NA MWANDISHI WETU
KUHANI Mkuu aliyeitwa Kayafa anatusimulia kwamba, Yesu aliyekuwa mtoto mchanga wakati huo, alimsemesha mama yake kabla ya kukua akiwa katika kitanda cha watoto wachanga.
Yesu alisema,"Maria, mimi mtoto wa Mungu, Yesu Kristo, uliambiwa neno na malaika Gabriel kuwa utazaa, Baba yangu amenileta mimi kwaajili ya ukombozi wa ulimwengu."
Katika miaka mia tatu na tisa wakati wa utawala wa siku zile, amri ilitoka kwa Kaisari Alexander Augusto ya kwamba iandikwe orodha ya majina ya watu wote wa ulimwengu.
Yusuphu pia akaondoka na Maria na kuelekea Yerusalemu, hadi Bethlehemu ambapo yeye na familia yake wangeweza kwenda kuhesabiwa katika jiji la baba zake.
Na mara waliporudi katika pango, Maria alikiri kwa Yusuphu kwamba muda wake wa kujifungua ulikuwa umefika, na asingeweza kurudi mjini, na akamwambia, "tuingie ndani ya pango lile."
Kipindi hicho jua lilikuwa linakaribia kutua, Lakini Yusuphu akatoka haraka kwenda kumtafutia mkunga, akiwa njiani akamuona mwanamke mzee Mwebrania wa Yerusalemu, akamwambia, "naomba twende kule kwenye pango mwanamke mwema, na utamuona mwanamke ambaye anakaribia kujifungua."
Ilikuwa tayari jua limetua wakati yule mwanamke mzee na Yusuphu wanafika pangoni, kisha wakaingia ndani. Na tazama, pango lote lilikuwa limejaa mwangaza mkubwa kuliko mwanga wa taa na mishumaa, na mkubwa kuliko jua lenyewe.
Kachanga kalikuwa kameviringishwa kwa kitambaa akiwa ananyonya maziwa ya mama yake mtakatifu Maria. Mara wote walipoiona nuru ile wakashangaa sana, Bibi akamuuliza Maria, wewe ni mama wa mtoto huyu,? Maria akamjibu, ndio mimi.
Yule Bibi akamwambia, upo tofauti sana na wanawake wengine wote.Na mara muda wa siku ya nane ulipofika wa kumtahiri mtoto uliwadia, kama sheria inavyotaka mtoto alipaswa kutahiriwa.
Na mwanamke mzee mwebrania akachukua kitovu na kukihifadhi katika boksi la chupa za kuhifadhia mafuta ya manukato.
Na alikuwa na kijana ambaye anauza madawa, akamwambia, chukua tahadhari usiuze hili boksi la mafuta, ingawa ni lazima utalipwa dinari mia tatu kwaajili ya hilo.
Hili ndilo boksi la mafuta ambalo Mariamu mdhambi alilinunua, na kummiminia Yesu mafuta kichwani na miguuni na kuyafuta kwa kutumia nywele za kichwani mwake.
Halafu baada ya siku kumi kupita, wakampeleka Yerusalemu, na siku ya kumi na nne, toka kuzaliwa kwake wakampeleka ndani ya hekalu la Mungu, wakamtolea sadaka kulingana na sheria ya Musa, kwamba, kila mwanaume anayefungua tumbo ataitwa mtakatifu kwa Mungu.
Kipindi hicho Simeoni alimwona Yesu akin'gaa kama nguzo ya taa, wakati mtakatifu Bikira Maria amembeba mikononi mwake na alikuwa kajazwa na furaha kubwa kwa mtazamo.
Na malaika walikuwa wamesimama wakimzunguka pande zote, wakimwabudu, kama walinzi wa Mfalme wakimlinda.
Kisha Simeoni akamsogelea Maria, na yeye mwenyewe akampokea mikononi mwake, akamshukuru Mungu, akisema, Sasa, Bwana, wamruhusu mtumishi wako, Kwa amani, kama ulivyosema; Kwa kuwa macho yangu yameuona wokovu wako, Uliouweka tayari machoni pa watu wote.
Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake.
Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba.
Huyu alitokea saa ile ile akamshukuru Mungu, na wote waliokuwa wakiutarajia ukombozi katika Yerusalemu akawatolea habari zake.
