NA DIRAMAKINI
WAZIRI wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kenya, Mheshimiwa Aden Duale ameunga mkono juhudi zinazoendeshwa na idara tofauti nchini humo kukabili matumizi ya Shisha.
Mheshimiwa Duale amesema, wale wote watakaopatikana wakitumia Shisha wanapaswa kuwajibishwa kwa mujibu taratibu na sheria nchini humo.
Usiku wa Desemba 23,2023 Mamlaka ya Kitaifa ya Kampeni Dhidi ya Matumizi Mabaya ya Pombe na Dawa za Kulevya nchini Kenya (NACADA) chini ya Afisa Mtendaji Mkuu, Anthony Omerikwa iliendesha operesheni kali dhidi ya vituo vya burudani ambako kileo hicho kimekuwa kikitumika.
Operesheni hiyo ilifanyika katika eneo la Kilimani jijini Nairobi, ambako watu 25 walikamatwa, huku misokoto kadhaa ya bidhaa hiyo pia ikinaswa.
Aidha,kutokana na operesheni hiyo,Waziri Duale alisema kuwa uvutaji wa Shisha ulipigwa marufuku nchini mnamo 2017, hivyo yeyote anayepatikana akiitumia ama akiiuza anafaa kukabiliwa kisheria.
“Waraibu wa Shisha lazima wakabiliwe kisheria, kwani ilipigwa marufuku nchini tangu 2017. Maafisa wa usalama lazima wavamie vituo vyote vya matumizi au uuzaji wa vileo hivyo,”alisema Waziri huyo.
Kupitia marufuku ya 2017 nchini Kenya shisha, ikijumuisha matumizi, kuagiza, kutengeneza, kuuza, utangazaji,usambazaji na kuhimiza au kuwezesha matumizi yake ni kosa kisheria.
"Ninachotaka kuuliza na kuwaambia wamiliki na waendeshaji wa hizi klabu ni kwamba sheria iko wazi sana.
"Tunajua kilicho halali ni kipi na kipi haramu. Mnamo 2017 Serikali ilitekeleza marufuku ya shisha na uuzaji ukapigwa marufuku,” Omerikwa alisema.
Afisa Mtendaji Mkuu huyo wa NACADA amesema, kutokana na kuenea polepole kwa matumizi na uuzaji wa Shisha katika vilabu vya usiku nchini humo uchunguzi wa hali ya juu utafanywa ili kupunguza mtindo huo.
DAKTARI MLONDO
Daktari Kalegamye Hinyuye Mlondo ameieleza DIRAMAKINI kuwa, watumiaji wa shisha wanapaswa kutambua kuwa ina madhara mengi na hatari kwa afya ya binadamu
Shisha ni nini?
Dkt.Mlondo anasema, shisha ni tumbaku iliyochanganywa na ladha za harufu ya kuvutia kama matunda aina mbalimbali ikiwemo vannila au chocolate.
"Shisha inapatikana sana maeneo ya starehe nje na ndani ya nchi na imejizolea umaarufu mkubwa sana hasa kwa vijana, bahati mbaya kuna vijana wengi hutumia shisha, lakini hawavuti sigara huku wakidhani shisha ni kitu kingine kabisa tofauti na sigara.
"Lakini leo napenda kuwaambia shisha ni zaidi ya sigara na madhara yake ni makubwa zaidi ya yale ya sigara.
"Hivi karibuni Serikali ya Tanzania imepiga marufuku matumizi ya shisha, lakini ikapingwa na vijana wengi ambao wengi wao huvuta kwa kuiga na kutaka kuonekana wa kisasa bila kujua madhara yake kiafya, hivyo ni vema wakatambua kuwa, shisha ina madhara mengi,"amesema Dkt.Mlondo.
Dkt.Mlondo anasema, miongoni mwa madhara yatokanayo na shisha ni pamoja na saratani za aina mbalimbali.
"Shisha inavutwa tofauti kidogo na sigara,yaani inavutwa mara nyingi kwa muda mfupi, huvutwa ndani zaidi ya mapafu na kwa kutumika muda mrefu yaani zaidi ya saa moja tofauti na sigara ambayo inavutwa dakika tano na kuisha.
"Lakini pia tofauti na sigara ambayo inasababisha saratani ya mapafu tu mara nyingi shisha inaleta saratani mbalimbali ikiwemo za figo, koo, mapafu, kibofu cha mkojo, ubongo na damu kwa wakati mmoja.
"Shisha ina mchanganyiko wa kemikali nzito ambazo kitaalamu zimethibitika kusababisha saratani, utafiti unaonyesha kuvuta shisha kwa saa moja ni sawasawa na kutumia sigara 100 mpaka 200,"anafafanua Dkt.Mlondo.
Pia Dkt.Mlondo anasema kuwa, shisha huwa inasababisha uraibu au mazoea kwani ina tumbaku kama sigara za kawaida.
