Mheshimiwa Dkt.Selemani Jafo aitwa Kijiji cha Mzenga B, waingia mtaani na mabango

PWANI-Wanakijiji wa Kijiji cha Mzenga B kilichopo Kata ya Vihigo wilayani Kisarawe wamemuomba Mbunge wao, Mheshimiwa Dkt.Selemani Jafo ambaye ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kufika kijijini hapo ili aweze kuwapa ufumbuzi kuhusu fidia ya ardhi yao.

Wanakijiji wa Mzenga na Kikongo Kata ya Vihingo, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani wanatarajia kulipwa fidia ili kupisha maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Maneromango-Mzenga-Mlandizi-Makofia (Km 100) .
Wito huo umetolewa na wanakijiji hao ambao wamewakilishwa na Bi.Tatu Mohamed mkazi wa Kijiji cha Mzenga B katika Kata ya Vihingo wilayani Kisarawe akisema,

“Mheshimiwa Jafo, Mbunge wetu popote ulipo tunakuomba sisi wakazi wa Nzenga B uje utuone tulivyonyanyasika kuhusu TANROADS.

“Maeneo yetu wameyachukua, lakini hatujaridhika na tathmini. Kwa hiyo chonde chonde baba, Mheshimiwa Jafo sisi ni wapiga kura wako, isitoshe mimi ni Mjumbe wako wa Mkutano Mkuu Wilaya.

“Kwa hiyo tunakuomba chonde chonde uje utusaidie utuone, wananchi wako wa Mzenga B, heka moja tumelipwa malipo ya laki saba kwa heka moja.

“Kwa hiyo tunaomba uje, wakati huu heka huku sasa hivi inauzwa takribani milioni tano na kuendelea mbele, inategemea na eneo lilipo, lakini sisi huku wote tuko barabarani.

“Na barabarani kwa hela hiyo ya laki saba haupati, kwa hiyo chonde baba tunakuomba sisi wapiga kura wako Mzenga B Kata ya Vihingo Wilaya ya Kisarawe, halafu mzaliwa mwenzetu wewe tunakutambua vizuri sana mwenzetu. Kata ya Vihingo wote wa umoja…
Akifafanua kuhusu haki ya fidia katika ardhi,Wakili Manace Ndoroma anabainisha kuwa, ardhi ni mali. “Hivyo, mali ni kitu au bidhaa yoyote yenye thamani. Kiwango cha thamani ya mali kinaweza kutofautiana kutoka mtu mmoja hadi mwingine, ama kutoka eneo moja kwenda eneo lingine.

“Kwa mfano, thamani ya ardhi katika Jiji la Dar es Salaam ni kubwa kuliko ile ya Mji wa Ngara. Aidha, uhitaji wa bidhaa ama kitu kinachonunuliwa pia unachangia katika kupunguza ama kuongeza thamani ya bidhaa hiyo.

“Mali inaweza kutumiwa kwa namna nyingi. Mojawapo ya namna hizo ni kutumia mali kupata mali yaani, mtu anaweza kubadilisha mali ili kupata mali.

“Kwa mfano, mtu anaweza kuuza mali yake ili apate pesa, ama anaweza kubadilishana mali moja na mali nyingine kwa thamani ambayo pande mbili zimekubaliana.

“Zamani, kabla ya pesa kuja, biashara zilikuwa zinafanyika kwa kubadilishana mali na mali. Katika kutambua umuhimu wa umiliki wa mali katika kulinda utengamano na ustawi wa jamii.

“Katiba na sheria za Tanzania zimeweka utaratibu ambao unahakikisha kwamba mtu akishapata mali yoyote kihalali basi mali hiyo inaendelea kutumika kwa faida yake na watu wengine ambao yeye mwenyewe atapenda waifaidi ama akiwa hai au hata akishakufa.

“Ibara ya 24 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inaeleza kwamba kila mtu anayo haki ya kumiliki mali na kwamba, mtu huyo anayo pia haki ya kulindiwa mali yake kwa mujibu wa Sheria.

