DAR ES SALAAM-Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Dkt. Jim Yonazi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanafunzi waliosoma Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM Alumin) ambao unajumuisha Watumishi na Wanafunzi waliosoma katika chuo hicho na ambao kwa sasa wanafanya kazi maeneo mbalimbali hapa nchini wamekabidhi vifaa vya TEHAMA ikiwemo projector tatu kwa uongozi wa chuo hicho jijini Dar es Salam.
Wamekabidhi vifaa hivyo katika hafla iliyoandaliwa na umoja huo na kufanyika katika Ukumbi wa mikutano wa chuo hicho ambapo vifaa hivyo ni sehemu ya michango iliyotokana na Changizo la IFM Alumin Marathon iliyofanyika tarehe 19 Novemba, 2023 jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo Dkt. Yonazi ambaye ni Mwenyekiti wa umoja huo amesema, wamefikia hatua hiyo mara baada ya kuona umuhimu wa kuongeza vitendea kazi kwa uongozi wa chuo hicho ili kuongeza tija katika masuala ya taaluma.
“Tumetoa vifaa hivi kwa lengo la kuendelea kuchochea ufanisi na kusaidia katika kufundisha wanafunzi wanaoendelea na masomo chuoni hapo na kutatua changamoto ya uhaba wa vifaa hivyo, tunaahidi kuendelea kushirikiana kwa kadiri inavyofaa,” alisema Dkt. Yonazi.
Naye Mkuu wa Chuo cha IFM Prof. Josephat amemshukuru kwa namna walivyojitoa na kuona umuhimu wa kufanya hivyo na kueleza kuwa, hatua hiyo imewapa furaha na faraja nakupongeza kwa namna walivyojitolea huku akiahidi kutunza na kuvitumia vifaa hivyo kama ilivyokusudiwa.
“Vifaa hivi vimekuja wakati sahihi na vitatusaidia sana katika kufundishia wanafunzi wetu, tuendelee kuwashukuru kwa namna mlivyojitoa kwa ajili ya Chuo chetu,” alisema Prof. Josephat.