"Ina kemikali inayoitwa kitaalamu kama nicotine ambayo mwili ukiizoea basi unaitaka mara kwa mara, ukizoea shisha hutaweza kuacha kirahisi na hata siku ukisafiri sehemu ambayo haipo basi utalazimika kuvuta sigara ili kukidhi haja ya mwili, hivyo mvuta shisha ataishia kuwa mvuta sigara, jambo ambalo ni hatari kiafya,"amebainisha.
Daktari huyo anaendelea kufafanua kuwa, pia matumizi ya shisha huwa yanasababisha kusambaza magonjwa kwani mara nyingi shisha inatumika na watu zaidi ya mmoja, wakati mwingine hata wasiofahamiana.
"Kama ule mpira usipooshwa vizuri, basi magonjwa kama kifua kikuu na pneumonia ya fangasi huweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine.
"Lakini hata ikioshwa vizuri basi kuchangia na mgonjwa wakati huo huo huweza kuleta maambukizi ya bacteria wa madonda ya tumbo kitaalamu kama helocobactor pylori huweza kuambukizwa pia.
"Vile vile uvutaji wa shisha una madhara kwa mtoto aliyepo tumboni, hii ninamaanisha kuwa, mama mjamzito kama ilivyo kwenye uvutaji wa sigara husababisha madhara makubwa kwa mtoto, ikiwemo kuzaa mtoto mwenye uzito mdogo sana au kuzaa mtoto asiye na baadhi ya viungo kama mikono au miguu, kitalaamu tunaita tetatorogenic effect,"anabainisha Dkt.Mlondo.
Mbali na hayo, Dkt.Mlondo anasema, shisha ni hatari kiafya kwani huwa inachangia kwa kiwango kikubwa magonjwa ya kinywa.
Anasema, mkusanyiko wa kemikali ya nicotine kwenye damu na mate mdomoni husababisha magonjwa ya meno na fizi ambayo huharibu sana meno na kumfanya mtu abaki bila meno ya kutosha.
"Lakini pia huwa inasababisha magonjwa ya moyo, kwani shisha huharibu mishipa ya damu na kuifanya iwe membamba sana kupitisha damu, hivyo husababisha shinikizo la damu kupanda na shambulio la moyo kitaalamu kama heart attack.
"Sambamba na kuharibika kwa ubongo, kwani kemikali ya nicotine na compound zingine zinazopatikana kwenye shisha huweza kuzuia damu kufika vizuri kwenye ubongo, hali hii husababisha kiharusi, ugonjwa ambao huanza na dalili za kushindwa kuongea na kupoteza nguvu za nusu ya mwili wa binadamu," amefafanua Mtaalamu huyo wa afya.
Dkt. Mlondo ameendelea kufafanua kuwa, matumizi ya shisha huwa yanamaliza nguvu za kiume, kwani kemikali za kwenye shisha pia huweza kuziba damu ambayo inaenda kwenye sehemu za siri.
"Hii huua nguvu za kiume kabisa kwa watumiaji wanaume, vivyo hivyo, huwa inasababisha ugumba kwani mirija inayopitisha mayai ya mwanamke kitaalamu kama fallopian tubes huzibwa na kemikali ya nicotine na kusababisha mbegu za mwanaume kushindwa kulifikia yai la mwanamke.
"Pia huleta makunyazi ya ngozi, kwani mkusanyiko mkubwa wa kemikali ya nicotine kwenye ngozi, mate, damu na kila aina ya maji ya mwili humfanya mtumiaji aonekane mzee kuliko umri wake halisi kitu ambacho watu wengi hawakipendelei,"anasema Dkt. Mlondo.
Mtaalamu huyo wa afya anabainisha kuwa, yapo madhara mengi ya kiafya lakini, aliyoyabainisha ni baadhi tu ya madhara ambayo yamegundulika mpaka sasa na huenda kuna mengine ambayo watafiti bado hawajayagundua.
"Nichukue nafasi hii kutoa rai kwa vijana na Watanzania kwa ujumla, wasivute shisha kufurahisha marafiki, vivyo hivyo usivute kwa sababu umelewa, usivute kwa sababu unataka kuonekana mjanja na usivute kwa sababu una msongo wa mawazo.
"Ndugu yangu kumbuka kila mvutaji ana kinga ya mwili tofauti na mwenzake na kila mtu ataingia kwenye jeneza lake mwenyewe, lakini pia taifa haliko tayari kupoteza nguvu kazi ya vijana, vijana amkeni mfanye kazi, achaneni na mambo ambayo hayana tija katika maisha yenu, kwani matumizi ya dawa za kulevya ni hatari kwa afya yako,"amesisitiza Dkt. Mlondo.
Tags
Afya
Habari
Kimataifa
National Authority for the Campaign Against Alcohol and Drug Abuse (NACADA)
Shisha