DAR ES SALAAM-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameiagiza Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kushirikiana na Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuendelea kufunga mtandao katika vijiji vyenye umeme ili kuwawezesha wanafunzi kufanya mitihani ya masomo ya sayansi kwa mtandao.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akivuta kitambaa pamoja na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Profesa Adolf Mkenda kuzindua mnara wa kumbukumbu ya miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) kwenye hafla iliyofanyika katika Ofisi za Baraza hilo Kijitonyama Jijini Dar es Salaam tarehe 16 Desemba, 2023.
Rais Samia ametoa maagizo hayo leo wakati wa hafla ya kilele cha Maadhimisho ya Miaka 50 ya Baraza la Mitihani la Taifa (NECTA) iliyofanyika katika Ofisi za Baraza hilo.
Aidha, Rais Samia amesema serikali imefanya uwekezaji kwenye TEHAMA ambao umeimarisha utendaji wa Baraza na kuongeza matumizi ya teknolojia katika usajili wa watahiniwa, uchapaji na usahihishaji wa mitihani na uchakataji wa matokeo.
Rais Samia pia amesema Serikali itaendelea kuijengea uwezo NECTA na walimu iili kuhakikisha ufundishaji, usomeshaji na utahini unafanyika kwa umahiri mkubwa kuwawezesha watahiniwa kumudu mahitaji ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Vile vile, Rais Samia ameitaka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia pamoja na NECTA kutafuta mkakati wa kushughulikia changamoto ya udanganyifu wa mitihani.
Aidha, Rais Samia pia amelitaka Baraza la Mitihani kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kuendana na shabaha ya sera ya elimu hususan katika upimaji wa umahiri.
Rais Samia amesema serikali itaendelea kuimarisha utendaji wa Baraza kulingana na mazingira mapya ya kiteknolojia na kushirikiana na Baraza hilo ili lifikie malengo ya muda mrefu ya kuweka mitambo ya kisasa ya uchapaji kadri uwezo utakavyoruhusu.