MAAFA KATESH:TFRA kuweka mfumo thabiti mbolea za misaada kuwafikia walengwa

MANYARA-Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA), Joel Laurent amesema, mamlaka hiyo inaweka mfumo sahihi utakaohakikisha mbolea za msaada kwa waathirika wa mafuriko wilayani Hanang' mkoani Manyara ili kuhakikisha zinawafikia walengwa.
Amesema,taarifa za wakulima waliojisajili katika eneo lililoathiriwa zipo na kutoa wito kwa wale ambao bado hawajajisajili kufanya hivyo ili kupata mbolea hizo.
Laurent ameeleza hayo Desemba 8, 2023 kwenye kituo cha kilimo alipokuwa akifanya makabidhiano maalum na Kamati ya Maafa kupitia Afisa Kilimo wa Wilaya ya Hanang', Liberatus Msasa.
Amesema,Ofisi ya Kilimo wilayani Hanang' itashirikiana na Ofisi ya Mamlaka Kanda ya Kaskazini kuhakikisha Afisa Kilimo anasajiliwa kama wakala na kuingiziwa mbolea hizo kwenye Akaunti yake ili aweze kuzigawa kwa waathirika bure kwa utaratibu uliowekwa.

Amehitimisha mazungumzo yake kwa kutoa pole kwa waathirika wote na kuwaombea majeruhi warejee katika hali zao za kawaida na wale waliotangulia mbele ya haki pumziko la amani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Uzalishaji wa Ndani na Ununuzi wa Mbolea kwa Pamoja wa TFRA, Louis Kasera ametoa shukrani kwa wadau wote waliochangia na kuwezesha kupatikana kiasi cha tani 78.5 za mbolea.
Amesema,kiasi hicho kitawasaidia waathirika kuendelea na shughuli zao za kilimo pasipokuwa na shida kwani watapokea mbolea za kupandia na kukuzia.

Naye, Afisa Kilimo wa Wilaya ya Hanang', Liberatus Msasa, ameshukuru kwa msaada huo na kueleza wilaya yake unategemea kilimo kwa asilimia 80 na kueleza sekta hiyo imeathiriwa na janga hilo.
Ameahidi kusimamia ugawaji wa mbolea hizo na kuhakikisha walengwa ndio wanaonufaika na pembejeo hiyo muhimu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news