“Sehemu ya pili ya Ibara hiyo inaeleza kwamba pale ambapo mali ya mtu inalazimika kutwaliwa na Serikali kwa matumizi yenye maslahi kwa umma, sharti mmiliki wa mali hiyo alipwe fidia stahiki.

“Tujikite katika mfano wa ardhi kama mojawapo ya mali zinazotambuliwa na kulindwa kwa mujibu wa Sheria. Kimsingi, ardhi katika nchi ya Tanzania ni mali inayomilikiwa kwa pamoja na watanzania wote, huku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiwa ndiye mdhamini na msimamizi mkuu wa maslahi ya wananchi hao katika rasilimali ardhi.

“Hata hivyo, pamoja na umiliki wa pamoja unaotajwa, mtu mmoja mmoja anayo haki ya kumiliki na kuendeleza kipande cha ardhi ama kwa njia ya umiliki wa kimila, au umiliki wa kupewa, unaoambatana na hati maalum.

“Umiliki wa kimila hurithiwa kutoka kizazi kimoja hadi kingine na hauna kikomo. Umiliki wa kupewa hutolewa kwa vipindi maalum.

“Kipindi kirefu kuliko vyote ni miaka 99. Pale ambapo ardhi inayotumiwa na mtu mmoja inapaswa kutwaliwa kwa ajili ya matumizi yenye maslahi ya watu wengi, Ibara ya 24 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, na kifungu cha (3) cha Sheria ya Ardhi hutumika.

“Maelezo ya kifungu hicho kuhusu suala la fidia ni sawa na yale yaliyomo katika kifungu cha (3) cha Sheria ya Ardhi ya Vijiji. Kwa ujumla, Ibara hiyo ya Katiba, ikisomwa kwa pamoja na kifungu cha (3) cha Sheria ya Ardhi, ama kifungu cha (3) cha Sheria ya ardhi ya Vijiji (kulingana na ilipo ardhi husika), inaelekeza kwamba pale ambapo ardhi ya mtu lazima itwaliwe basi mtu huyu atastahili kulipwa fidia ambayo ni kamilifu (full), ya haraka (prompt) na ya haki (fair).

“Haki katika fidia ya ardhi inapaswa ionekane ikitendeka kwa wote; yaani mlipaji na mlipwaji wa fidia, na inapatikana kwa kufanya uthamini wa mali husika kabla fidia haijalipwa.

“Fidia ya ardhi inazingatia ardhi yenyewe na maendelezo yaliyofanyika juu yake. Kwa mfano, iwapo kwenye ardhi hiyo kumejengwa nyumba, au kumepandwa mazao basi tathmini hufanyika kwa kuzingatia bei halisi ya soko kama ilivyopitishwa na kutangazwa na mamlaka stahiki za serikali.

“Tathimini ikishafanyika malipo sharti yafanyike katika kipindi maalum kilichotajwa, vinginevyo fidia itapaswa kurudiwa upya kwa sababu thamani ya mali husika itakuwa imeongezeka.

“Hiyo ndiyo maana ya fidia kulipwa haraka (prompt). Aidha, fidia haipaswi kulipwa kwa mafungu. Fidia sharti ilipwe kikamilifu (full).

“Yapo mazingira ambapo kama suala linahusisha ardhi fidia inayolipwa hujumuisha pia malipo ya usumbufu na pango la mahali mbadala pa kujihifadhi wakati aliyehamishwa akijenga makazi yake mapya.

“Kwa ujumla, fidia haipaswi kumsababishia mhusika ugumu wa maisha ambao hakuwa nao kabla ya kutakiwa kuhamishwa.

“Badala yake, fidia inapaswa ijumuishe kifuta machozi cha kumfanya mtu ambaye ameondoka katika eneo analolimiliki kimila ama kwa kupewa ajisikie faraja na kukiri kwamba kuhamishwa kwake kuna manufaa kwake yeye mwenyewe na wananchi wenzake,”amefafanua Wakili Ndoroma.

