ZANZIBAR-Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba Sheria,Utumishi na Utawala Bora,Mheshimiwa Haroun Ali Suleiman amesema maamuzi ya Kuadhimisha Siku ya Maadili na Haki za Binadamu ni Kuungana na mataifa mengine Duniani katika harakati za mapambano dhidi ya rushwa na haki za binadamu.
Ameyasema hayo ofisini kwake Mazizini alipozungumza na Waandishi wa Habari wakati akitoa taarifa ya Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binaadamu.
Aidha, amesema siku hiyo inatokana na tamko la Kimataifa lililoidhinishwa na Kupitishwa na Baraza kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 10 Disemba mwaka 1948, hivyo Serikali zote mbili nchini Tanzania zimekubaliana kuadhimisha siku hiyo ya Kitaifa.
Akizitaja taasisi zinazohusika na Usimamizi wa Maadili na Haki za Binaadamu amesema ni Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Uhujumu Uchumi, Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Idara ya Utawala Bora na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.
“Kupitia siku hii taasisi hizi hufanya shughuli mbalimbali za uimarishaji wa misingi ya utawala bora nchini ikiwemo kuratibu matukio yenye mnasaba na maadili, haki za binadamu,mapambano dhidi ya rushwa uwazi na uwajibikaji,”amesema Waziri.
Hata hivyo,Waziri Haroun amesema, Maadhimisho hayo kila mwaka hubeba Ujumbe maalum ambapo ujumbe wa mwaka huu ni “TUIMARISHE UTAWALA BORA NA HAKI ZA BINADAMU KWA KUONDOA UBADHIRIFU NA KUKUZA MAADILI KWA USTAWI WA JAMII”.
Siku ya Madili na Haki za Binadamu huadhimishwa kitaifa kila ifikapo Tarehe kumi Disemba ya kila mwaka, aidha kwa kua siku ya tarehe tisa Desemba ni Siku ya Uhuru wa Tanganyika hivyo Siku ya Maadili na Haki za Binadamu kwa mwaka huu itadhimishwa tarehe 12 Disemba, katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdul Wakil Kikwajuni Zanzibar.