RABAT-Serikali ya Morocco imezindua mpango uliosubiriwa kwa muda mrefu wa kuzisaidia kaya masikini ambao unajumuisha malipo ya kila mwezi kwa karibu familia milioni moja zenye kipato kidogo nchini humo.
Picha na borgenproject.
Waziri Mkuu Aziz Akhannouch amenukuliwa katika taarifa rasmi akifafanua kwamba kila mnufaika atapokea angalau dirham 500 (€ 46) kwa mwezi, bila kujali ukubwa wa familia na utekelezaji utaanza ndani ya wiki hii.
"Utekelezaji wa mpango huu unahitaji bajeti ya dirham bilioni 25 (karibu €2.29 bilioni) kwa 2024," alisema msemaji wa Serikali Mustapha Baitas mwishoni mwa Oktoba.
Ruzuku hizi za familia zinazolengwa, na zilizojadiliwa kwa muongo mmoja bila kuzaa matunda, ni sehemu ya mageuzi mapana ya kijamii yaliyochochewa na Mfalme Mohammed VI mnamo 2020.
Mpango huu pia unajumuisha upanuzi wa huduma ya hifadhi ya jamii kwa watu wote wa Morocco, ambao ulianza mwaka wa 2021.
Bima ya lazima ya afya, ambayo hapo awali ilikuwa inapatikana kwa watumishi wa umma na wafanyakazi wa sekta ya binafsi, tayari inawanufaisha zaidi ya wafanyakazi milioni 3.8 na familia zao, kulingana na shirika la habari la MAP.
Huduma hii ya matibabu pia imeongezwa bila malipo kwa zaidi ya watu milioni 10 wasiojiweza, huku serikali ikisimamia michango yao.
Marekebisho haya ya kijamii yanaimarishwa huku kukiwa na kuzorota kwa uchumi na tofauti kubwa za kijamii zinazoathiri wakazi milioni 36 wa nchi hiyo.
Taifa hilo lilitabiriwa kusajili kiwango cha ukuaji uchumi cha 2.7% na mfumuko wa bei wa 6.1% mnamo 2023, kulingana na makadirio ya hivi karibuni kutoka Benki Kuu ya Morocco.
Hadi sasa, misaada ya kijamii imekuwa isiyo ya moja kwa moja huku Serikali ikitoa ruzuku kwa bidhaa fulani za watumiaji kupitia hazina ya fidia.
Hazina hii inatakiwa kufanyiwa mageuzi tarehe ambayo haijawekwa ili kutoa nafasi kwa ajili ya misaada inayolengwa kwa wasiojiweza.