MANYARA-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wakazi wa mji mdogo wa Katesh walioathirika na mafuriko makubwa kuwa Serikali itarejesha huduma zote za msingi za kijamii.
Rais Dkt.Samia amesisitiza kuwa serikali itaendelea kufanya tathmini ya uharibifu wa mali huku akiiagiza Wizara ya Nishati kuangalia uwezekano wa upatikanaji wa umeme wa dharura baada ya miundombinu kuharibika na maafa haya ili shughuli za uopoaji zifanyike usiku na mchana.
Rais Samia ametoa kauli hiyo Desemba 7, 2023 wakati akizungumza na wananchi na waathirika mara baada ya kutembelea maeneo yaliyoathirika na mafuriko hayo na kushuhudia hali halisi ya uharibifu wa maafa.
Aidha, Rais Dkt.Samia ameongeza kuwa mbali na michango mbalimbali iliyotolewa ndani ya nchi, lakini pia kumetolewa takribani shilingi bilioni 2.5 kutoka kwa wahisani walioshiriki kwenye mkutano wa COP 28, Dubai.
"Baada ya maafa yaliyochukua uhai wa baadhi ya ndugu zetu, kazi ya kuurudisha mji mdogo wa Katesh pamoja na vijiji jirani katika hali ya kawaida sasa inaendelea.
Waathirika wa maafa haya waliopo kwenye matibabu tutaendelea kuwahudumia mpaka pale watakaporejea katika hali ya kawaida. Wale walio kwenye kambi tutaendelea kuhakikisha wanapata huduma zote muhimu.
Nimeagiza pia uwepo wa huduma ya kisaikolojia kama sehemu ya tiba kwa madhila waliyopitia ndugu zetu hawa. Sambamba na hayo, nimewaeleza kwamba Serikali itashirikiana na wadau mbalimbali kuwapatia makazi.
Nawakumbusha wale tuliowapa jukumu la kuratibu misaada hii kwa ndugu zetu kuwa fedha za majanga si fedha za kumnufaisha mtu binafsi, hivyo basi, uadilifu uzingatiwe.
"Tutumie fedha hizi kwa lengo lililokusudiwa ambalo ni kuwahudumia waathirika, kufanya marekebisho na kuwafariji ili waweze kurejea katika maisha yao ya kawaida,"alisisitiza Mhe.Rais Dkt.Samia.