DAR ES SALAAM-Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa January Makamba amesema, taarifa walizopokea kutoka nchini Israel zinadai, mwanafunzi Joshua Mollel aliyetekwa na Hamas ameuawa.
Hayo ni kwa mujibu wa taarifa ambayo Mheshimiwa Makamba ameibandika katika ukurasa wake wa X huku akifafanua kuwa, wanaendelea na mpango wa awali ili kwenda kupata taarifa za ziada.
"Tumejulishwa na Serikali ya Israel kwamba Joshua Mollel, kijana wa Kitanzania aliyekuwa anasoma nchini Israel, na ambaye tulipoteza naye mawasiliano tangu tarehe 7 Oktoba 2023, na ambaye Serikali imekuwa inafanya jitihada kubwa kupata taarifa zake tangu wakati huo, aliuawa mara tu baada ya kutekwa na kundi la Hamas mnamo tarehe 7 Oktoba 2023.
"Nimeongea na Mzee Mollel, baba mzazi wa Joshua, kuhusu ujumbe huo wa Serikali ya Israel.
"Tunaendelea na mpango wa awali wa kuwapeleka Mzee Mollel na mwanafamilia mwingine pamoja na Afisa wa Serikali nchini Israel, kuungana na Balozi wetu na maafisa waliopo huko, kukutana na kuzungumza na mamlaka za nchi hiyo ili kupata taarifa za ziada.
"Kwa ridhaa ya familia, na itakapobidi, tutatoa taarifa za ziada katika siku zijazo,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Makamba.