NA LWAGA MWAMBANDE
REJEA Biblia takatifu katika kitabu cha Warumi 15:1-3 inasema..."basi imetupasa sisi tulio na nguvu kuuchukua udhaifu wao wasio na nguvu, wala haitupasi kujipendeza wenyewe.
Kila mtu miongoni mwetu na ampendeze jirani yake apate wema ajengwe. Kwa maana Kristo naye hakujipendeza mwenyewe bali kama ilivyoandikwa; "malaumu yao waliokulaumu wewe yalinipata mimi".
Neno linatusisitiza kuchukua udhaifu wao wasio na nguvu ili wapate wema na kujengwa kiimani kwa sisi kuwa sehemu katika shida zao na matatizo yao kwa maana huo wema nasi tutaupata na kujengwa pia.
Kitabu cha Ayubu 1:5 kinatufundisha namna ya kusimama kwa ajili ya wengine, kubeba mizigo ya ndugu, marafiki, majirani, wajane, yatima, familia na wengineo wasiojiweza.
Aidha,kwa habari ya Ayubu biblia inasema...”Basi ilikuwa hapo hizo siku za karamu zao zilipokuwa zimetimia,Ayubu hutuma kwao akawatakasa, kisha akaamka asubuhi na mapema, na kusongeza sadaka za kuteketezwa kama hesabu yao wote ilivyokuwa; kwani alisema,
Yamkini kwamba hawa wanangu wamefanya dhambi na kumkufuru Mungu mioyoni mwao, ndivyo alivyofanya Ayubu siku zote".
Hivyo mizigo ya wengine tuwasaidiao katika Kristo tusichoke wala kukoma mpaka furaha zao zitapowarejea tena na amani ya roho zao ili wapate wema na kujengwa na Bwana na sisi pia.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasema kuwa,kubebeana mizigo hilo ni jambo la ki-Mungu, Endelea;
1.Funika aibu zao, siyo kuwaaibisha,
Yajenge maisha yao, wala si kuyafifisha,
Kwenye kumbukumbu zao, utazidi kuwakosha,
Kubebeana mizigo, hilo jambo la KiMungu.
2.Mwaka wa kuaibisha, sasa ndiyo umekwisha,
Tukimaliza mkesha, mema nenda sababisha,
Nenda watu furahisha badala ya kuwakomesha,
Kubebeana mizigo, hilo jambo la KiMungu.
3.Tarehe moja anzisha, pendo na kulizidisha,
Ubadilishe maisha, mimi ninakufundisha,
Fanya yanayoridhisha, amani utadumisha,
Kubebeana mizigo, hilo jambo la KiMungu.
4. Hakuna mkamilifu, Neno wanatufundisha,
Kuna mambo ya kukifu, sote yanatutonesha,
Lakini utakatifu, msamaha sababisha,
Kubebeana mizigo, hilo jambo la KiMungu.
5.Mwanadamu ameumbwa, mema anaadhimisha,
Wachache ni kama mbwa, ambao waaibisha,
Nawe ndio unaombwa, fanya ya kufurahisha,
Kubebeana mizigo, hilo jambo la KiMungu.
6.Mtu ukimwaibisha, kifo utasababisha,
Kwani aweza kukesha, na mawazo ya kuchosha,
Ila ukimweshimisha, afya utaizidisha,
Kubebeana mizigo, hilo jambo la KiMungu.
7.Mungu utusaidie, upate tuelimisha,
Wala tusifurahie, wengine kuaibisha,
Hofu itutangulie, kwamba hujatutowesha,
Kubebeana mizigo, hilo jambo la KiMungu.
Lwaga Mwambande (KimpaB)