NA LWAGA MWAMBADE
IKIWA ni saa chache zimesalia kabla ya kuuaga mwaka 2023 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2024, neno la Mungu linasema kuwa, tumshukuru Mungu kwa kila jambo.
Rejea Biblia Takatifu katika kitabu cha 1 Wathesalonike 5:18..."Shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu."
Ni wazi kuwa, katika miezi 12 iliyopita katika maisha yetu ya kila siku huenda kuna mambo yalitufurahisha, lakini pia yapo ambayo yalituchefua na kutuvunja mioyo.
Lakini yote katika yote tunapaswa kumshukuru Mungu.Maisha yetu yanatakiwa yawe ya shukrani mbele za Mungu kila iitwapo leo, tunapotarajia kuiana safari nyingine ya miezi 12 yafaa tuendelee kumpa Mungu kipaumbele cha kwanza kabla na baada ya kufanya jambo lolote.
Mshairi wa kisasa, Lwaga Mwambande anasisitiza kuwa, mara zote Mungu huwa hasusiwi bali huwa anashukuriwa. Endelea;
1.Mungu huwa hasusiwi, bali anashukuriwa,
Pengine hufanikiwi, ni hasara waibiwa,
Ufanye kama Walawi, Mwenyezi wa kusifiwa,
Mwaka ndio wakatika, ashukuriwe Muumba.
2.Anakaa kwenye sifa, huyu wa kuabudiwa,
Hata kama wewe lofa, Mungu ni wa kusifiwa,
Wewe mzima hujafa, msifu umejaliwa,
Mwaka ndio wakatika, ashukuriwe Muumba.
3.Katika maisha yetu, muhimu kufanikiwa,
Siyo yale mambo yetu, ya mapesa kujaziwa,
Hayo hayafai katu, kama afya wazidiwa,
Mwaka ndio wakatika, ashukuriwe Muumba.
4. Kama wewe wapumua, ujue umejaliwa,
Angeweza kuamua, mbali ukafutiliwa,
Hilo kama walijua, unaye wa kusifiwa,
Mwaka ndio wakatika, ashukuriwe Muumba.
5.Mwaka mefika mwishoni, huu tuliojaliwa,
Wewe usiulaani, pale hujafanikiwa,
Shukuru Mungu mbinguni, uhai umejaliwa,
Mwaka ndio wakatika, ashukuriwe Muumba.
6.Wale waliofariki, yote wameshaishiwa,
Lakini wewe rafiki, kesho utafanikiwa,
Ndiyo maana ni haki, Mwenyezi kuinuliwa,
Mwaka ndio wakatika, ashukuriwe Muumba.
7.Huu na ubaya wake, yako uliyojaliwa,
Ule mema peke yake, tuone wafanikiwa?
Mabaya usiyachoke, mbele utafanikiwa,
Mwaka ndio wakatika, ashukuriwe Muumba.
8.Mungu tunakushukuru, uzima tumejaliwa,
Mbele iangaze nuru, tuweze kufanikiwa,
Mateso kama tanuru, tusije tukafikiwa,
Mwaka ndio wakatika, ashukuriwe Muumba.
Lwaga Mwambande (KiMPAB)