Uthamini ni nini?


Uthamini ni utaratibu wa utaalam wa kukadiria na kushauri kuhusu thamani ya mali isiyohamishika (kama vile ardhi,majengo na mazao). Hivyo neno uthamini linatokana na neno thamani


2.Thamani ni nini?


Thamani kwa ujumla wake inaweza kuelezeka kama bei inayolipwa kwa ajili ya kupata kitu. Lakini kwa lugha ya kitaaluma: thamani hususan ya mali isiyohamishika kwa mfano ardhi, inahusisha;-

  • Upatikanaji wake(availability)
  • Ubora wa matumizi yake(utility)
  • Mahali ilipo(location)
  • Umiliki wake(ownership)


3.Je, Ardhi ina thamani?


Ndiyo, kwa sababu ardhi ni rasilimali ya msingi ambayo shughuli zote za kijamiii, kiuchumi na kimaendeleo zinafanyika juu yake. Kwa Tanzania, asilimia takriban themanini (80) ya wananchi wa vijijini hutegemea ardhi kwa maisha yao ya kila siku kwa chakula, kipato na mahitaji mengine.


  • Ardhi ni rasilimnali adimu ambayo hushindaniwa na watu au shughuli mbalimbali na hivyo kuifanya iwe na thamani kubwa

· Ardhi humilikiwa kiserikali na kimila kwa sheria, kanuni na taratibu zinazokubalika. Ni kutokana na thamani ya ardhi watu hulazimika kumiliki ardhi na kuishi ndani yake.


4.Nini umuhimu wa uthamini?


Kuongezeka kwa ushindani wa mahitaji ya ardhi inayomilikiwa kiserikali, ikilinganishwa na ardhi iliyopo kumejenga umuhimu wa kusimamia na kutawala mali hiyo adimu kwa umakini mkubwa. Hivyo, uthamini ni nguzo mojawapo ya utawala na usimamizi bora wa ardhi kwa kuwezesha maamuzi ya maendeleo bora ya ardhi kufanyika.


5. Nini sababu ya uthamini?

Uthamini unaweza kutakiwa kwa madhumuni mbalimbali kama vile:

  • Ushauri wa maamuzi ya uuzaji na ununuzi
  • Kupandisha/kushauri bei ya pango
  • Rehani/mikopo
  • Bima
  • Ukadiriaji wa misingi ya utozaji kodi, ushuru na ada mbalimbali za kiserikali na uchumi
  • Sababu za kiuhasibu na mizani
  • Ukadiriaji fidia kutokana na utwaaji ardhi


6.Uthamini kwa madhumuni ya fidia:

Dhana ya fidia:


Kwa kuwa ardhi ya Tanzania ni mali ya wananchi wote, Rais ndiye mwenye dhamana ya kulinda kwa manufaa ya wote. Hata hivyo mwananchi anaruhusiwa kuitumia na pale ambapo inahitajika kutwaliwa kwa ajili ya sababu nyingine hasa za maendeleo ya taifa, basi mmiliki wa ardhi hiyo anastahili kulipwa fidia.


7. Nini misingi ya uthamini wa fidia?

  • Uthamini na ulipwaji wa fidia hufanyika kulingana na misingi ya taaluma na kwa kuzingatia Sheria ya Ardhi Na.4 ya mwaka 1999(kifungu namba 3(I)(g) na kanuni zake husika).
  • Misingi ya uthamini wa fidia inatawaliwa na agizo la sheria ya uthamini wa haki, kamilifu na kulipwa kwa wakati muafaka (fair, full and prompt compensation)
  • kulingana na kifungu cha 3 cha Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 na kanuni (taarifa ya Serikali Na.78 ya 2001) za fidia inapaswa ijumuishe yafuatayo pale panapohusika

· Thamani ya ardhi na mali isiyohamishika (unexhausted improvements)

  • Posho ya usumbufu (distabance allowance)
  • Posho ya usafiri (transport allowance)
  • Posho ya upotevu wa makazi (lost of accomodation)
  • Posho ya upotevu wa faida (loss of profit)
  • Gharama za awali za kupata ardhi
  • Kama fidia imecheleweshwa, ilipwe pamoja na riba kwa kiwango cha soko huria.

