NA MWANDISHI WETU
WENGINE walisema Hassan bin Omari katika maisha yake alikuwa na jinsia mbili za kike na kiume, lakini uchunguzi wa kidaktari baada ya kifo chake haukuthibitisha hilo.
Hassan bin Omari au Makunganya; alifariki Novemba 26 mwaka 1895, alikuwa wa kabila la kiyao mwenye dini ya kiislamu huko Makanjila, aliishi mlimani, na alifanya biashara ya pembe za ndovu na ya watumwa, na pia alikuwa hodari katika kushambulia misafara iliyopita katika eneo lake la Mavuji, karibu na Kilwa Kivinje.
Baada ya kupigana na Wajerumani alikamatwa, na mwishowe alinyongwa na Wajerumani hao akiwa pamoja na wenzake.
Asili ya Hassan bin Omari ni kutoka kwa watu wa kabila la Makanjila, wayao, ambao kufikia karne ya 19 walikuwa wasimamizi wa njia kuu ya misafara ya biashara, kutoka maeneo ya Nyasa na majirani ya mto Zambezi, mpaka pwani ya kusini mwa Tanzania ya leo, hasa mji wa Kilwa Kivinje, kilomita 25 kaskazini mwa Kilwa Kisiwani, ambapo watu wengi kabila la Wayao walikuwa wamekwishaanza kuishi.
Kilwa Kivinje ilikuwa Bandari kuu ya usafirishaji wa watumwa na bidhaa mbali mbali katika eneo hilo wakati wa utawala wa Omani na wajerumani.
Hassan bin Omari alishirikiana na watu wa kabila la Wayao na wengine katika mapigano ya mwaka 1888. Pia, idadi kubwa ya Wayao katika karne hiyo tayari walifuata dini ya Uislamu. Biashara yenyewe kati ya Uyao na Kilwa pamoja na nchi za kusini mbele ya kisiwa cha Msumbiji, ilianza kabla ya karne ya 17.
Misafara ya biashara hii ilifika Kilwa kila mwaka na kuleta pembe za ndovu, watumwa na bidhaa zingine.Wayao walikuwa watu wa kwanza kukaa katika mji wa Kilwa Kivinje.
Makanjila III, mfalme wa Mangochi huko Nyasa mnamo mwaka 1870, aliikaribisha dini ya kiislamu kuwa dini yake binafsi, na ya baraza lake. Viongozi wengineo wa kiyao, walihusika sana kwenye kukamata watu wa makabila yaliyo jirani na kuwatia utumwani.
James Frederic Elton, Septemba, mwaka 1877 alisimulia kwamba Makanjila ni "... Chifu Mkuu wa biashara ya watumwa katika pwani ya Mashariki ya Nyasa". Aliendelea kusema, aliona "nchi iliyolimwa vizuri ... na nyumba zilizojengwa kwa uangalifu sana... Mkuu mwenyewe anaye veranda na 'baraza' la ukubwa kupita nyumba nyingi za Zanzibar".
Makanjila alionyesha heshima kubwa sana kwa Sultani wa Zanzibar, Makanjila alimwambia, Harry Johnston mnamo mwaka1890, kuwa "Wazungu wakija kuivamia nchi ya Sultani wa Zanzibar, mimi, Makanjila, nitamwokoa!"
Katika karne ya 19, vikosi vya Ujerumani na Uingereza vilipigana na wenyeji wengi kwaajili ya kuifuta biashara ya utumwa na kuhakikisha inamalizika, biashara ambayo ilikuwa na faida kubwa kwa watu wa kabila la Wayao.
Wakati uleule Wajerumani waliwasili katika pwani ya Afrika Mashariki mwaka 1888 na kuweka bendera zao pamoja na manowari za Ujerumani na zingine za Ulaya, ambazo zilikuwa zinalinda miji ya pwani, Wayao waliteswa na kampuni na vikosi vya Uingereza dhidi ya eneo lao katika mji wa Nyasa.
Harry Johnston, pamoja na kikosi chake cha wanajeshi wa Sikhi na wa Zanzibar, kwa maneno yake alitoa taarifa kwamba "Ongezeko kubwa la nguvu nilizonazo ziliniwezesha katika msimu wa vuli wa mwaka1893, kutekeleza ushindi dhidi ya Makanjila. Tulimfukuza kwanza kutoka Pwani ya Magharibi ya ziwa...na kisha kumshambulia katika nchi yake na kuteka kila moja ya miji yake kwa mfululizo".
