DAR ES SALAAM-Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni Taasisi ya umma ya elimu ya juu ambayo imeanzishwa kwa sheria ya Bunge namba 17 ya mwaka 1992.
Chuo hiki kilianzishwa kwa malengo ya kuongeza fursa za elimu ya juu kupitia mifumo ya kutoa elimu kwa njia ya masafa, Huria na Mtandao kwa watu wote ambao wanapenda kujiendeleza kielimu na huku wanaendelea na kazi zao na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na hivyo kuwa vigumu kwao kujiunga na vyuo vya bweni.
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ni cha tatu kuanzishwa hapa nchini kufuatia wazo la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere.
Chuo Kikuu Huria cha Tanzania kinatekeleza majukumu yake kupitia sheria ya Vyuo Vikuu ya mwaka 2005, Charter na kanuni za chuo ya mwaka 2007, miongozo na taratibu za Tume ya Vyuo Vikuu ya Tanzania na sheria zote zinazosimamia elimu ya juu nchini.
Hivi karibuni kumekuwa na taarifa zisizo sahihi zikisambaa katika mitandao ya kijamii kuhusu udahili wa mwanafunzi Nape Moses Nnauye aliyedahiliwa katika shahada ya sheria ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania mwaka wa masomo wa 2022/2023.
Tunapenda kutoa ufafanuzi kwamba, mwanafunzi tajwa amedahiliwa kwa vigezo na sifa timilifu kama zilivyoainishwa kwenye Prospectus ya chuo ya mwaka 2022/2023 na katika kitabu cha muongozo wa udahili cha Tume ya Vyuo Vikuu cha mwaka 2022/2023 katika ukurasa wa 8-9 ambapo sifa namba tatu katika kitabu hicho ndiyo iliyotumika kumdahili mtajwa.
Miongozo hiyo ya udahili inapatikana kupitia www.out.ac.tz na www.tcu.go.tz. Mwanafunzi Nape Moses Nnauye ni mwanafunzi halali wa Chuo Kikuu Huria cha Tanzania ambaye amedahiliwa kwa kukidhi vigezo vyote stahiki.
Kwa ufafanuzi zaidi usisite kuwasiliana na chuo kupitia ofisi ya Naibu Makamu Mkuu
wa Chuo-Taaluma, Utafiti na Ushauri wa kitaalamu.