KAGERA-Uongozi wa Klabu ya Kagera Sugar ya mkoani Kagera umefikia uamuzi wa kumfuta kazi Kocha Meck Mexime.
Uamuzi huo unakuja ikiwa ni siku moja tu baada ya kupokea kichapo cha mabao 4-0 kutoka kwa Azam FC mchuano wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.
Uamuzi huo umefikiwa baada ya Kagera Sugar kuwa na mwendo wa kusuasua kwenye michuano ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania ikiwa wameshuka dimbani mara 13 na kukusanya alama 13 tu.
Mexime alijiunga na Kagera Sugar katikati ya msimu uliopita kuchukuwa nafasi ya Kocha raia wa Kenya, Francis Baraza.
Mbali na Mexime, pia Kagera Sugar wametangaza kuachana na Kocha wao wa viungo, Francis Mkanula.
"Tumefikia maamuzi ya kuachana na Kocha Mkuu, Mecky Mexime, vile vile tumeachana na Kocha wa Viungo Francis Mkanula."
Kwa mujibu wa Kagera kikosi cha timu hiyo kitakuwa chini ya Kocha wa mpito, Marwa Chamberi ambaye ataongoza timu wakati zoezi la kusaka kocha mpya likiendelea.