Makanjila, wakati huu alikuwa yupo huko kwa, Mwinchande Salimu, ambaye baada ya kushindwa mikononi mwa Johnston, alikimbilia "Mwembe, kwa rafiki yake Che Mataka ambaye; baadaye alijiunga na Che Makunganya huko Mrimani, ambapo alikaa hadi mwaka 1914, aliporudi." alifika Pwani mwaka 1894 akawa pamoja na Makunganya, yaani Hassan bin Omari, wakati huo.
Kampuni ya Kijerumani ya Afrika ya Mashariki, (Deutsch-Ostafrikanische Gesellschaft (DOAG)) ilipata haki mwezi Aprili mwaka 1888 ya kumiliki Bandari na biashara ya Pwani ya Zanzibar, na usimamizi wa eneo hilo badala ya Sultani wa Zanzibar, kampuni hii ilifanya harakati na kuanza kumiliki Bandari zote muhimu ikiwemo Kilwa Kivinje, mwezi Agosti mwaka 1888.
Watu wa kampuni hii walishuka katika miji muhimu yote ya pwani kusimika bendera ya kampuni pamoja na ile ya Sultan wa Zanzibar. Lakini, baada ya siku chache watu walikerwa na wageni hao na kusababisha kutokea kwa machafuko makubwa katika miji ya Pwani ikiwemo Pangani, Saadani na Bagamoyo, vurugu hizo zilijumuisha idadi kubwa ya watu wa asili, hasa Wayao katika eneo la Kilwa.
Septemba mwaka uleule katika mji wa Kilwa Kivinje, baada ya liwali wa Sultani kuondoshwa, watu walichukua silaha mikononi na kuwaambia maafisa wa Kampuni ya Kijerumani Afrika ya Mashariki kuishusha bendera yao na kuiacha ya Kilwa.
Walipokataa, maafisa wa kampuni, Heinrich Hessell na Gustav Krieger, walizingirwa katika ofisi zao na wenyeji kwa siku kadhaa.
Mjerumani mmoja, Krieger, aliuawa kwa kupigwa risasi alipojaribu kutoka nje ya ngome ili kuwapa habari watu wa kwenye meli ya kijeshi ya Ujerumani iliyosimama baharini; yule mwingine, Hessell, aljifungia ndani ya chumba cha juu, na alijiua mwenyewe kwa risasi, maofisa wengi waliokufa walikuwa ni wa kijerumani, na maasi yalikuwa makubwa.
Baadaye, paliwekwa kumbukumbu huko Kilwa Kivinje, kukumbuka ya vifo vya maafisa hawa wawili wa kijerumani. Habari ilitumwa na Gustav Michahelles, Balozi wa Ujerumani huko Zanzibar, kwenda kwa Otto von Bismarck, kwamba "Waarabu, wafanyabiashara wa watumwa karibu na Ziwa Nyasa, walichochea Wayao kuwashambulia Wajerumani", na haikuwa ghasia iliyosababishwa kwa nia mbaya ya kuupinga utawala wa Ujerumani bali ilikuwa na chimbuko lake kusini mwa Ruvuma, ndani ya majimbo ya Ureno na majirani wa Ziwa Nyasa.
Muda mfupi baadaye, Februari 2 mwaka 1889, Bunge la Ujerumani lilikubali kuiokoa kampuni ya DOAG iliyokuwa katika hali mbaya, na Hermann von Wissmann alichaguliwa kuwa kamishna wa kifalme, kuongoza kikosi cha kwenda Afrika Mashariki kukabiliana na ghasia za Pwani.
Hermann von Wissmann aliwasili na wanajeshi wake mamluki Machi mwaka 1889. Huku akisaidiwa na meli za kijerumani zilizolinda miji iliyo kando ya bahari, alifaulu kutuliza vurugu maeneo ya Pwani ya Kaskazini
Kisha akaelekea Kilwa na nchi ya kusini, akatua na wanaume 1200 kusini mwa Kilwa, akafika mji wa Kilwa Kivinje kwa miguu. Aliuchukua mji kwa kutumia nguvu za meli zilizo baharini pamoja na za watu walio nchi kavu. Mabomu yaliipiga Kilwa Kivinje kuanza Mei 3, na kuendelea usiku kucha na siku iliyofuatia.