Na ikafika wakati ambapo Yesu Kristo alipozaliwa Bethlehemu jiji la Yudea, kipindi cha utawala wa Mfalme Herode, Mamajusi (Wise men) wa Mashariki walikuja Yerusalemu, kulingana na utabiri wa nyota wakamsujudia na kumpa hazina zao za, tunu, uvumba, manemane na dhahabu.
Halafu Maria akachukua Moja ya nguo alizomfunikia kichanga kisha akawapa mbadala wa baraka, ambayo waliipokea kama zawadi nzuri na kubwa.
Wakati huohuo akajitokeza malaika katika umbo la nyota, huyu alikuwa mlinzi wao kabla katika safari yao, alikuwa ni mwanga waliokuwa wanaufuata mpaka waliporudi katika nchi yao.
Wakati wanarudi Wafalme na Malkia wao, walikuja wakataka kujua nani walimuona na alifanya nini?, aina gani ya safari waliyoifanya na kurudi kwao, na usaidizi gani waliupata wakiwa barabarani?
Maria akawatolea nguo ya mtoto Yesu kisha akawapa, kwaajili ya hilo wakafanya sherehe. Kisha kulingana na desturi za nchi, wakawasha moto, kisha wakaiabudu. Wakautupa ule mbebeo katika moto, moto ukaichoma na kuiacha.
Na mara moto ulipozima wakaichukua Ile nguo ikiwa haijadhurika na moto, kana kwamba moto haukuigusa.
Halafu wakaanza kuibusu, na kuiweka vichwani mwao na machoni mwao wakisema, huu hakika ni ukweli usio na shaka na kiukweli inashangaza kwamba moto umeshindwa kuiunguza nguo na kuiteketeza?.
Kisha wakaichukua na kwa heshima kubwa wakailaza katika kati ya hazina zao.Sasa Herode akatambua kuwa wale Mamajusi wamechelewa na kutorudi kwake, akawaita kwa pamoja kuhani na wenye hekima na kuwaambia;" niambieni ni mahali gani atakuwa kazaliwa Yesu Kristo."
Na mara walipomjibu kuwa ni Bethlehemu, Jiji la Yudea, akaanza kupanga katika akili yake kuhusu jinsi ya kumuua Yesu Kristo.
Lakini malaika wa Mungu akamtokea Yusuphu akiwa ndotoni, na kumwambia, amka umchukue mtoto na mama yake na elekeeni Misri mara tu jogoo atakapowika. Hivyo akaamka na kuondoka.
Yusuphu akawa akifikiria kuhusu safari yake ilipofika asubuhi hiyo. Kutokana na umbali wa safari wakiwa njiani kamba ya kufungia mizigo ya farasi ikakatika.
Mara akakaribia katika Jiji kubwa, ambapo kulikuwa na masanamu ya Mungu ambapo makuhani wa miungu na masanamu mengine wa Misri walileta sadaka na nadhiri.
Pakawa na sanamu ambalo kuhani analihudumu, ambalo mara kwa mara lina uhusiano na vitu anavyosema kwa wakazi wa Misri na hizo nchi.
Kuhani huyu alikuwa na kijana mwenye miaka mitatu aliyekuwa ana sumbuliwa na mapepo mengi sana, na wakati shetani anapomkamata huwa anatembea uchi na nguo zake zilizochanika, anawatupia mawe anaowaona njiani.
Karibu na sanamu hilo palikuwa na mkahawa wa Jiji, ambapo Yusuphu na Maria walikuwa wanakuja kupita na mara sanamu hilo likageukia kwenye mkahawa wakazi wote wa Jiji wakashangaa sana.
Na majaji wote na makuhani wa masanamu wakakusanyika mbele ya sanamu, na kuulizia pale, wakasema, Nini maana ya hofu hii yote, ambayo imeangukia katika nchi yetu.
Kisha wakaelekea katika jiji lingine ambapo palikuwa na mwanamke anamilikiwa na shetani, na shetani huyo mwasi aliyelaaniwa alichukua makazi yake.
Usiku mmoja wakati amekwenda kuchota maji, hakuweza kuvumilia akazivua nguo zake alizovaa, au hakutaka kuishi katika nyumba yoyote, lakini mara kwa mara wanapomfunga kwa minyororo na kamba aliivunja na kukimbilia maeneo ya jangwani, na wakati mwingine alisimama barabarani au kanisani na kuwarushia mawe wapita njia.
Maria alipomuona mwanamke huyu, alimuonea huruma, baadaye shetani anapomuacha huwa anakimbia akiwa katika umbo la kijana mdogo, akisema, nionee huruma kwasababu yako Maria na mtoto wako.
