Desemba 30,2023 wakati akizungumza wafanyakazi wa hospitali hiyo na watu mbalimbali katika uzinduzi wa wodi mbili za wagonjwa Hospitali hiyo.

Amesema kuwa, katika kipindi chake chote ambacho amekuwa Mbunge wa Jimbo la Bukombe hajawahi kupata malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi kuhusu hospitali hiyo badala yake wananchi wana imani kubwa na huduma wanazopata.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Biteko amesema kuwa serikali inaendelea kuweka mazingira mazuri ya afya nchini na serikali itaendelea kushirikishana wadau ili kuhakikisha huduma za afya nchini zinaimarika zaidi.
Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martine Shigella ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema kuwa Hospitali hiyo imeendelea kuwa ya mfano katika mkoa huo kwa kutoa huduma bora ya matibabu.

Amewataka wafanyakazi wa hospitali hiyo kuendelea kufanya kazi kwa uadilifu mkubwa kwa kufuata maadili ya taaluma zao na miongozi mingine.

Amesema,hospitali hiyo imeajiri wafanyakazi wapatao 83 hivyo imesaidia kupunguza upungufu wa ajira kwa serikali na wananchi hao isingekuwa hospitali hiyo kuwepo wangekuwa hawana ajira.
Mkurugenzi wa hospitali hiyo, Dkt. Baraka Charles amesema kuwa Hospitali hiyo ilianzishwa mwaka 1992 ikiwa na hadhi ya zahanati chini ya baba yake mzazi Charles Kulwa na hadi sasa Hospitali hiyo imefikia hadhi ya Hospitali ya Wilaya.

Amesema kuwa wanaendelea kuhakikisha wanatoa huduma bora na za uhakika muda wote ili kulinda afya za wananchi wanaofika kupata huduma za tiba.

Ameongeza kuwa pamoja na kuendelea kufanya vizuri pia wanatoa huduma za kibingwa na mwelekeo wao ni kuhakikisha Hospitali hiyo inakuwa na hadhi kubwa zaidi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news