ZANZIBAR-Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba, Sheria, Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Haroun Ali Suleiman amesema, Serikali imehakikisha inawapatia huduma bora wananchi wake kwa kuzingatia sera, sheria, kanuni na miongozo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Amesema hayo alipokuwa akizungumza n waandishi wa habari kuelezea maendeleo na mafanikio ya wizara ikiwa ni miongoni mwa shamrashamra za Maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Amesema,Serikali imeimarisha mbinu za utendaji kazi ili kutoa huduma kwa haraka na zilizo bora kwa jamii kwa kuzingatia utawala wa sheria na haki za binadamu.
Aidha,alifafanua kuwa, sekta ya sheria imepewa jukumu la kusimamia masuala ya kisheria ili kuhakikisha Zanzibar inazingatia utawala wa sheria na haki za binadamu.
Vilevile itasimamia utoaji wa haki na utungwaji wa sheria na kufanya mapitio ya sheria mbalimbali ili ziweze kukabiliana na mabadiliko ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Ameeleza kuwa, Serikali imechukuwa juhudi kubwa katika kuanzisha mfumo wa kielektroniki kwa ajili ya utoaji huduma ikiwemo ya mishahara, manunuzi,ajira, ukaguzi,uwekaji wa taarifa za watumishi na malipo yao pamoja Mfumo wa Ofisi Mtandao.
Waziri Haroun amesema, Wizara ya Utumishi imekuwa na mikakati endelevu ya kuwajengea mazingira mazuri watumishi wa umma pamoja na kuimarisha maslahi na marupurupu ili kuweza kufanya kazi zao kwa ufanisi.
Alibainisha kuwa, Serikali imeimarisha muhimili wa Mahakama kwa kuongeza idadi ya Majaji, Mahakimu na watendaji mbalimbali kwa kurahisisha na kuharakisha uendeshaji wa kesi na utoaji kwa haki kwa wananchi.
Mkutano huo wa waandishi wa habari ni muendelezo wa utoaji wa taarifa za maendeleo na mafanikio ya wizara mbalimbali ikiwa ni miongoni mwa Maadhimisho ya Miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.