MAAFA KATESH:Waliofariki wafikia 87, Serikali yatoa mkono wa pole milioni 1/- kwa kila mwili

NA GODFREY NNKO

SERIKALI imesema hadi kufikia sasa miili iliyopatikana kutokana na maafa yaliyotokea mji mdogo wa Katesh wilayani Hanang' Mkoa wa Manyara ni 87 na yote imeshatambuliwa na ndugu zao na kuchukuliwa kwa maziko.

Hayo yamesemwa leo Desemba 10, 2023 na Mobhare Matinyi ambaye ni Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali wakati akitoa taarifa ya Serikali ya maendeleo baada ya maafa hayo.

Miili hiyo imepatikana baada ya maafa ya maporomoko ya tope, mawe, magogo na maji kutoka mlima Hanang' wilayani Hanang' mkoani Manyara alfajiri ya Desemba 3, 2023.

Amesema, kwa maelekezo ya Mheshimiwa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan, Serikali inagharamia mazishi yote na kutoa mkono wa pole wa shilingi milioni moja kwa kila mwili.

Msemaji Mkuu wa Serikali amefafanua kuwa,hadi sasa jumla ya majeruhi na wagonjwa waliopokelewa tangu maafa yatokee ni 139, lakini waliopo hospitalini hadi leo ni 30.

"Wagonjwa wengine wote isipokuwa wawili waliofariki wamesharuhusiwa kurejea nyumbani. Wagonjwa 30 waliopo hospitalini hadi kufikia sasa wamegawanyika kama ifuatavyo, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara (19). Hospitali ya Wilaya ya Hanang-Tumaini (8) na Kituo cha Afya Gendabi (3)."

Pia, amesema hadi sasa kambi tatu za waathirika zilishapokea jumla ya waathirika 517, lakini kutokana na juhudi za Serikali hadi sasa waathirika 215 wameshaunganishwa na familia zao na waliobakia kambini ni 302.

Aidha, jumla ya kaya 212 zipo tayari kuunganishwa na familia zao baada ya kupatiwa mahitaji muhimu ya maisha.

Vile vile, tayari waathirika 517 wameshapatiwa huduma za kisaikolojia kutokea kambini na wengine 721 walioko nje ya kambi.

Amebainisha kuwa, Serikali ina jumla ya maafisa ustawi wa jamii 43 wanaotoa ushauri nasaha kwa wananchi walioathirika na maafa hayo.

"Kila kaya inayoondoka kambini inapewa chakula cha siku 30 kwa kufuata mwongozo wa lishe ambacho ni unga, mchele, maharage, mafuta ya kula, sukari, chumvi, maji ya kunywa, jiko la kupikia na watoto wanapewa unga wa lishe.

"Vile vile, kila kaya inapewa godoro, blanketi, duveti, shuka, sufuria, nguo za ndani, taulo za kile, pampasi za watoto, dawa za meno, miswaki, sabuni za miche na unga, sahani, vikombe, beseni na ndoo."

Katika hatua nyingine, Msemaji Mkuu huyo wa Serikali amesema, Serikali inaendelea na juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata maji safi na salama ambapo hadi kufikia sasa ilikuwa imeshazitembelea kaya 2,143 na kutoa elimu ya afya kwa umma pamoja na kugawa jumla ya vidonge 32,154 vya kutibia maji.

Kazi hii amebainisha kuwa, inasimamiwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Prof. Tumaini Nagu. Serikali pia imeongeza wataalamu wa afya ya akili ambapo sasa kuna wauguzi wawili na madaktari bingwa watatu wanaoongozwa na Mkurugenzi Msaidizi wa Magonjwa Yasiyokuwa ya Kuambukiza, Dkt. Omary Ubuguyu.

"Timu hii imeshatoa msaada wa kisaikolojia kwa watu 267 na bado inaendelea. Serikali inaendelea na utambuzi wa mashamba yaliyoharibiwa ili iendelee kutoa msaada wa mbegu na mbolea kwa wananchi walioathirika.