Mwanamke huyo akapona katika mateso yake, lakini akajikuta yupo uchi, akaona haya na kukwepa kuonekana na wanaume baada ya kuvaa nguo akaenda nyumbani, kisha akamsimulia baba yake, wao walikuwa ni watu maarufu katika Jiji kwa Sanaa, hivyo wakawaburudisha Maria na Yusuphu kwa heshima kubwa.
Asubuhi iliyofuata wakapokea mahitaji yote ya safari yao wakaondoka kwao, na ilipofika jioni wakawasili katika mji mwingine, ambapo palikuwa na ndoa inatakiwa kufungwa kanisani, lakini kutokana na michezo ya shetani na wachawi Bibi harusi alikuwa amepigwa uchawi na kuwa bubu, akawa anashindwa kufungua mdomo wake.
Lakini wakati huyu Bibi harusi bubu anamuona Maria anaingia mjini, huku amembeba Bwana Yesu mikononi mwake, akanyosha mikono yake kwa Yesu na kumchukua mikononi mwa Maria, kisha akamkumbatia, mara chache alimbusu, akaendelea kwa kumpakata mwilini mwake.
Mara moja uzi wa ulimi wake ukafunguka, masikio yake yakafunguka akaanza kuimba akimsifu Mungu, aliyemponya.
Hivyo pakawa na furaha kubwa usiku, kati ya wakazi wa mji ule walifikiria kuwa Mungu akiwa na malaika zake wameshuka miongoni mwao. Katika eneo hili wakakaa siku tatu, wakikutana na heshima kubwa na burudani tukufu.
Baada ya kupewa mahitaji ya njiani na watu, wakaondoka kuelekea mji mwingine ambapo wakakaribishwa nyumba ya kupanga kwasababu lilikuwa ni jiji maarufu. Wakaja baadaye kwenye Jiji lingine wakawa na mawazo ya kupangisha chumba kule,
Walitoka wakaelekea katika nyumba ya mtu ambaye ana ndoa mpya iliyoshinikizwa kwa nguvu ya wachawi, hivyo akawa hafurahii maisha ya ndoa na mke wake.
Lakini wakapanga katika nyumba yake usiku ule, yule mtu alikuwa anapata shida kwa vurugu za mke. Wakati wanajiandaa baada ya kukucha asubuhi waendelee na safari yule kijana mwenye ndoa mpya akawazuia na kuwafanyia burudani nzuri baada ya mke wake kutulizwa mapepo.
Kesho yake wakaelekea katika jiji lingine, wakawaona wanawake watatu wanaelekea katika kaburi fulani wakiwa na na kilio kikubwa.
Mara Maria alipowaona akaongea na msichana aliyekuwa nao, akasema, nenda na uwaulize wamepatwa na tatizo gani? Na bahati mbaya gani imewapata?
Yule msichana alipowauliza hawakumjibu, akawauliza tena, ninyi ni akina nani? Na wapi mnapokwenda?, mchana unaishia na usiku unakaribia.
Msichana mmojawapo, akasema, tunatafuta nyumba ya wageni ili tupange. akamjibu, twende pamoja nasi na tupange pamoja. Kisha wakawafuata, wakatambulishwa katika nyumba mpya, ambayo ilikuwa ina samani za kila aina.
Kikaja kipindi cha baridi, na yule msichana akaelekea sebuleni walipokuwepo wale wanawake, akawakuta wanalia na kulalamika kama mwanzo. Kati yao alisimama mwanapunda kafunikwa kwa hariri, na skafu nyeusi inaning'inia chini ya shingo yake, walikuwa wanambusu na kumlisha.
Lakini wakati msichana yule anawaongelesha, jinsi gani alivyo mzuri yule mwanapunda, wale wanawake, wakamjibu wakilia, na kusema, Huyu mwanapunda unayemuona alikuwa kaka yetu, tumezaliwa mama mmoja na yeye.
Baba yetu alipofariki akatuachia eneo kubwa sana, tulikuwa na kaka yetu huyu pekee, tukajitahidi kumkuwadia mwanamke anayemfaa, tukidhani ataoa kama wenzake, baadhi ya wanawake wenye wivu wakamroga bila sisi kujua.
Usiku mmoja kabla hakujapambazuka, wakati milango imefungwa ghafla, tulimuona kaka yetu kageuka na kuwa mwanapunda, kama unavyomuona alivyo sasa.
