KINSHASA-Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (CENI) imetoa matokeo zaidi ya awali ya uchaguzi wa Rais, yakionesha Rais Felix Tshisekedi anaongoza kwa mbali, akifuatiwa na mfanyabiashara maarufu Moise Katumbi.
Matokeo yaliyotangazwa na CENI kufikia sasa yanatokana na takribani kura milioni 1.9, kati ya jumla ya wapiga kura milioni 44 waliojiandikisha katika nchi hiyo kubwa ya Afrika ya Kati yenye ukubwa sawa na eneo la Ulaya Magharibi na yenye wakazi zaidi ya milioni 100.
CENI imesema, Tshisekedi mwenye umri wa miaka 60, aliye madarakani tangu 2019 na anayewania muhula wa pili wa miaka mitano, alikuwa anaongoza kwa zaidi ya asilimia 81 ya kura.
Alikuwa akifuatiwa kwa mbali na mfanyabiashara tajiri na Gavana wa zamani wa Jimbo la Katanga, Moise Katumbi mwenye umri wa miaka 58 akiwa na zaidi ya asilimia 15 ya kura na mtendaji mkuu wa zamani wa mafuta Martin Fayulu mwenye umri wa miaka 67 kwa zaidi ya asilimia moja.
Wapinzani wengine karibu 20, akiwemo Denis Mukwege, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel mwenye umri wa miaka 68 walishindwa kupata asilimia moja.
Aidha, CENI haijatangaza idadi ya watu waliojitokeza kupiga kura katika uchaguzi wa Desemba 20 na 21 lakini bado imekuwa ikitoa matokeo hatua kwa hatua tangu Ijumaa, ambayo ni pamoja na uchaguzi wa Wabunge, mikoa na mitaa. (DW)