MPC yaridhishwa na ukuaji wa uchumi 2023, yasema 2024 matokeo yatakuwa chanya zaidi

NA GODFREY NNKO

KAMATI ya Sera ya Fedha (MPC) imebainisha kuwa, mwenendo wa ukuaji wa uchumi nchini 2023 unaridhisha na matokeo chanya yanatarajiwa zaidi 2023.
Hayo yamebainishwa kupitia taarifa iliyotolewa na Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye ni Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Emmanuel Tutuba leo Desemba 19,2023.

Amesema, hayo yalibainika baada ya kamati hiyo kufanya kikao chake cha 229 tarehe 18 Desemba 2023, kutathmini utekelezaji wa sera ya fedha na mwenendo wa uchumi.

Katika tathmini yake, kamati ilibaini kuwa utekelezajiwa sera ya fedha,umechangia kuhakikisha mfumuko wa bei unabaki ndani ya lengo la asilimia 5, kuongeza uzalishaji katika shughulimbalimbaliza kiuchumi pamoja na kudumisha uthabiti wa sekta ya fedha.

Utekelezaji huu,ukichagiwa na Sera thabiti ya bajeti na ongezeko la mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa nje ya nchi pamoja na shughuli za utalii umesaidia kupunguza uhabawa fedha za kigeni nchini kwa mwezi Oktoba na Novemba 2023.

Kamati pia ilitathmini mwenendo wa uchumi wa dunia na kubaini kuwa uchumi wa dunia umeendelea kubaki dhaifu kwa kipindi cha mwaka 2023, kutokana na migogoro ya kisiasa,kubanwa kwa sera ya fedha katika nchi nyingi duniani na ongezeko la bei za nishati.

Hata hivyo,hali hii inatarajiwa kuimarika mwaka 2024 kutegemeana na kupungua kwa bei za nishati na matarajio ya kupungua kwa kubanwa kwa sera ya fedha katika nchi zilizoendelea pamoja na utatuzi wa migogoro ya kisiasa duniani.

"Kamati pia ilifanya tathmini ya kina ya mwenendo wa uchumi wa ndani na kubaini kuwa,licha ya changamoto zinazotokana na mtikisiko wa kiuchumi duniani, mwenendo wa
uchumi wa ndani ulikuwa wa kuridhisha mwaka 2023.

"Na unatarajiwa kuimarika zaidi mwaka 2024, kutokana na utekelezaji wa sera zenye lengo la kuchochea uzalishaji nchini pamoja na ongezeko la uwekezaji wa sekta binafsi,"amefafanua Mwenyekiti wa MPC,Gavana Tutuba.

Amebainisha kuwa, Pato la Taifa kwa Tanzania Bara lilikua kwa asilimia 5.4 na asilimia 5.2 kwa robo ya kwanza na ya pili ya 2023, mtawalia.

Kutokana na ukuaji huu pamoja na tathmini ya viashiria vya awali vya kiuchumi kwa nusu ya pili ya mwaka 2023, ukuaji uchumi unatarajiwa kuwa juu ya makadirio ya asilimia 5 kwa mwaka 2023.

"Uchumi wa Zanzibar pia uliendelea kuimarika kutokana na kuongezeka kwa shughuli za utalii na uwekezaji wa sekta binafsi."

Kutokana na hayo, ukuaji wa pato la taifa kwa Zanzibar ulikuwa kwa asilimia 5 katika robo ya pili ya mwaka 2023 na unatarajiwa kufikia asilimia 7.1 kwa mwaka 2023.

Vile vile amesema, mfumuko wa bei kwa Tanzania Bara umeendelea kubaki chini ya lengo la asilimia 5,kufuatia utekelezaji wa sera madhubuti za fedha, bajeti na za kimfumo.

"Mfumuko wa bei ulipungua kufikia asilimia 3.2 kwa mwezi Novemba na Oktoba 2023 ukilinganisha na asilimia 3.3 iliyorekodiwa kwa kipindi cha miezi mitatu mfululizo hadi Septemba 2023 kutokana na kupungua kwa bei za chakula nchini."

Kwa upande wa Zanzibar, mfumuko wa bei uliendelea kupungua kufikia asilimia 6.5 mwezi Oktoba 2023, kutoka asilimia 7.5 mwezi Septemba 2023 kutokana na kushuka kwa bei za chakula na bidhaa zisizo chakula.

Amesema, mfumuko wa bei unatarajiwa kubakia chini ya lengo la muda wa kati la asilimia 5 kwa Tanzania Bara na Zanzibar.

Kufuatia utekelezaji thabiti wa sera ya fedha inayolenga kupunguza ongezeko la ukwasi
katika uchumi,Gavana Tutuba amesema ukuaji wa ujazi wa fedha ulipungua mwezi Novemba 2023.

"Ukuaji wa ujazi wa fedha kwa tafsiri pana zaidi (M3) ulikua kwa asilimia 13.8 mwezi Novemba 2023,ukilinganisha na asilimia 14.5 kwa mwezi Septemba 2023.

"Kasi ya ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ilipungua kufikia asilimia 18.3 mwezi Novemba 2023 ukilinganisha na asilimia 19.5 mwezi Septemba 2023."

Hata hivyo, ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ulikuwa juu ya makadirio ya ukuaji wa asilimia 16.4 kwa kipindi kinachoishia Desemba 2023.

Aidha,kuongezeka kwa hamasa ya uwekezaji sambamba na uboreshaji wa mazingira ya ufanyaji biashara nchini zinategemea kuendelea kuchochea ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi.

"Ukusanyaji wa mapato ya Serikali ulikuwa wa kuridhisha, ambapo katika miezi minne ya kwanza ya mwaka 2023/24, makusanyo yalifikia asilimia 96 ya lengo kwa Tanzania Bara, huku matumizi yakiendelea kuendana na mapato.

"Kwa upande wa Zanzibar, ukusanyaji wa mapato ulishabihiana na malengo yaliyowekwa,"amefafanua Mwenyekiti huyo wa MPC.

Pia,Gavana Tutuba amesema,nakisi ya urari wa biashara, huduma na uhamisho mali nje ya nchi, iliimarika kidogo kutokana na ongezeko la mapato yatokanayo na mauzo ya bidhaa nje ya nchi pamoja na shughuli za utalii.

Kufuatia hali hii, nakisi ya urari wa biashara na uhamisho mali nje ya nchi ilifikia dola milioni 3,265.5 mwezi Oktoba 2023, kutoka dola milioni 4,990.1 kwa mwaka unaoishia Oktoba 2022.

"Kwa upande wa Zanzibar, nakisi ya urari wa biashara,huduma na uhamisho mali nje ya nchi iliongezeka kufikia dola milioni 477.7 kutoka dola milioni 362.8, kutokana na kupanda kwa gharama za uagizaji wa bidhaa na huduma kutoka nje,"amesema Gavana Tutuba.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news