Paul Makonda atibua dili la makada CCM

NA DIRAMAKINI

KATIBU wa Itikadi,Uenezi na Mafunzo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amewataka makada ambao wameanza kuwasumbua wabunge na madiwani kuacha mara moja.
"CCM inatoa rai kwa watu walio na shauku ya kutaka majimbo na udiwani, sasa CCM inasema chokochoko zote ziachwe mara moja, wabunge wapewe nafasi ya kufanya kazi zao kama ulivyo utaratibu.

"Na katika hili nitoe mfano mimi niligombea ubunge Kigamboni nikashindwa na akateuliwa mgombea wa chama kwa kura za maoni na mimi nikakubali kushindwa na kuacha na sijawahi tena kwenda Kigamboni nimemuacha mbunge afanye kazi zake.

"Acheni kuwanyima utulivu viongozi wetu, waacheni wafanye kazi zao, acheni kuwachafua huko kwenye magroups ya Whatsapp.

"Tuwape ushirikiano kwa sababu kumuyumbisha maana yake unayumbisha utekelezaji wa Ilani ya CCM.Marufuku kufanya hivyo;

Ameyasema hayo leo Desemba 21,2023 wakati akizungumza na Wanahabari katika ofisi ndogo za chama zilizopo Lumumba jijini Dar es Salaam.

Vile vile amefafanua kuwa, Chama Cha Mapinduzi kinaanzisha utaratibu na utamaduni wa kutoa ripoti ya kila robo ya mwaka ya utendaji na utekelezaji wa Ilani yake ya Uchaguzi.

Amesema, ni ripoti ambazo zinatokana na Bajeti ya Mwaka ya Serikali, Maelekezo ya Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mahitaji ya wananchi pamoja na ziara mbalimbali za viongozi.

"Utamaduni huu utakuwa kila robo ya mwaka na tutakutana na kujadiliana na tutatoa nafasi kwa waandishi wa habari kuhoji nini wanataka kujua katika utekelezaji wa mambo mbalimbali ya kimaendeleo kwa Taifa letu la Tanzania."

Aidha, Makonda amesema, Chama Cha Mapinduzi kikiongozwa na Mwenyekiti wake Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kinatoa rai kwa Watanzania wote kushiriki kikamilifu katika kutoa maoni kuhusu Dira ya Maendeleo ya Taifa.

"Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan, amezindua na kutoa fursa kwa Watanzanja wote kutoa maoni katika hili, wataalamu, wafanyabiashara, wasomi.

"Mafundi ujenzi na watu wote yaani kila mwananchi ana wajibu wa kushiriki kutoa maoni ya kutaka kuona Tanzania inatakiwa kuwa ya namna gani.

"Watanzania tusisubiri mambo yaende vibaya baadaye tuseme viongozi wetu wanakosea, shirikini kutoa maoni ili tuijenge Tanzania yetu iliyo bora,"amesema Makonda.

Katika hatua nyingine, Makonda amewataka watendaji wa Shirika la Umeme nchini (TANESCO) kujitathimini, kwani hali ya umeme imezidi kuwa mbaya.

"Sisi sote tunaishi huko mtaani na tunaona tatizo hili lilivyo kubwa na ndio maana mimi kila siku ninasema kuwa nitasema kweli daima na hapa lazima TANESCO wajipime, kwani mara nyingi hatua zinachukuliwa kwa wanasiasa tu na hivi tutaangalia na uwajibikaji wa watendaji wetu,"amesema Makonda.

Makonda ameongeza kuwa, Chama Cha Mapinduzi kinaelekea kwenye chaguzi mwaka ujao na hakitamuonea mtu haya na hakitakuwa tayari kumvumilia mtu mzembe hivyo lazima wajipime kama kweli wanafanya kazi walizotumwa kwa ustawi wa wananchi na Taifa kwa ujumla.

"Chama hakifurahii hali ya umeme inayoendelea huko mtaani ni vema sasa watendaji walioko kwenye sekta ya umeme kuangalia ufanisi wa kazi zao na kujitathimini upya.

"Tatizo la umeme si la Waziri mwenye dhamana tu, bali ni la watalamu wote,"amesema Paul Makonda.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news