Rais Dkt.Samia ataka mikakati endelevu ya kuwezesha wanawake kibiashara Afrika

DAR ES SALAAM-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan amewataka washiriki wa Kongamano la Pili la Wanawake katika Biashara ndani ya Eneo Huru la Biashara barani Afrika (AfCFTA) kujadili namna ya kuwezesha ushiriki imara wa wanawake katika biashara ndani ya Bara la Afrika.
“Ni muhimu sana katika kongamano hili mkaja na mipango mahususi ya hatua zinazotakiwa kuchukuliwa na kuimarisha ushirikiano kwa lengo la kuwa na ushiriki wenye tija kwa wanawake katika biashara unakamilishwa;

Kauli hiyo imetolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo Desemba 6, 2023 alipomuwakilisha Rais Dkt. Samia katika ufunguzi wa kongamano hilo linalofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa, kufanyika kwa kongamano hili kwa mara ya pili ni ishara tosha ya kuonyesha dhamira ya Nchi Washiriki wa Eneo Huru la Biashara Barani Afrika kukuza ushiriki wa wanawake katika biashara chini ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika.

“Kufanyika kwa makongamano haya kunatoa nafasi muhimu kwa wadau mbalimbali wa kuwawezesha wanawake kujadiliana na kutafuta ufumbuzi wa pamoja wa changamoto zinazokwamisha jitihada za wanawake katika biashara.”

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa, miongoni mwa faida za kuwa na Eneo Huru la Biashara la Barani Afrika ni kusaidia kuongezeka kwa biashara baina ya nchi za Afrika kutokana na nchi kuondoleana ushuru wa forodha.

“Faida Nyingine ni kushughulikia kwa pamoja vikwazo vya biashara visivyo vya kodi na kukuza uongezaji thamani wa malighafi zinazozalishwa ndani ya Afrika.”

Katika hatua nyingine Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa, Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imeanzisha Mfumo Rahisi wa Biashara (Simplified Trade Regime-STR) kwa ajili ya mauzo ya nje ya mipakani kwa ajili ya kuwasaidia wafanyabiashara wadogo kwa mipakani.

Mheshimiwa Majaliwa amesema, uamuzi wa kuazisha mfumo umeonesha dhamara ya jumuiya hiyo katika kutambua ushiriki mkubwa wa wanawake kwenye biashara ndogo ndogo za mipakani.

Naye Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji amesema kuwa, kampuni nane za Kitanzania zimeanza kufanya biashara na zimepeleka biashara mara 17 kwenye nchi tano zilizopo katika ndani ya Eneo Huru la Biashara Barani Afrika.

Amesema, baadhi ya kampuni hizo ni Ajat ltd, Mama Mia’s Soko na NatureRipe zote za nchini Tanzania na zinamilikiwa na wanawake.

“Tutaendelea kufanya kazi kwa karibu na sekta binfsi na kushughulikia kero zote ili tuendelee kuwainua wakawake.”

Kwa upande wake, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dkt. Doroth Gwajima amesema, uwezeshaji wanawake na vijana kiuchumi ni miongoni mwa vipaumbele vya Serikali ili kuleta usawa wa kijinsia na hivyo kufikia maendeleo jumuishi na endelevu.

“Katika kufikia adhima hiyo Serikali imeridhia na inatekeleza mkataba na maazimio ya kikanda na kimataifa ikiwemo mkataba wa Eneo huru barani Afrika ambao unatoa fursa za kiuchumi kwa wanawake na hata wanaume ndani ya bara letu,"amesema Waziri Dkt.Gwajima.

Wakati huo huo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mheshimiwa Albert Chalamila amewakaribisha na kuwahamasisha wageni kutoka nje ya nchi kujifunza lugha ya Kiswahili kwani kama hakitawafaa kwa matumizi ya sasa siku za mbeleni watakitumia.

Kongamano hili la siku tatu kuanzia  leo Desemba 6 hadi 8,2023 la wanawake katika Biashara chini ya Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika, ni kongamano la pili kufanyika nchini ambapo Kongamano la Kwanza lililofanyika tarehe 12-14 Septemba 2022 jijini Dar es Salaam ambalo lilihudhuriwa na washiriki wapatao 1060 kutoka nchi mbalimbali za Afrika wakiwemo viongozi wananwake katika ngazi mbalimbali. 

Kongamano hilo lililenga kuwakutanisha Viongozi Wakuu Wanawake, Mawaziri, Wanawake Wajasiriamali na wadau wengine ili kujadili, kutoa maoni, ushauri na mapendekezo ya kuwezesha uandaaji wa Itifaki kwa ajili ya kuwawezesha Wanawake na Vijana kushiriki kikamilifu katika biashara ndani ya AfCFTA.

Mafanikio makubwa yaliyotokana na Kongamano la kwanza la mwaka 2022 ikiwa ni pamoja na kufanikiwa kupata maazimio yaliyowezesha kuandaa na kukamilisha Rasimu ya Itifaki ya Wanawake na Vijana katika Biashara ndani ya AfCFTA ambayo kwa upande wa Tanzania iko katika hatua mbalimbali za kuridhiwa ili iannze kutumika nchini

Pamoja na kufanikiwa kwa itifaki hiyo, Kongamano hilo lilitoa njia sahihi za kutatua vikwazo na changamoto mbalimbali zinazowakabili wanawake na vijana katika biashara ili kuwawezesha kushiriki kikamilifu katika biashara barani Afrika, ikiwa ni pamoja na upatikanaji mdogo wa fedha, taarifa za masoko, pembejeo, matumizi ya teknolojia, masoko, uwezo mdogo wa kufuata viwango na mahitaji mengine ya kisheria

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news