Tukiwa katika hali ya huzuni kama unavyotuona sasa, hatuna baba wa kutufariji, tumewaona watu wenye busara, waganga, na wapiga ramli duniani lakini hawakutupa huduma yoyote.
Mara kwa mara tunajikuta katika huzuni, tukiamka tutakwenda pamoja na mama yetu huyu kwenye kaburi la baba yetu, ambapo tutalia tukitosheka tutarudi nyumbani.
Msichana aliposikia haya, akawaambia, muwe jasiri, ondoeni woga, tayari mmepata njia ya utatuzi, kwa mateso kati yenu na nyumbani kwenu.
Mimi mwenyewe nilikuwa na ukoma, lakini wakati nilipomuona huyu mwanamke, na huyu kichanga chake anayeitwa Yesu, nilijimwagia maji ambayo mtoto wake alikuwa kayaoga na mara nikapona kabisa.
Na nina uhakika anauwezo wa kuwasaidia kwenye janga lenu, mkiamka nendeni kwa bimkubwa wangu Maria, na mkimleta kwenye sebule yenu mwambieni siri hii, wakati huohuo muombeni kwa bidii awaonee huruma katika shida yenu.
Mara walipomaliza majadiliano na yule msichana wakaelekea upesi kwa Bikira Maria, wakajitambulisha kwake, na kukaa mbele yake wakilia.
Wakasema, Eeh mama yetu waonee huruma wahudumu wako, hatuna kiongozi wa familia, katika familia yetu hakuna aliye mkubwa zaidi yetu, hatuna baba wala kaka.
Lakini huyu mwanapunda, unayemuona, alikuwa ni kaka yetu, baadhi ya wanawake walimgeuza kichawi na kuwa katika hali hii unayoiona, kwahiyo tunakuomba utuhurumie, na mara kaka yao akapona baada ya kuguswa na mbebeo wa Yesu.
Katika safari yao wakafika katika nchi yenye jangwa na waliambiwa mapema kuwa palikuwa na vibaka sana, hivyo Yusuphu na Maria wakajiandaa kuvuka wakati wa usiku.
Na walipokuwa wapo njiani, tazama, wakawaona wezi wawili wamelala barabarani, wakiwa na kundi kubwa la wenzao waliokuwa wameungana pamoja nao, pia wamelala.
Majina ya wale wezi wawili waliitwa,Titus na Dumachus. "Naomba watu hawa wapite kimyakimya, kwani kundi letu halitapata chochote kwao," alisema Titus.
Lakini Dumachus akakataa, Titus akasema tena, nitawapa unga wa nafaka uliokobolewa gunia 40, na ninawapa ahadi chukueni mkaja wangu, ambao aliwapa kabla ya kuanza kuongea, kwamba asingeweza kufungua mdomo wake au kupiga kelele wakiwa wanapita watu wale.
Wakati mtakatifu Bikira Maria anaona huruma ambayo vibaka wale wameionyesha kwao, akawaambia, Bwana Mungu atawapokea kwa mkono wake wa kulia na kuwapa msamaha kwa dhambi zao.
Kisha Bwana Yesu akajibu, akamwambia mama yake, "ikifika miaka 30, Ewe mama, wayahudi watanitundika msalabani pale Yerusalemu na hawa wezi wawili kipindi hicho watakuwa pamoja na mimi juu ya msalaba, Titus upande wa kulia na Dumachus kushoto kwangu, na toka muda huo Titus atakwenda peponi kabla yangu.
Na mara alipomaliza kuongea, Maria akasema, Mungu pishia mbali hili halipaswi kuwa Eeh mwanangu. Walikwenda mjini ambapo palikuwa na masanamu kadhaa ambayo mara moja walipoyakaribia yaligeuka kuwa vilima vya mchanga.
Kwa sababu hiyo wakaenda kwenye mti ule wa mbuyu ambao sasa unaitwa Matarea. Na pale Matarea bwana Yesu alisababisha chemchemi ya maji kuwa kisima ambapo Bikira Maria alifua koti la Yesu.
Na Balsamu ilizalishwa au kukua katika nchi ile, kutokea katika kisima kilichosababishwa na Bwana Yesu.Kutoka pale wakaendelea hadi Memphis na kuonana na Farao, na kukaa Misri kwa muda wa miaka mitatu.
