ZANZIBAR-Makamu wa Pili wa Rais mstaafu, Mhe. Balozi Seif Ali Iddi amewataka Wananchi kutumia vyakula na dawa zenye kiwango ili kuzilinda afya zao
Akifunguwa jengo jipya la Maabara ya Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA) huko Mombasa Wilaya ya Magharibi 'B'.ikiwa ni miongoni mwa Shamra Shamra za Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema, utumiaji wa dawa na vyakula ambavyo viko chini ya viwango vitasababisha madhara ya kiafya Kwa mtumiaji na kuipatia mzigo Serikali ya kuhudumia matibabu.
Aidha,amewataka wafanyakazi wa Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi kuvitunza vifaa vya maabara walivyowekewa pamoja na kutoa huduma kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.
Vile vile amewataka wafanyakazi hao kudumisha nidhamu na mashirikiano katika utendaji wa kazi zao ili kufanyakazi Kwa ufanisi pamoja na kutoa haki bila ya kumuonea mfanyabiashara yeyote
Waziri wa Afya, Nassour Ahmed Mazrui amesema,hiyo ni maabara ya aina yake ya kuchunguza madawa na vyakula vyote viwe na viwango vya kimataifa ili wawekezaji kupata fursa ya kuekeza na kunua bidhaa hizo.
"Wawekezaji wanaokuja kuwekeza katika vyakula na viwanda wakiona kuna maabara ya kupimia bidhaa zao na yenye hadhi kubwa ya kimataifa watawekeza,"alisema Mhe.Mazrui.
Naye Mkurugenzi Mtendaji Wakala wa Chakula Dawa na Vipodozi Zanzibar (ZFDA), Burhan Othman amesema, kukamilika kwa maabara hiyo kutasaidia kuongeza nyanja za uchunguzi wa bidhaa mbalimbali pamoja na kurahisisha mzunguko kwa wafanyabiashara.
Amesema, jengo la maabara ya ZFDA ni la Kwanza kwa hapa Zanzibar lenye ghorofa tatu na lenye vigezo vya kimataifa ambayo imejengwa kupitia pesa za mradi wa maendeleo ambazo zimetolewa kwa awamu mbili tofauti awamu ya kwanza shilingi bilioni 5.4 kwa ajili ya jengo na shilingi bilioni 4.4 kwa ajili ya vifaa.