Karibu robo ya mji uliangamizwa. Kufikia Juni mwaka1890, waasi wote walikuwa wamekimbilia milimani huko eneo la Mavuji, ambalo Hassan bin Omari alikuwepo na ngome yake. Wissmann alimuacha Von Zelewski pamoja na kampuni mbili za Waafrika, Wazungu 15, na bunduki 5 katika eneo la mjini, kusimamia kituo cha kudumu huko Kilwa.
Baadaye pakawa na amani bila usumbufu wa aina yoyote, Baadae Von Zelewski aliwakamata watu waliotuhumiwa kwa vifo vya maafisa wa Kampuni ya Kijerumani ya Afrika Mashariki, Hessell na Krieger, na kisha kuwaua.
Juni mwaka 1894, Luteni Fromm, alipokea maagizo kutoka kwa Gavana kwenda na kuingia katika milima ya Mavuji, na kuvamia ngome ya Hassan bin Omari, lakini hakuweza kumtia mikononi mwake kwani Omari aliweza kutokomea baada ya kupata taarifa yake mapema.
Katika Shajara (Diary) ya, Josef Weinberger, askari Mjerumani iliandika habari ya jaribio hilo. Na kueleza, Jioni ya tarehe 5 Juni, kutofaulu kukamatwa Kwa Hassan bin Omari kulitokana na usaliti wa akida wa Kilwa, Abdalla bin Omari, kama ilivyotaarifiwa na mfungwa mpelelezi, ambaye alikiri hivyo baada ya kupigwa vibaya.
Ilipofika Mwezi Septemba, ilisikika kuwa watu wa Mavuji wameharibu laini ya simu kati ya Mohoro na Kilwa. Siku chache baadaye, alfajiri ya tarehe 7 Septemba mwaka 1894, kufuatia uvumi mwingi, watu wa Hassan bin Omar, pamoja na Wayao walio maelfu, walipiga risasi kituo cha Kilwa, na kisha kupandisha bendera mbili nyekundu za Sultan wa Zanzibar.
Msikiti ulio karibu ulifikwa na wasiwasi kutokana na machafuko haya kwa sababu ya sauti kubwa zilizotokea wakati wa sala ya 'fajr'. Milio mikali ya risasi iliendelea pande zote mbili, na mizinga ilipigwa na kina Omari ndani ya kituo. Karibu saa sita za mchana, majirani walioishi karibu na kituo walikuwa wametulia, na watu wa Hassan bin Omari walikuwa wamerudi nyuma.
Askari wa kijerumani mmoja na askari wanne wenyeji walijeruhiwa, na upande wa Wamavuji waliuawa watu 37, na hawa wakaachwa karibu na kituo hicho. Baada ya mambo haya kwisha, wafungwa kadhaa walinyongwa wakati Luteni Kanali von Trotha alipokuja Kilwa. Zilisikika pia habari wakati huu kwamba mikebe 600 ya baruti, makasha 6 ya mirao, na masanduku 10 ya fedha vilipelekwa katika chombo kutoka Zanzibar kwenda Mtapatapa, kumfikisha mikononi Hassan bin Omari.
Inadaiwa kwamba, Hassan bin Omari, alikuwa na mpango wa kumkamata Wissmann mwenyewe kwa mkono wake, bila Omari kujua kwamba wissmann alikuwa amekwisha ondoka mjini muda mrefu. Shambulio hilo liliwatisha sana Wajerumani, na lilikuwa ndio sababu kubwa ya msako mkali kwa Hassan bin Omari na wenzake.
Miezi iliyofuata, Hassan bin Omari, Mkuu wa Mavuji, alionekana akiingia tena katika uvamizi wa misafara na biashara, pamoja na uporaji wa miji, mauaji, na kuteketeza miji na mashamba kwa moto. Alishtakiwa pia kwa kulazimisha watu wengine kupandisha bendera yake, badala ya bendera ya Ujerumani, na pia kupora silaha na dhahabu.
