Mradi wa Samia Housing Scheme Kawe sasa ni gumzo, Mbunge asema NHC waikumbuke Vingunguti, Buguruni, Kigogo…

NA GODFREY NNKO

MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Janeth Massaburi ameliomba Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na wadau wengine wa ujenzi kuja na mkakati wa kujenga majengo ya kisasa kama ya Mradi wa Samia Housing Scheme ili kuondoa mabanda mabanda yanayoshusha hadhi ya Jiji.
Ameyasema hayo leo Desemba 14, 2023 baada ya kufanya ziara katika Mradi wa Samia Housing Scheme ambao unatekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) eneo la Tanganyika Packers lililopo Kata ya Kawe jijini Dar es Salaam.

Ziara hiyo ambayo ameambatana na Kamati ya Siasa Wilaya ya Kinondoni ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yao ya kukagua Ilani ya Uchaguzi 2020 hadi 2025, Mheshimiwa Massaburi amesema,kuwa na makazi bora kunaepusha majanga mengi.

“Maana yake kuna faida na athari kuhusu makazi, unapopata makazi mazuri unaponguza majanga. Unapokaa kwenye makazi ambayo si salama kuna majanga.

“Tunajua, ukiwa katika makazi bora mtu unakuwa na uwezo wa kutulia na hata kufikiri, unakuwa katika hali ya utulivu na kufikiria masuala mazuri, na ndiyo maana unakuta wafanyakazi wanahimizwa kuwa na makazi bora ili wawe watendaji wazuri.

“Ukiwa haujui mahali pa kukaa au hapana uhakika, hauwezi kufanya kazi kwa ufanisi…nyumbani kwako kunafikika kirahisi, lakini kuna mgonjwa, ukiwa na mgonjwa nyumbani kwako gari la wagonjwa litafika kirahisi na kutoka.

“Kukiwa na moto, zimamoto gari itafika kirahisi na kutoka, kukiwa hata na uhalifu pia patafikika na kutoka.
"Lakini,na ninyi kwa ninyi mtaweza kuangaliana kwa maana ya kulindana wenyewe kwa kujua nyumba ile kuna nani, nyumba ile ana tabia gani.

“Lakini, athari za kukosa makazi hasa hizi squaters unakuta mlango wa huyu huko huko, choo cha huyu kiko huku, mwingine hivyo hivyo huo ndiyo mwingiliano wa pale na unakuta uhalifu ni mkubwa.

“Ikitokea nyumba kuungua, magari hayafiki, ikitokea mwizi amefika pale ameingia uchochoro huu haujui ametokea wapi.

“Mgonjwa, kuna watu wanajifungulia njiani kwa kukosa hata hizo njia za kupita kutokana na makazi holela.Kwa hiyo nyumba bora ni msingi wa maisha na maendeleo katika jamii tunayoishi.

“Kwa hiyo nichukue fursa hii, niliombe shirika (NHC) liendeleze ujenzi na ubunifu zaidi ili Mkoa wa Dar es Salaam uondokane na yale mabanda mabanda ukiwa kwenye ndege pale unashuka unakutana na mabanda mabanda Mkoa wa Dar es Salaam ni mabanda mabanda tofauti na ukienda hata Dodoma.

“Ukiwa angani Dar es Salaam asilimia kubwa ni nyumba ambazo si rasmi, kwa hiyo taasisi kama National Housing na zingine zichukue hatua ya kutafuta uwezekano na kubuni, kujenga makazi kwa kuendeleza Buguruni kule, Vingunguti kule,Kigogo, Manzese, kutengeneza pale.
“Unaboresha unajenga maghorofa kama haya ili watu waweze kujikusanya kukaa katika eneo dogo na eneo kubwa linakuwa wazi, mambo mengine yanaweza kuendelea.

“Maana yake tumebanana pale kwa sababu ya vibanda vibanda vidogo kama mtajenga maghorofa kama haya katika maeneo hayo niliyoyataja ambayo yataweza kuwasaidia watu wa hali ya chini kwa kuweza kuwapa mikopo ya muda mrefu.

“Maana yake mnaweza kujenga mkawapa mikopo ya muda mrefu.Kama huko nyuma iliwahi kutokea wakati wa Mwalimu Nyerere kulikuwa kuna nyumba za bei rahisi za miaka mingi tu.

“Za elfu saba saba za Magomeni, lakini waliboresha maisha ya watu.Baada ya Uhuru, Mwalimu alibuni hiyo ya kuboresha maisha ya wakazi wa Dar es Salaam.

