DODOMA-Waziri wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Mhe. Jenista Mhagama amepokea fedha taslimu kiasi cha shilingi 2,034,000.50 kutoka kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI,Mhe. Mohamed Mchengerwa ikiwa kama sehemu ya mchango wa Walimu Wakuu wa shule za sekondari nchini kwa waathirika wa maafa ya maporomoko ya matope na mawe kutoka mlima Hanang’.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu ),Mhe. Jenista Mhagama akipokea mchango wa walimu wakuu wa shule za sekondari nchini kwaajili ya waathirika wa maafa ya maporomoko ya matope na mawe kutoka mlima Hanang' uliowasilishwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI,Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa niaba yao.
Waziri amepokea fedha hizo Desemba 19,2023 ofisini kwake jijini Dodoma, ambapo kwa niaba ya Ofisi ya Waziri Mkuu amewashukuru walimu hao kwa mchango wao.
"Jambo hili la maafa la maporomoko ya matope na mawe kutoka Mlima Hanang’ mafanikio yake yalipatikana na yameongozwa na utashi wa Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Walimu ni viongozi,na wamedhihirisha uongozi wao katika mambo makubwa ikiwa ni pamoja na kutambua kazi kubwa inayofanywa na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kumuunga mkono katika masuala mbalimbali,"amesisitiza Waziri Mhagama.
Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI,Mhe. Mohamed Mchengerwa alisema Walimu hawa kwa ushirikiano wao nchini, “Waliona umuhimu wa kuchangishana na kusaidia waathirika wa maafa yaliyotokea Hanang’ na kunituma nikukabidhi wewe Waziri mwenye dhamana.”