Hatimaye wakafika katika Jiji la Bethlehemu, kule wakakuta ugonjwa wa mbwa na wanyama wengineo uliowakatisha tamaa watu, uliokuwa unasumbua sana watoto kwa kuwaangalia na wengi wamefariki.
Palikuwa na mwanamke aliyekuwa na mtoto mgonjwa, alimleta kwa Bikira Maria alipokuwa anakaribia kufa, akaenda kumuona wakati anamuogesha Yesu. Kisha yule mwanamke akasema, Eeh mama Maria, umwangalie mwanangu, anasumbuliwa na maumivu makali ya ugonjwa unaotisha.
Mtakatifu Maria akamsikia, akamwambia chukua maji kidogo niliyomuogeshea mwanangu, na kisha mmiminie. Kisha akachukua yale maji kiasi na kummwagia mwilini, kama alivyoambiwa na Maria, mtoto wake aliyekuwa anasumbuliwa na maumivu makali, alikuwa kalala kidogo, baada ya kuamka akawa amepona kabisa.
Mama akajawa na furaha tele ya mafanikio yale, akaenda tena kwa Maria, na Maria akamwambia, msifu Bwana Mungu ndiye aliyemponya mtoto wako.
Palikuwa na mwanamke mwingine eneo lilelile, jirani yake, ambaye kijana wake aliponywa, kijana wa mwanamke huyu alikuwa anasumbuliwa na ugonjwa uleule ,na macho yake yalikuwa yanakaribia kufumba, alikuwa anamnung'unikia usiku na mchana.
Mama wa mtoto aliyeponywa, akamwambia, kwanini hukumleta mwanao kwa mtakatifu Maria kama nilivyompeleka mwanangu alipokuwa anakaribia kufa na kuponywa na yale maji ambayo mtoto wake Yesu aliyaoga?.
Yule mwanamke aliposikia alichosema, akaenda na kumuosha mtoto wake kwa maji yaleyale na mara akapona macho yake na maumivu.
Katika mji ule palikuwa na wake wawili wa mwanaume mmoja, ambao kila mmoja mtoto wake alikuwa mgonjwa, mmoja aliitwa Maria ambaye mtoto wake aliitwa Caleb.
Aliamka na kumchukua mwanae akaelekea kwa mtakatifu Maria, akampa zawadi ya kapeti, akamwambia, Eeh mama yangu Maria pokea kapeti langu, na badala yake nipe mbebeo wa Yesu.
Hivyo Maria alikubali, akampa, na Mama Caleb akaondoka na mbebeo, akaenda kutengeneza koti kwaajili ya mwanae, akamvalisha mara ugonjwa wake ukapona. Baadae zikaibuka tofauti kati yao wakati wa kufanya zamu za biashara ya familia yao, za kila wiki.
Wakati wa zamu ya Maria, Mama yake na Caleb ilipofika, alikuwa akioka mikate kisha akaondoka kuelekea kuchukua chakula, akamuacha mtoto wake Caleb karibu na Oveni.
Mke mwenza, yule adui yake, alipoona yupo peke yake akamchukua Caleb na kumtupia ndani ya moto wa Oveni uliokuwa mkali sana, kisha akaondoka.
Maria aliporudi akamuona mwanae katikati ya moto anacheka na Oveni ina ubaridi utadhani haikuwa na moto, akagundua kuwa mke mwenza, yule adui yake, atakuwa alimtupia mwanae ndani ya moto.
Akamtoa nje ya Oveni, akampeleka kwa mtakatifu Maria na kumsimulia habari Ile, Bikira akamwambia, Kaa kimya, usilifanye jambo hili kujulikana kwa watu.
Baada ya hili, adui yake yule mke mwenza, akiwa anachota maji kisimani ghafla akamuona Caleb anacheza karibu na kisima, na hapakuwa na mtu karibu, akamchukua na kumtumbukiza ndani ya kisima.
Wakatokea wanaume kadhaa kuja kuchota maji kisimani, wakamuona kijana mtoto amekaa juu ya maji, wakamtoa kwa kamba, wakaendelea kumshangaa mtoto yule na kumsifu Mungu.
Akaja mama yake na kumchukua hadi kwa Bikira Maria, akinung'unika na kusema, Eeh Mama Maria, ona jinsi mtesi wangu anachomfanyia mwanangu, na jinsi alivyomtumbukiza ndani ya kisima, ila sitamuuliza kitu lakini siku moja atakuja kumuua mwanangu.