Rais Dkt.Samia kushiriki COP28 UAE

DUBAI-Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan atashiriki katika Mkutano wa 28 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi.
Mkutano huo umeanza tarehe 30 Novemba hadi 12 Desemba 2023, Dubai katika Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo utahudhuriwa na washiriki zaidi ya elfu sabini kutoka nchi takribani 190.

Ujumbe wa Tanzania utashirikisha Mawaziri, Makatibu Wakuu, Mabalozi, Viongozi na Watalaamu kutoka Wizara za Kisekta, Idara za Serikali, Mashirika ya Umma, Vyuo Vikuu, Sekta Binafsi, Asasi za Kiraia, Vijana na Wanahabari kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Kaulimbiu ya Mkutano huo ni UNITE. ACT. DELIVER. Kitaifa kaulimbiu ni Kuimarisha Kilimo Himilivu na Uchumi wa Bluu katika Kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.

Lengo la kauli mbiu ni kutoa msisitizo katika matumizi ya teknolojia na mbinu bora zinazozingatia changamoto za mabadiliko ya tabianchi, ili kuongeza tija katika uzalishaji, mnyororo wa thamani wa mazao na masoko.

Vile vile, kauli mbiu inalenga kujenga uwezo wa kuhimili athari za mabadiliko ya tabianchi katika kukuza uchumi wa buluu na kuchochea maendeleo endelevu.

Wakuu wa Nchi na Serikali wanachama wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi watahutubia katika Mkutano huo, ambapo Mheshimiwa Rais Samia atakuwa mzungumzaji wa 11 miongoni mwa Wakuu wa Nchi na Serikali takriban 160 wanaoshiriki Mkutano huo.

Sambamba na kuhutubia Mkutano huo, Tanzania imeandaa na itakuwa mwenyeji wa Mikutano Mikuu Mitatu ya Pembezoni (High-Level Side Events) inayohusu Nishati Safi ya Kupikia, Kilimo Endelevu, na Uchumi wa Buluu.

Katika Mkutano unaohusu nishati safi ya kupikia, Mheshimiwa Rais ataongoza viongozi wenzake kutoka nchi mbalimbali duniani na taasisi za kimataifa kuzindua Programu ya Kuwakomboa Wanawake wa Afrika Kupitia Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (African Women Clean Cooking Support Programme - AWCCSP).

Programu hiyo inalenga kuhamasisha matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kukabiliana na changamoto za afya, mazingira, uchumi na kijamii ambazo huathiri zaidi wanawake na watoto. Kutokana na kwamba wanawake hutumia muda mrefu kutafuta kuni, programu hii itawasaidia kupata muda wa kutosha kushiriki kwenye shughuli za maendeleo.

Hali kadhalika, Mheshimiwa Rais atashiriki katika mikutano ya uwili na viongozi wa serikali za nchi mbalimbali pamoja na mashirika ya kimataifa kwa lengo la kuimarisha mahusiano baina ya Tanzania na nchi hizo pamoja na mashirika husika.

Mheshimiwa Rais pia atashuhudia uwekaji saini hati nne za makubaliano baina ya Serikali za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Umoja wa Falme za Kiarabu kuhusu ajira; ushirikiano baina ya Kituo cha Uhusiano wa Kimataifa cha Dkt. Salim Ahmed Salim na Chuo cha Diplomasia cha Dkt. Anwar Gargash cha Umoja wa Falme za Kiarabu; ushirikiano katika masuala ya usalama na mapambano dhidi ya ugaidi; na ushirikiano katika sekta za elimu, sayansi na ufundi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news