DAR ES SALAAM-Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT),Emmanuel Tutuba amezindua Mtaala wa Elimu ya Fedha kwa Wakufunzi huku akisisitiza utekelezaji wake uwe endelevu na wenye ubunifu ili ulete tija kwa watanzania wengi kufahamu elimu ya fedha.
Uzinduzi huo uliowashirikisha wadau mbalimbali wa masuala ya fedha yakiwemo mabenki umefanyika leo Desemba 18,2023 katika Ukumbi wa Kilimanjaro uliopo katika Ofisi ya Makao Makuu Ndogo ya Benki Kuu jijini Dar es Salaam
Akizindua mtaala huo, Gavana Tutuba amesema kuwa, katika utekelezaji wa mtaala huo ni vyema vyuo vikuu vilivyoingia mkataba na BoT kwa ajili ya utoaji wa elimu ya fedha kuweka utaratibu wa kufanya tathmini.
Sambamba na kupata takwimu ni watu wangapi wamenufaika kwa kuwepo kwa mtaala huo huku akisisitiza kwamba gharama ziwe rafiki Ili watanzania wengi wafikiwe.
"Naomba nisisitize kwa vyuo vyote ambavyo tumeingia makubaliano ya kufundisha elimu ya fedha kuhakikisha kwamba taarifa za utekelezaji zinatolewa ili kuona tumefanikiwa kwa kiwango gani,"amesema Gavana Tutuba.
Aidha,Tutuba ameongeza kuwa, Sekta ya Fedha hapa nchini ipo imara na imekidhi vigezo vyote vya Kimataifa na kuongeza kuwa, suala la utoaji wa mikopo pamoja na mashariti ungekuwa una uwazi kabla ya utoaji wa mikopo kwa wakopaji tungeondokana na baadhi ya changamoto zilizopo kwenye sekta hiyo.
Amesema, hatua hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Baraza la Taifa la Huduma Jumuishi za Kifedha (National Council for Financial Inclusion) baada ya kuona ujuzi wa kifedha ni muhimu kwa ustawi wa ushirikishwaji, ukichochea ukuaji endelevu kwa kuwawezesha watu kusimamia fedha zao binafsi.
Vile vile, baraza kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia limefanikiwa kuingiza elimu ya fedha katika mfumo rasmi wa elimu, kuanzia ngazi ya shule ya msingi mpaka chuo kikuu kwa lengo la kutoa elimu ya fedha mapema na kukabiliana na changamoto hyo kwa wale walioko shuleni.
Kwa upande wake Naibu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Cha Iringa, Prof.Andrew Mbwambo ambacho ni miongoni mwa Chuo Kikuu kilichoingia mkataba na BoT kwa ajili ya kutekeleza mtaala huo amesema,mtaala huo ukitekelezwa vizuri litakuwa ni jambo bora kwa nchi na ni baraka kwa watanzania kwani watakuwa na uelewa na elimu ya fedha.
Ameongeza kuwa, kwa upande wa chuo chake watakuwa wakitoa mafunzo hayo kwa muda wa wiki mbili na kwa kuanzia watajikita katika mikoa ya Iringa, Mbeya ,Ruvuma,Rukwa pamoja na wilaya za mikoa hiyo.
Naye, Katibu Mtendaji wa Baraza la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi (NEEC),Beng'i Issa amesema kutokuwa na elimu ya fedha kwa wananchi walio wengi hususani wanawake ni changamoto kubwa inayosababisha wanawake kuchukua mikopo ikiwemo ya kausha damu na mwisho wa siku wanashindwa kurejesha kutokana na riba kubwa wanayotozwa.
"Wanawake wengi wamekuwa wakikopa hususani hii mikopo ya kausha damu bila kufahamu masuala ya riba.
"Sasa wakati wa kufanya marejesho ndipo wanapogundua hilo, iwapo wangekuwa na elimu ya fedha changamoto hizo zisingekuwepo,"amesema.
Amesema,sekta ya fedha inapendwa na inatumiwa na watu wote,lakini mbaya zaidi watu hao wawe wasomi na wasio wasomi, wenye fedha na wasio na fedha elimu ya fedha bado ni tatizo kwao.
Amesema kuwa, kutekelezwa kwa mtaala huo kutasaidia sana watu kujua namna ya kuzitawala fedha na sio fedha kuwatawala.
Kwa upande wake Naibu Gavana Udhibiti na Usimamizi wa Sekta ya Fedha, Sauda Msemo, amesema mtaala huo una lengo la kukuza maadili katika masuala ya fedha.
Pia,amesema wanategeme kwamba baada ya uzinduzi, ifikapo 2024 litapatikana kundi la kwanza la wakufunzi ambao nao watakuwa chachu ya kuwafikia watanzania wengi kwa pande zote za Muungano.