“Sasa tunaomba hizi zama za Awamu ya Sita za Mama Samia kupitia watendaji wake taasisi za ujenzi wa nyumba basi waangalie maeneo hayo ili kuboresha na kubadilisha Jiji la Dar es Salaam liwe na nyumba bora.

“Nyumba za kisasa, ndiyo liitwe haswa Jiji la Kibiashara, liendane na jina.Jina la Dar es Salaam, ndiyo jiji la kibiashara lakini nyumba nyingi ni makazi ambayo si bora sana kwa hiyo tunaomba hilo NHF mlipokee.

“Lakini, ninaamini pia kupitia vyombo vya habari na taasisi zingine zitanisikia waboreshe mfano hapo Jangwani watu wanatolewa, wakitolewa inawekwa nyumba wanarudi tena hii hapana.Lazima kila mahali pawepo utaratibu,”amefafanua Mheshimiwa Massaburi.

Wakati huo huo, Mbunge Massaburi amelipongeza shirika hilo kwa kuendelea kutekeleza miradi ya nyumba ambayo ina manufaa makubwa kwa Watanzania na Taifa.

“Tunapeleka pongezi kwa Mkurugenzi Mkuu na timu yake yote, tunawapenda sana NHC na tunawaombea muendelee kuendeleza nyumba zetu.

“Nirudie kumshukuru sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake anazozifanya katika kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inaenda kutatua matatizo ya Watanzania na kuongeza kwa Watanzania pia.

“Lakini, Mheshimiwa Rais wetu amefanya jitihada nyingi sana kupitia National Housing juzi tulikuwa kwenye mradi wa machinjio Vingunguti.

“Yale machinjio ni ya kisasa, ni ya Kimataifa na baada ya kufanya ile ziara watu wengi walinipigia simu wakasema, walikuwa hawajui kama kuna kitu kama kile.
“Kwa hiyo kumbe tunatakiwa tuvitangaze vitu vyetu vinavyofanyika ili wananchi wengi waweze kujua na kupitia ziara yetu hii hapa umetuambia haya majengo yote yameshachukuliwa.

“Kwa hiyo na watu wengine kama wanahitaji, waje National Housing kwa sababu bado mnajenga.Kwa hiyo kwa kupitia Rais wetu na utekelezaji wake amefanya kazi kubwa sana ambayo anastahili pongezi, anastahili kupewa nguvu.

“Tumuunge mkono Mheshimiwa Rais,ni kazi nyingi sana amezifanya, nichukue pia fursa hii kumpongeza Mkurugenzi Mkuu wa NHC pamoja na wasaidizi wake.Kazi wanayoifanya ni ya kizalendo sana, tumeona,Mama amekwamua palipokwama, lakini ninyi mnatekeleza kikamilifu,”amefafanua kwa kina Mheshimiwa Janeth Massaburi.

NHC

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Hamad Abdallah, Meneja Habari na Uhusiano wa NHC, Muungano Saguya amesema,mradi huo ni sehemu ya kuendelea kuenzi kazi nzuri ambazo zinafanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.
"Mradi huu tumeuita Samia Housing Scheme ili kuenzi kazi nzuri anayoifanya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa.

“Kama unakumbuka kulikuwa na miradi mingi eneo hili la Kawe ilikuwa imesimama, lakini Mheshimiwa Rais alivyoingia madarakani ameikwamua miradi hii yote iliyokuwa imesimama ukiwemo Mradi wa Morocco Square.

“Mheshimiwa Rais ameifungua miradi hii, kwa kuliruhusu Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kuweza kukopa fedha ambazo ndiyo zilikuwa kikwazo kikubwa, fedha ambazo zinawezesha kumalizia miradi hii.

“Hata mradi ambao upo pembeni wa Kawe 7/11 ambao upo pembeni mkipita mnaona maghorofa yamesimama zaidi ya miaka sita hadi saba, Mheshimiwa Rais ameshafungua.

“Tayari shirika limeshapata fedha na ujenzi unaweza ukaanza wakati wowote mwezi Januari, mwakani na unaenda kukamilika.

“Lakini, mradi huu wa Kawe ambao tunaufanya wa Samia Housing Scheme wenye nyumba 560 kwa ujumla zimeshapata wanunuzi.

“Na tunataka kwenda awamu nyingine kwa ajili ya kuweka nyumba ili kukidhi mahitaji ya Watanzania wanaoomba nyumba hizi.

Bw.Saguya amesema, Mradi wa Samia Housing Scheme utakuwa na nyumba takribani 5,000 ambazo zitajengwa katika maeneo mbalimbali nchini.