Mashambulio yake hayo yalifika maeneo mengi, kuanzia Kilwa hadi Kiswere, Bandari na Kijiji kidogo cha zamani kusini mwa Kilwa ambapo mwezi Novemba mwaka 1894, alikuwa ameiba bidhaa kutoka katika ofisi ya forodha yenye thamani ya Rupia 17,000, na kusababisha wafanyabiashara wa kihindi wote kukimbia eneo hilo.
Hekaheka kama hizi ziliendelea mara kwa mara hadi mwaka uliofuatia. Oktoba mwaka 1895, Wissmann alitolea macho machafuko haya ya Kilwa. Akatangaza kwamba haiwezekani kuyavumilia mambo ya Hassan bin Omari, ya kuwalazimisha wenyeji kusimika bendera yake binafsi badala ya ile ya Ujerumani.
Mbali na kufanya jeuri na kulishambulia boma la Ujerumani, aliwanyanyasa majirani wa Kilwa mpaka watu wote wameshindwa kutoka nje ya mji hata zaidi ya nusu saa bila ya kukutana na hatari. Aliendelea kusema Hassan bin Omari aliwakamata wajumbe, na mara nyingi amewaua, na pia amemuunga mkono Machemba, ambaye ni mtekaji mkubwa wa watumwa.
Wissmann sasa aliona kuna umuhimu wa kumuangamiza Hassan bin Omari na kuyamaliza mambo haya mabaya. Kumpa adhabu kali na kuwa mfano kwa watu wengine, pia Adhabu hiyo itaweza kusaidia kuondoa matatizo ya wakuu wengine.
Ghafla akatangaza zawadi ya rupia 1000 Kwa atakayeleta taarifa kwake mahali alipo, na adhabu ya faini kwa wale watakaopandisha bendera ya Omari.
Alisimamisha kampuni nne chini ya kamanda wa Schutztruppe, kikosi cha ulinzi, wamshughulikie, Hassan bin Omari. Aliamuru kampuni mbili kumalizia ujenzi wa boma karibu na kijiji chake ili kuwaweka askari macho na kuanza maandalizi ya eneo hilo.
Kampuni zingine mbili zilitumwa kuondoa mvuto wake kwa watu na kuvirudisha vijiji tena kutii utawala wa kijerumani. Alitaka vita dhidi yake viendelee kabla ya msimu wa mvua kuanza, yaani mwezi mmoja na nusu kutoka siku ya tangazo.
Baada ya kupata idhini iliyotakiwa kufanya kazi hizo, kampuni nne za wanajeshi walitumwa mwezi Novemba mwaka 1895. Wanajeshi wa namba 8 walikaa Kiswere, wa 9 walipenya barani, wa 3 walipanda milimani, juu ya mto Mavuji, na wa 6 walipiga kambi huko Mavuji, kuweka msingi wa boma milimani kule.
Siku ya tarehe 13, huko Kiswere askari wa kijerumani walipokea taarifa kwamba, Hassan bin Omari, alikuwa amekaa na Myao aliyeitwa, Saidi Mitole, huko Mpingiro, wanajeshi walishindwa kumkamata kwani tayari Omari alikuwa amekwisha toroka.
Luteni Fromm alianza kumfuata chapu chapu kwa miguu, na mwishowe akagundua kuwa alikuwa amerudi Mavuji.
Alipofika mto Luawa, alisikia taarifa kwamba Hassan bin Omari alikuwa mahali pale amekaa pamoja na wanawake wake wengi.
Tarehe 15 wanajeshi wa kijerumani waliingia ndani ya eneo hilo wakiwa na nguvu kamili, bila tabu kubwa, Luteni Glauning, aliwakamata watu wawili na mmojawapo alikuwa na kigongo, huyu alijaribu kujitetea na kisu.
Huyo mwenye kisu kumbe alikuwa ni Hassan bin Omari. Muda mfupi baadaye, Waziri wake Omari Muenda, na Jumbe wake pia, walikamatwa. Mtu maarufu miongoni mwao, Sham bin Shaude, akatoroka. Vifaa na vyakula vingi vilipatikana kule, vikachomwa moto, ingawa katika mlipuko Afisa wa chini, Lachemeier, aliungua vibaya. Siku iliyofuata, tarehe 16 walivunja kambi na walirudi kituoni kwao.
