MOROGORO-Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Prof. William Mwegoha leo Desemba 11, 2023 amekutana na kuongea na baadhi ya wanafunzi wanaotarajia kushiriki michezo mbalimbali katika Mashindano ya Vyuo Vikuu (TUSA) 2023 yanayotarajiwa kufanyika jijini Tanga kuanzia Desemba 13 hadi 21, 2023.
Prof. Mwegoha amewaasa wanamichezo hao kuipeperusha vema bendera ya Chuo Kikuu Mzumbe kwa kuendeleza nidhamu, uadilifu na maadili mema ya kitanzania.
“Mkumbuke mmebeba taswira ya Chuo Kikuu Mzumbe, mkimwakilisha Mkuu wa Chuo Dkt. Ali Mohamed Shein, Mwenyekiti wa Baraza Prof. Saida Yahya-Othman na Uongozi wote. Ninawatakia kila la heri, mje na vikombe vingi zaidi kama mfanyavyo miaka mingine, mmebeba dhamana ya Chuo, mkatuheshimishe,”amesisitiza Prof. Mwegoha.
Awali Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi Bi. Mariam Mattao amesema wamejiandaa vema kushiriki katika michezo hiyo huku akimhakikishia Makamu Mkuu wa Chuo ushindi katika michezo mbalimbali watakayoshiriki.
Naye, Rais wa Wanafunzi wa Chuo Kikuu Mzumbe Bw. Edwin Ntabindi amemuomba Kaimu Mkuu wa Chuo na viongozi wengine kutembelea washiriki wa michezo hiyo wakiwa kambini Tanga kwa lengo la kuwatia moyo.
Sambamba na nasaha za Makamu Mkuu wa Chuo kwa wanamichezo hao, Prof. William Mwegoha pia amewakabidhi bendera ya Chuo Kikuu Mzumbe na kuwataka kuipeperusha vyema.
Kikosi cha wanamichezo kutoka Chuo Kikuu Mzumbe kimehusisha wanafunzi kutoka Kampasi Kuu Morogoro, Ndaki ya Dar es Salaam na Ndaki ya Mbeya.
Tags
Chuo Kikuu Mzumbe
Habari
Michezo
Mzumbe University
Vyuo Vikuu vya Tanzania
ya Vyuo Vikuu (TUSA)