DAR ES SALAAM-Wadau wanaotekeleza Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA) wametakiwa kuhakikisha mwongozo wa uratibu wa mpango huo unagusa sekta zote, ngazi zote pamoja na mifumo yote ya utawala, uongozi na utendaji ikiwemo sekta binafsi na wadau wote wa maendeleo.
Akifungua kikao cha Wadau hao chenye lengo la kupitia rasimu ya Mpango huo kwa Awamu ya Pili, Disemba 07, 2023, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameelekeza timu hiyo kuwashirikisha Viongozi wote kuanzia wa Serikali, makundi yote ya viongozi wa kisiasa na sekta binafsi ili kufanya utekelezaji.
Amebainisha kwamba, baadhi ya changamoto za Mpango wa Kwanza ilikuwa ni pamoja na baadhi ya mifumo kutotajwa hivyo mifumo hiyo kutowekeza juhudi za kutosha.
"Baadhi ya Kamati za MTAKUWWA ngazi za Mikoa, Wilaya, Kata na Vijiji hazikufanikiwa vizuri kutokana na changamoto ya mifumo kutokwenda pamoja wakati wa utekelezaji hivyo, mwongozo huu mpya uondoe mapungufu hayo ngazi zote," amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Awali, akimkaribisha Waziri kufungua kikao hicho, Mratibu wa MTAKUWWA kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Victor Nkya amesema wanaopitia rasimu ya Mpango huo ni Wizara za kisekta, Taasisi na Mashirika Binafsi wanaohusika na masuala ya wanawake na watoto kabla ya uzinduzi wa awamu ya pili.
Kwa upande wake Mwakilishi Mkaazi wa UNICEF Elke Wisch amewapongeza Wadau wote wa MTAKUWWA kwa kazi kubwa iliyofanyika katika awamu ya kwanza na kusisitiza uwajibikaji katika kuangalia changamoto zilizopo na kuzifanyia kazi.
Kikao hicho kimehusisha wadau kutoka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ikiwemo ICS, WHO, UNWOMEN, TANRAP, UNFPA, UNICEF, LSF na WFT. Wizara za Kisekta zilizoshiriki ni Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Waziri Mkuu, Katiba na Sheria, Elimu na Kilimo.