MAAFA KATESH:Dar es Salaam watoa pole na kukabidhi msaada

DAR SALAAM-Viongozi wa Mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa mkoa, Albert Chalamila wametoa salamu za pole kwa waathirika wa maaafa ya mafuriko wilayani Hanang’ mkoani Manyara.
Katika salamu hizo viongozi hao wametoa vifaa ikiwemo magodoro 250, mablanketi ya wakubwa 1200 na ya watoto 300, sabuni katoni 100, mikeka 500, ndoo ndogo 350 ambazo zina ujazo wa lita 10 na ndoo kubwa zenye ujazo wa lita 20 wametoa 350, sahani 500 na seti za kupikia 20.

"Tunatoa pole kwa watanzania wenzetu ambao wamefikwa na maafa hayo, sisi wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam na mimi Mkuu wao wa Mkoa, tunaungana na viongozi wa Mkoa wa Manyara na hasa Mkuu wa Mkoa huo, Queen Sendiga kumpa pole za dhati kabisa,”amesema Chalamila.

Aidha, amesema majanga yaliyotokea Hanang yachukuliwe kama somo na yanaweza kutokea sehemu yoyote.

“Nitoe wito kwa wakazi wa Mkoa wa Dar es Salaam kuendelee kuchukua tahadhari, kuhama mabondeni, kufungua njia za maji, kufanya usafi ili kuepuka magonjwa ya mlipuko ikiwemo kipindupindu,”amesema.

Amesema, Dar es Salaam ni mji muhimu kwa mengi ikiwemo biashara, diplomasia, na uchumi hivyo tatizo lolote likitokea litagharimu maisha ya wengi.

"Natoa wito kwa wakazi wa Dar es Salaam kuulinda mji huu kama mboni ya jicho kwa maslahi mapana ya taifa letu," alisisitiza.

Desemba 3, mwaka huu wakazi wa Hanang' walikumbwa na mafuriko ya maji yaliyoambatana matope, mawe na magogo na kusababisha vifo na majeruhi kwa watu na mifugo, na uharibifu wa miundombinu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news