“ Kwa hapa Dar es Salaam,tutajenga asilimia 50 ya nyumba hizo,lakini Dodoma tutajenga asilimia 30 ya nyumba hizo.

“Na mikoa mingine itachukua asilimia 20,kwa hiyo ujenzi Dodoma utaanza katika mwaka huu wa fedha pia.

“Mradi huu utakwenda kugharimu fedha za Kitanzania takribani shilingi bilioni 460, kwa hiyo unaweza kuona kwamba ni mradi mkubwa.Ni mradi ambao unakwenda kuleta manufaa makubwa sana kwa Watanzania.

“Kama ulivyosikia tunaenda kutoa ajira kupitia ujenzi wa miradi itakayokuwa inaendelea.Tunaenda kutoa makazi kwa ajili ya Watanzania waweze kupata sehemu za kuishi.

“Kwa ujumla, kama unavyofahamu nyumba ni kitu ambacho kinampa mtu maisha bora.Kama hauna nyumba hauwezi hata kuwaza vizuri,kufanya miradi au mambo ya maendeleo.

“Kwa hiyo ni mradi ambao utakuwa mkubwa sana na uwekezaji wake ni mkubwa sana, utakaofanywa kwa awamu na hapa tupo Kawe nyumba 560 na kwa kuwa zimkaribia kuisha.

“Tukimaliza ujenzi, tunabandika zingine, hii yote tunatekeleza Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).”

Wengine

Kwa nyakati tofauti ujumbe huo umelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kutekeleza miradi jumuishi na shirikishi ambayo imekuwa ikitoa fursa kwa makundi mbalimbali ya Watanzania.

Wamesema, kupitia mradi huo wa Samia Housing Scheme vijana wengi wa Kawe na maeneo mengine nchini wamepata ajira mbalimbali katika ujenzi huo.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Mzimuni katika Kata ya Kawe amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuonesha uhodari katika utekelezaji wa majukumu yake kwa ustawi bora wa Taifa.

…pia ninapenda kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwa Rais bora katika nchi zote za Afrika.

“Na kuendelea kuchapa kazi, kwa sababu kazi zake Watanzania tunaziona, tunamshukuru sana kwa kuendelea kuipa maendeleo nchi yetu ya Tanzania.”

“Aidha, ninawashukuru sana National Housing kwa kuendelea kushirikiana nasi toka walipofika mpaka hapa walipo, wamesaidia, wamewapa vijana wangu ajira, hivyo tutaendelea kushirikiana nao kwa kila hatua, vivyo hivyo katika suala la ulinzi na usalama tunashirikiana nao bega kwa bega.”

Mhandisi

Awali Msimamizi wa Mradi huo wa Samia Housing Sheme uliopo Kawe,Mhandisi Grace Musita amesema kuwa, mradi huo hadi ulipofikia wameweza kutengeneza ajira 750 kwa mafundi mbalimbali.
"Lakini, pia kuna watu wenye taaluma ambao ni wasaidizi wetu, wengine wametoka vyuoni, lakini wote wamenufaika na huu mradi mpaka sasa, kuna mama lishe ambao wanatoa huduma za vyakula humu ndani, kampuni za ulinzi, hao wote wapo nje ya hiyo 750.

“Kwa hiyo utaona jinsi gani uwepo wa mradi huu umetengeneza ajira kwa wananchi mbalimbali wa hapa Dar es Salaam, wa hapa Kawe, lakini na wengine kutoka nje ya hapa.”

Amesema, majengo hayo yatakuwa na uhakika wa maji ya kutosha, nishati ya gesi asilia, umeme na nyinginezo huku wakihakikisha kabla ya kuanza ujenzi vifaa vyote vinapimwa ubora na kila hatua wanafanya ukaguzi kabla ya kuendelea.

“Kipekee tumshukuru Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) pamoja na menejimenti yote ya shirika kwa kutuamini na kuweza kutupa nafasi ya kuweza kusimamia ujenzi wa majengo haya.

“Lakini, pia shukurani za pekee ziende kwa Mheshimiwa Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa sababu fedha za ujenzi wa mradi huu hata kama hazijatoka moja kwa moja kwake, lakini Serikali yake yenyewe imepitisha kuweza kufanyia hii kazi kwenye huu mradi.

“Kwa hiyo, tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais, kupitia fedha hizo ndiyo sisi tupo hapa tunafanya kazi,lakini pia na hao watu 750 ambao nimewataja nao wananufaika kwa namna mbalimbali wengine wanasomesha watoto,”amesema Mhandisi Musita.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news