"Tayari kilo 17,000 za mbegu za alizeti, mahindi na ngano zimeshagawiwa kwa wananchi hao. Serikali pia kupitia Wizara ya Maji inatoa huduma za maji kwenye kambi zote tatu, na maeneo muhimu kama hospitali na makazi.

"Visima 10 vinachimbwa kwenye vijiji vilivyoathirika vya Gendabi, Harghushay, Gidamambura, Dajameda, Galagala, Gasaboy, Gidagamowd, Nyabat, Sebasi na Barjomot.

"Aidha, pampu kubwa inafungwa kwenye mradi unaohudumia eneo la Katesh ili kuwezesha upatikanaji wa huduma ya maji kwenye baadhi ya maeneo yaliyoathirika."

Serikali pia inajenga vituo 20 vya kuchotea maji na pia tathmini ya vyanzo vinne vilivyoathirika na mafuriko eneo la Dumanang, Sebasi, Barjomot na Himiti inaendelea.

Bw.Matinyi amefafanua kuwa, Ofisi ya Waziri Mkuu inaendelea kuratibu misaada mbalimbali ya vifaa na fedha taslimu inayotolewa wadau mbalimbali nchini.


Hadi sasa jumla ya fedha ni kiasi cha shilingi 138,645,500 zilizokwishapokelewa kwenye akaunti ya Mfuko wa Taifa wa Misaada ya Maafa (National Relief Fund) iliopo Benki Kuu ya Tanzania.

"Fedha hizi ni kando ya zile alizokadhibiwa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, zilizochangwa na mashirika ya umma kiasi cha shilingi bilioni mbili.

"Hivyo basi, hadi sasa fedha zote zilizochangwa kupitia mfuko huu ni shilingi 2,138,645,500. Vifaa vya misaada mbalimbali vilivyotolewa ni pamoja na chakula mahindi kilo 47,627, maharage kilo 8,692; unga wa sembe kilo 37,745, unga wa ngano kilo 13,800; mchele kilo 39,330; mafuta ya kupikia lita 12,290 na sukari kilo 12,954.

"Aidha, vifaa vya malazi vilivyotolewa ni magodoro 1,920; mahema ya familia 5; mabegi ya kulalia 600; mashuka 2,559 na maduveti 170.

"Vifaa vingine vilivyotolewa ni ndoo za lita 10 jumla 1,485; ndoo za lita 20 jumla 331; madumu ya lita 10 jumla 240; madumu ya lita 20 jumla 141; mabeseni 720; pamoja na nguo za kike na za kiume, vyombo vya chakula, mataulo ya kike na vifaa vya uokozi kama tochi, majembe, buti za mvua, matoroli na glovu."

Aidha, Msemaji Mkuu huyo amesema Serikali imeshapokea mabati 5,200 ya kuwasaidia waathirika kujenga makazi mapya.

Wakati huo huo, Bw.Matinyi amesema, Serikali inaendelea kuwashukuru na kuwapongeza Watanzania pamoja na taasisi mbalimbali za umma na binafsi ndani ya nchi yetu kwa moyo wa utu na uzalendo.

"Misaada mbalimbali ya vitu na fedha inaendelea kupokelewa na taarifa yake itatolea. Serikali inatoa wito kwa wanaojitolea kufanya hivyo kuleta vifaa vya ujenzi pale inapowezekana ili visaidie waathirika kuanzisha makazi mapya.

"Kamati ya Maafa ya Taifa iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, imetangaza akaunti ya benki ya kuwekea fedha kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022.

"Akaunti hiyo ya kielektronikia inaitwa National Relief Fund - Na. 9921159801. Akaunti hii ina swift code TANZTZTX kwa wanaotuma fedha kutoka nje ya nchi. Miamala inapotumwa inatakiwa kuwa na maelezo MAAFA HANANG. Akaunti hiyo ipo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na inapokea fedha kutoka ndani na nje ya nchi."

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news