DAR ES SALAAM-Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imemfanyia upasuaji kwa njia ya matundu madogo mtoto mwenye umri wa miaka tisa ambaye alikua na tatizo la kumeza (Achalasia) tangu akiwa na miaka sita kutokana na mishipa yake ya fahamu ya koo la chakula kuharibika na kumfanya ashindwe kumeza kwa urahisi.
Upasuaji huo umefanyika ili kupunguza kizuizi kati ya umio (koo la chakula) na tumbo na kugawanya safu ya misuli kutoka kwenye umio hadi tumbo ili kumuwezesha mtoto huyo kumeza chakula kwa urahisi.
Bingwa Mbobezi wa Upasuaji Mfumo wa Chakula, Ini na Mbobezi wa Upasuaji wa Matundu Madogo kutoka MNH, Dkt. Kitembo Kibwana ambaye pia ameongoza timu nzima ya upasuaji huo amesema Achalasia ni ugonjwa ambao hufanya iwe vigumu kwa chakula na kioevu kupita kutoka koo la kumeza linalounganisha kinywa na tumbo (umio) ndani ya tumbo.
Dkt. Kibwana amesema, tatizo hili hutokana na mishipa kwenye umio kuharibiwa na mwili wenyewe (auto-immune) au baadhi ya maambukizi na kusabaisha umio kupooza na kupanuka kwa muda na hatimaye kupoteza uwezo wa kukamua chakula hadi tumboni na matokeo yake chakula hicho hujikusanya kwenye umio, wakati mwingine huchacha na kurudishwa hadi mdomoni kikiwa na ladha chungu.
Amewataka wananchi wenye changamoto ya kumeza (Achalasia) na wale wenye tatizo sugu la kucheua (Gastro-Esophageal Reflux Disease) kufika Hospitali ili kufanyiwa uchunguzi na kisha kupatiwa matibabu stahiki kwani huduma hiyo hutolewa kwa muda mfupi na kumruhusu mgonjwa ndani ya siku angalau mbili kwenda nyumbani kuendelea na shughuli zake.
“Mpaka sasa tumeweza kufanya upasuaji wa aina hii kupitia njia ya matundu madogo kwa wagonjwa wapatao 28 kwa ufanisi mkubwa zaidi ambapo kati yao, 23 walikuwa na tatizo la kumeza(Achalasia) na watano tatizo la kucheua,"amefafanua Dkt. Kibwana.