ZANZIBAR-Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imesema, imetambua rasmi uwepo wa wahudumu wa afya jamii wanaojitolea, sasa kuwa kada rasmi inayosaidia jamii kuhudumia kwenye sekta ya afya.
Sambamba na kukubali kuwapandisha hadhi kutoka wahudumu wa kujitolea (CHV) hadi kuwa wafanyakazi rasmi wa huduma za afya jamii kwenye sekta hiyo, CHW pamoja na kuwaongezea malipo mara tatu ya posho walizokuwa wakilipwa awali kutokana na utendajikazi wao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameyasema hayo viwanja vya Maishara, Wilaya ya Mjini Mkoa wa Mjini Magharibi alipozindua Mpango wa Wahudumu wa Afya Jamii kitaifa unaolenga kutoa uelewa mpana kwa jamii na kusaidia kwenye masuala ya afya.
Dkt. Mwinyi amesema, uzinduzi wa mpango huo ni ishara njema kwa wananchi kupata huduma zilizo bora zaidi nakueleza kuwa Zanzibar itakuwa nchi ya mwanzo duniani kuusimamia na kuutekeleza Kitaifa kwa kutumia mifumo ya kidigitali.
Rais Dkt. Mwinyi alieleza, Zanzibar itapiga hatua nyengine muhimu ya maendeleo kwenye sekta ya afya kutokana na mpango huo kuunganisha huduma za afya nje ya vituo vya afya sehemu zote wanazoishi wananchi.
Alifahamisha hatua hiyo kubwa ya maendeleo, ni uimarishaji wa huduma za afya ya jamii ambayo Serikali inajivunia kutoa fursa kwa mataifa mengine duniani kuja Zanzibar kujifunza.
Pia, Rais Dkt. Mwinyi alisifu juhudi za wahudumu hao kwa kazi kubwa wanayoifanya kutoka ngazi ya chini ya jamii kupita nyumba hadi nyumba ili kupata taarifa zinazosaidia kutoa huduma kwa ufanisi na kutumia teknolojia ya kisasa.
Halikadhalika Rais Dkt. Mwinyi alisema Serikali pia itawawezesha wahudumu hao kitaaluma ili kwenda sambamba na mahitaji ya Sekta ya Afya nchini.
“Naamini tukiendeleza huduma hizi katika ngazi ya jamii kwa wananchi, basi tutafanikiwa sana kwenye kutoa huduma bora za afya kwani hili ndio eneo la kwanza la utoaji huduma ni lazima kuweka nguvu kubwa hapa na kwengine katika eneo la kati na juu,” alifafanua Rais Dkt.Mwinyi.
Alisema, sekta ya afya inategemeana kutokana na ushirikiano wanaoupata kutoka kwa wahudumu hao kama wadau wengine wa afya, kutokana na ugumu na maumbile ya kazi za sekta hiyo.
Dkt. Mwinyi pia aliishauri jamii kutoa ushirikiano na kuwaungamkono wahudumu hao ili watekeleze vyema majukumu yao.
Akitoa ufafanuzi juu ya changamoto wanazokabiliana nazo wahudumu hao, Rais Dk. Mwinyi mbali na kuwaongezea kima cha malipo ya sehemu ya posho zao, pia aliwaahidi kuwaongezea vitendea kazi ikiwemo, kupatiwa simu mpya 3000 zilizotolewa na kampuni ya Tigo - Zantel pamoja na kuiagiza Wizara ya Afya kutowacheleweshea malipo wakati wa mafunzo.
Pia, Rais Dkt. Mwinyi, aliwahakikishia wahudumu hao kwamba Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya sekta ya afya na kuongeza vifaa vya kisasa vya utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Tutahakikisha huduma hizi zinawafikia wananchi wote kuanzia ngazi ya jamii kwenye msingi hadi ngazi ya rufaa,” alisema.
Aliongeza, Serikali inathamini mchango wa wahisani wakiwemo wadau wa maendeleo kwa jitihada zao zinazoimarisha huduma za afya nchini pamoja na ushirikiano wanaoutoa kwa kuendelea kuiungamkono Serikali.
Naye, Waziri wa Afya Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui, alisema wahudumu hao ni kiungo muhimu cha Wizara kutoka ngazi ya jamii, wanafanya kazi kubwa ya kuisaidia Serikali kutoa elimu na huduma za afya kwa wananchi.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya Zanzibar, Dkt. Amour Suleiman Mohammed alisifu mchango wa wahudumu hao kuihudumia jamii, ikiwemo kutoa elimu ya afya juu magojwa mbalimbali na kutoa uelewa mpana juu ya masuala ya mama na mtoto, kusaidia rufaa kwa wanajamii wenye matatizo ya afya au viashiria vya hatari dhidi ya magonjwa mbalimbali kwa kuwaunganisha kwenye vituo vya Afya kwa lengo la kupatiwa matibabu sahihi kwa wakati.
Pia, Dkt. Amour alieleza wahudumu hao wameibua matatizo ya afya na kuyaripoti sehemu husika, kuibua watoto walioasi chanjo na walikoseshwa kabisa pamoja na kuiunganisha jamii kwenye vituo vya Afya kwa kupunguza wimbi la mama wajawazito kujivungua majumbani pamoja na kupunguza vifo vya watoto na mama wajawazito.
Wahudumu wa Afya jamii, wanailinda jamii juu ya magonjwa ya miripuko yatokanayo na magonjwa yanayodhibitiwa kwa chanjo, kushiriki kampeni zote za kiafya kwenye shehia zao, ugawaji wa vifaa mbalimbali vya afya, kwenye jamii kama vile vyandarua, ugawaji wa dawa za minyoo na matende na mengine yanayofanana na hayo.
Mpango wa Kitaifa wa Wahudumu wa Afya jamii wenye kaulimbiu “Twende pamoja kusaidia wahudumu wa afya ngazi ya jamii kuelekea upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wote”, unalenga kuwatambua rasmi, wahudumu hao, kuwajengea uwezo kitaalamu na kuwawekea mazingira wezeshi ya utendaji kazi.
Umefanikiwa kusajili wanajamii asilimia 85, una jumla ya Wahudumu Afya Jamii 2300 Unguja na Pemba pia mpango huo unaungwa mkono kwa kushirikiana Serikali na wadau wa Maendeleo wakiwemo UNICEF, D- Tree na USAID.