Mfumo wa BPS waokoa mabilioni ya fedha uagizaji wa mafuta

NA GODFREY NNKO

MTENDAJI Mkuu wa Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (PBPA), Erasto Mulokozi amesema, Mfumo wa Uagizaji wa Pamoja wa Mafuta nchini (BPS) huwa unaokoa zaidi ya shilingi bilioni 500 kila mwaka.

Wakala wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja (Petroleum Bulk Procurement Agency (PBPA) ulianzishwa mwaka 2015 kwa Amri ya Serikali (Establishment Order,2015) chini ya Mwongozo wa Sheria ya Wakala wa Serikali (The Executive Agencies Act, (Cap.245) kwa lengo la kuratibu na kusimamia Mfumo wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja.

Sambamba na kuhakikisha ununuzi wa mafuta unafanyika kwa ufanisi ili kupata manufaa ya kiuchumi na upatikanaji wa mafuta nchini wakati wote.
"Kwa hiyo kwa wastani zaidi ya dola za Marekani milioni 200 sawa na shilingi bilioni 500 huokolewa kila mwaka kupitia mfumo wa BPS;

Bw.Mulokozi ameyabainisha hayo leo Desemba 11,2023 jijini Dar es Salaam katika kikao kazi na wahariri wa vyombo vya habari nchini chini ya uratibu wa Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Vile vile amesema, Mfumo wa Uagizaji wa Mafuta kwa Pamoja umeleta manufaa mengi ikiwemo uhakika wa upatikanaji wa mafuta yanayotosheleza mahitaji ya nchi na yenye viwango vya ubora unaotakiwa wakati wote.
Afisa Habari na Mawasiliano kutoka Ofisi ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri akiongoza kikao hicho.

Sambamba na kupata unafuu wa gharama za uletaji wa mafuta (premium) kutokana na uagizaji wa pamoja.

Manufaa mengine, Mulokozi amesema ni kupungua kwa bei ya mafuta kutokana na uagizaji wenye ufanisi ikiwemo kuongezeka kwa mapato ya kikodi yatokanayo na bidhaa ya mafuta.
"Pia, mfumo umewezesha kupunguza vitendo vya ukwepaji kodi kutokana na udanganyifu uliokuwa unafanywa na baadhi ya waagizaji wa mafuta.”

Mulokozi pia amesema, mfumo umewezesha kudhibiti udanganyifu katika gharama za mafuta katika soko la Dunia na gharama za uletaji wa mafuta nchini.

Aidha, mfumo umewezesha kupunguza msongamano wa meli bandarini.

Katika hili, Mulokozi amesema wastani wa Dola za Marekeni milioni 170 sawa na shilingi bilioni 425 huokolewa kila mwaka ikilinganishwa na gharama za demurrage zilizokuwa zikilipwa kabla ya mfumo wa BPS.
Mtendaji Mkuu huyo ameomngeza kuwa, pia mfumo unatumika na nchi jirani katika ununuzi wa mafuta kwa nchi hizo.

“Hivyo kuipatia Serikali mapato kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya bandari. Kwa sasa uagizaji wa mafuta kwa ajili ya nchi jirani umefikia wastani wa asilimia 55 ya kiwango cha mafuta kinachoagizwa kupitia BPS kutoka wastani wa asilimia 33 za awali.”

Jambo lingine amesema ni kupungua kwa upotevu wa mafuta wakati kwa kupakua mafuta kutoka melini ambapo wastani wa tani 1,100 sawa na lita 1,300,000 huokolewa kila mwezi (sawa na takribani shilingi bilioni 4.16 kwa bei kikomo za Desemba 2023”.
Mulokozi amefafanua kuwa,kwa mwaka takribani shilingi bilioni 49.9 huokolewa kupitia mfumo huo.

Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF),Yasin Sadick ameipongeza mamlaka hiyo kwa kazi nzuri inayofanya kwa maslahi makubwa ya Taifa.

"Wengi wetu tulidhani PBPA ni kikundi cha Waarabu ambacho kimejikusanya na kuagiza mafuta hivyo kuiuzia Serikali, kumbe ni taasisi ya Serikali, hongereni sana kwa kazi nzuri."
Aidha, ametoa wito kwa mamlaka hiyo kuendelea kushirikiana na vyombo vya habari na wanahabari ili waweze kutoa taarifa za mara kwa mara kuhusu majukumu yanayofanywa na mamlaka hiyo nchini

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news