NA GODFREY NNKO
SHIRIKA la Taifa la Nyumba (NHC) limetoa msaada wa saruji tani 10 kwa Kikundi cha Wasioona Kigamboni kilichopo Halmashauri ya Manispaa ya Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Msaada huo umetolewa leo Desemba 28,2023 na kukabidhiwa na Afisa Uhusiano Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NHC, Yahya Cherehani kwa mwakilishi wa kikundi hicho, Salum Salum.
Amesema, msaada huo wenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 3.6 wameutoa baada ya kikundi hicho kuwasilisha ombi kwa shirika ili waweze kuanzisha mradi wao utakaowasaidia kujikwamua kiuchumi.
"Shirika la Taifa la Nyumba (NHC) tumefika hapa leo kutoa msaada wa saruji mifuko 200 (tani 10) kwa ajili ya Kikundi cha Wasioona Kigamboni.
"Msaada huu ulikuja kuombwa katika shirika letu kwa ajili ya kwenda kusaidia vijana hawa ambao walikuja wakitaka msaada utakaowaokoa katika maisha na kuwasaidia katika shughuli zao za kila siku."
Aidha,Cherehani amesema, shirika hilo linawatakia vijana hao kila la heri ili waweze kwenda kutekeleza kile ambacho wamekusudia kwa ajili ya kuyaendea malengo yao na kuzifikia ndoto zao.
"Msaada huu mkautumie kwa kusudi mlilokusudia ili muweze kuyafikia malengo yenu ya kujikomboa kiuchumi kwa ustawi wenu na jamii inayowazunguka,"amesisitiza Cherehani.
"Shirika la Taifa la Nyumba lina Sera ya Huduma kwa Jamii ambayo imelenga kusaidia jamii mbalimbali mahitaji muhimu, kupitia sera yetu tunasaidia watu wenye mahitaji maalumu wakiwemo vijana, wazee na wanawake.
"Sera hiyo pia inaliagiza shirika kusaidia sekta ya elimu, afya, watu waliopatwa na majanga mathalani janga kama lille lililotokea kule Hanang'."
Pia. Bw.Cherehani ametoa wito kwa jamii kuendelea kujitolea kusaidia jamii. "Wito wangu ni kwamba kama jamii ambayo inawajibika duniani hapa, tuna wajibu wa kuwasaidia watu ambao wana mahitaji maalum kwani sisi wenyewe kesho hatujui tutakuwa ni kina nani.
"Sisi kama tulivyo ni walemavu watarajiwa, unaweza ukaona umejisahau ukaona huko sawa sawa, lakini ipo siku ambayo utahitaji msaada kutoka kwa watu wengine, kwa hiyo watu mbalimbali ambao wana fursa katika jamii wasaidie watu wenye mahitaji katika jamii,"amefafanua Cherehani.
Mwakilishi
Mwakilishi wa kikundi hicho, Salum Salum akipokea msaada huo kwa niaba ya wenzake amesema kuwa, wanalishukuru shirika hilo kwa msaada huo ambao unakwenda kufanya jambo kubwa kwa ustawi bora wa uchumi wa kundi hilo la watu wasioona Kigamboni.
"Tunaishukuru NHC kwa msaada walioutoa, tunawaombea kwa Mwenyenzi Mungu mwingi wa rehema awape mengi zaidi ili waweze kuwasaidia wenzetu wengine wenye mahitaji maalumu katika jamii yetu nchini."
Kuhusu NHC
Shirika la Nyumba la Taifa lilianzishwa kwa Sheria ya Bunge Na.45 ya mwaka 1962.NHC baadae liliunganishwa na iliyokuwa Msajili wa Majumba kwa Sheria Na. 2 ya mwaka 1990 ambayo ilirekebishwa mwaka 2005 ili kulifanya shirika lijiendeshe lenyewe kibiashara.
Malengo ya shirika kwa mujibu wa Mpango Mkakati wake (2015/16-2024/25) ni pamoja na kuwa msimamizi mahiri wa miliki, kuimarisha uwezo wa kiuendeshaji na udhibiti.
Pia, kutumia kikamilifu rasilimali watu, kuwa kiongozi katika uendelezaji miliki, kuhuisha mikataba na mazingira ya kisheria na kujenga taswira ya shirika nchini.