NA FRESHA KINASA
MBUNGE wa Jimbo la Musoma Vijijini mkoani Mara,Prof. Sospeter Muhongo amesema, Halmashauri ya Wilaya ya Musoma inatakiwa kutambua na kuthamini juhudi na michango ya maendeleo inayotolewa na wananchi katika miradi ya maendeleo jimboni humo.
Prof. Muhongo ameyasema hayo leo Desemba 22, 2023 Wakati akizungumza katika kikao Cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Mara ( RCC) kilichofanyika Ukumbi wa Uwekezaji uliopo ofisi ya mkoa huo katika Manispaa ya Musoma mkoani humo.
Amesema kuwa, katika Jimbo la Musoma Vijijini Prof. Muhongo ameendelea kushirikana na wananchi katika ujenzi wa miradi mbalimbali ikiwemo vyumba vya madarasa na maabara ambapo wananchi hujitolea kwa kutoa mjchango yao na nguvu kazi,lakini halmashauri haitambui wala kuthamini michango ya wananchi na mchango wake katika miradi ya maendeleo.
Ameongeza kuwa,halmashauri kushindwa kutambua na kuthamini michango yao si jambo zuri, lakini yeye hataacha kufanya kwa ajili ya maendeleo ya Wananchi wa Jimbo la Musoma Vijijini.
"Halmashauri ikiulizwa ina vyumba vingapi vya madarasa imejenga, wanataja idadi yote mpaka nilivyojenga mimi.
"Yaani hawatambui michango yangu na wananchi, lakini wanapotaja idadi wanasema ambavyo nimejenga na wananchi kwa michango yao na nguvu kazi wamejitolea " amesema Prof. Muhongo.
Ameongeza kuwa, wananchi jimboni humo wanapaswa kuthaminiwa na kutambuliwa pamoja na kuungwa mkono na halmashauri hiyo ili kuwapa moyo na nguvu ya kuendelea kujitolea.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Butiama ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Jumanne Sagini amesema Halmashauri ya Wilaya ya Musoma kushindwa kutambua mchango wa Prof. Muhongo na wananchi wake haitendi haki, kwani yeye katika Jimbo la Butiama amekuwa akitambuliwa na hivyo kuandikiwa barua ya shukrani pamoja na wote wanaojitolea kuchangia.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara,Mheshimiwa Said Mtanda ameitaka halmashauri hiyo kulipa umuhimu jambo hilo na kuendelea kutambua michango ya wananchi na mbunge katika maendeleo.