8.Taratibu za uthamini wa fidia

Uthamini hutekelezwa katika hatua kuu nne:

(a) Maandalizi ya awali (pre-site inspection):

  • Mthamini atatembelea eneo husika, ili kubaini ukubwa wa kazi na wahusika
  • Maandalizi ya vitendea kazi na viwango vya thamani.

b) Ukaguzi wa mali

  • Kumtambua mwenye mali na kumuorodhesha katika fomu ya ukaguzi
  • Kutoa namba ya kumbukumbu kwa mwenye mali
  • Mwenye shamba kuonyesha mipaka ya shamba au mali yake.
  • Kuchukua taarifa ya ukubwa wa eneo husika kwa kutumia GPS au ramani ya picha za anga

· Kuhesabu mazao ili kubaini idadi na kiwango cha ukuaji wa mazao ya aina mbalimbali

  • Kukagua majengo na kuchukua taarifa zote husika ikiwa ni pamoja na vipimo.
  • Kujaza taarifa ya majengo au idadi ya mazao kwenye fomu ya ukaguzi
  • Kumpiga picha mfidiwa mbele ya mali yake akiwa ameshika bango lenye namba ya kumbukumbu iliyotolewa
  • Kuhakikisha fomu ya ukaguzi imesainiwa na mwenye mali, Mthamini husika na Kiongozi wa Serikali ya Mtaa ambaye atathibitisha uhalali wa mfidiwa

) Ukokotoaji wa thamani

  • Taarifa huhamishwa kutoka fomu ya ukaguzi na kuingiza kwenye fomu ya ukokotoaji thamani
  • Ukokotoaji wa mahesabu ya thamani hutumia viwango vilivyotolewa na Ofisi ya Mthamini Mkuu ili kupata thamani ya mali husika
  • Kuwasilisha fomu zote kwa Mthamini kwa ajili ya kuthibishwa

d) Utayarishaji wa Hati za Fidia (Compensation Schedules)

Baada ya kumalizika uthamini na kuandaa taarifa,majedwali ya fidia yanatayarishwa yakionesha;

  • Majina ya walipwaji
  • Mali zitakazolipwa fidia
  • Thamani ya fidia kwa kila mali
  • Kisha jumla ya fidia itasainiwa na

1. Mthamini Mkuu

2. Afisa Ardhi anayeshughulika na zoezi hilo

3. Katibu Kata wa Kata husika

4. Mkuu wa Wilaya husika

5. Mkuu wa Mkoa

Ulipaji wa Fidia

Husimamiwa na Katibu Mtendaji kwa kuwatambulisha walipwaji fidia.

9.TARATIBU ZA UTHAMINI KWA UJUMLA ;

Kwa mwananchi anayehitaji huduma ya uthamini kuna taratibu za utendaji zinazohusisha:-

  • Maombi ya uthamini kwa maandishi yakiambatanishwa na kivuli cha hati au barua ya toleo

· Ili kumwezesha Mthamini aifanye kazi yake kwa ufanisi mkubwa, ushirikiano kati ya mteja na Mthamini unahitajika sana. Mteja anapaswa kuwa mwaminifu kwa kujibu maswali mbalimbali atakayoulizwa na Mthamini.

  • Mthamini hutakiwa kufanya ukaguzi wa mali (Physical site inspection)
  • Kisha ukokotoaji wa thamani hufanyika kwa kuzingatia viwango na kanuni za kitaalamu na za kisheria na hatimaye taarifa ya uthamini huandaliwa
  • Mteja hutakiwa kulipia ada ya uthamini kabla ya taarifa ya uthamini kuthibitishwa
  • Mwisho, taarifa ya uthamini huthibitishwa na Mthamini Mkuu na kisha kukabidhiwa kwa mwombaji.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news