Pamoja na kumkamata Hassan, wanajeshi walilikuta sanduku kubwa lenye maandiko, na barua zake. Hans Sache, aliyeandamana na Gavana Wissmann, alichaguliwa kuwa hakimu kuyachunguza mambo haya, kisha Mahakama ikakutana. Omari alikuwa amezitunza sana barua zake za uhaini kwa miaka mingi.
Carl Velten, msomi mashuhuri wa Mashariki, alipewa kazi ya kutafsiri maandishi hayo ambayo kwa sehemu kubwa yalikuwa yameandikwa kwa Kiarabu. Hatimaye, uchunguzi uliwahusu watu zaidi ya mia moja, na haukumalizika kwa takribani wiki saba.
Hukumu za vifo za watu 16 zilikamilika, pamoja na Hassan bin Omari na Jumbe wote walinyongwa. Makran bin Shaude, jumbe wa Kilwa, na Abdalla bin Omari, akida, wote wawili ambao walikuwa wameaminiwa sana katika huduma za kiserikali tangu ghasia za mwaka 1888, walihusishwa katika kesi hizi nao pia walifungwa. Yule wa kwanza alikufa usiku uleule gerezani. Mji wote ulitiwa hatiani, na kupigwa faini.
Wahindi wanne walioheshimiwa sana na wafanyabiashara wakuu, ambao katika vitabu vyao vya kumbukumbu za hali ya fedha vilivyonyang'anywa na Wajerumani walikuwa wametumia neno la 'mshenzi' walimaanisha "Hassan bin Omari," walihukumiwa wauawe, mmojawapo alitajwa katika 'Shairi la Makunganya' kwa jina la Kassam Peera.
Lakini, hukumu hii ilibadilishwa na kuwa ya kifungo na kisha kuwafunga na minyororo, hata mwishowe ilibadilishwa tena, kuwa faini na kufukuzwa nchini, ingawa waliingia merikebuni huku bado wakiwa na minyororo, kuelekea Dar es Salaam, na baadaye Mombasa na kisha Aden.
Hawa wote walikuja kutundikwa chini ya mwembe huko Kilwa Kivinje, na mti huu uliitwa 'Mwembe kinyonga'.
Mti huu ulikufa baadaye, lakini kuna ukumbusho pale wa "Mashujaa walionyongwa na Mjerumani katika Vita vya Maji Maji", bali ilikuwa ni kosa kutaja jina la 'Hassani Omari Makunganya' la kwanza pale, kwa sababu yeye hakuwa hai wakati wa Maji Maji. Mwalimu Julius Nyerere, alifanya ziara ya ukumbusho huo wakati wa Uhuru wa Tanzania, kwa heshima ya mababa wa Kilwa Kivinje waliouawa wakati ule.
Tukio hili la, Hassan bin Omari, lilionekana kwa walowezi wengi wa kijerumani kama ndio somo la kutumia nguvu dhidi ya maasi kwa wenyeji wote, na vitendo hivi vya Kilwa Kivinje vilikuwa kama mifano ya kuwapa funzo wenyeji wote, na ukatili ule ule au zaidi ulitumika kwa wapiganaji wa vita ya Maji Maji uliozuka miaka michache tu baadaye.
Iilichochea moto zaidi pia kwa wale walowezi waliochukizwa na Wahindi, wengine wao ambao walifananisha Wahindi na Wayahudi, kama hula riba, na huwa wananchi hafifu ya moyo, na hukataa kutumia utaratibu na hesabu za Ulaya katika daftari zao, na hushirikiana pamoja na waasi, ingawa hulinda uhusiano wao wa Uingereza.
Machemba, yule mporaji wa watumwa wa kusini, aliyepeana mikono na Hassan bin Omari, ambaye awali aliishi kwa amani na Wajerumani baada ya kufanya mapatano nao, aliharibu kazi tena kwa kuvunja ahadi na kushikwa na hofu ya kushambuliwa, akatoroka kwenda Msumbiji mwaka 1899, na baadaye akiwa kule akapigana vita na Wareno hadi kifo chake.